Yanga yaendelea kugawa dozi nzito

Muktasari:
- Yanga ilipata ushindi huo uliokuwa wa 26 kwa msimu huu kupitia 29 ilizocheza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar na kuiacha igande kileleni ikiwa na pointi 79 na mabao 81, huku yenyewe ikiruhusu 10 ikiwa ndio yenye ukuta mgumu.
WATETEZI wa Ligi Kuu Bara, Yanga imeendeleza ubabe ikisaka taji la msimu wa nne mfululizo kwa kuifumua Dodoma Jiji kwa mabao 5-0, ikiwa ni mechi ya 10 kushinda katika ligi hiyo ikisaliwa na mechi moja ya kufungia msimu dhidi ya watani wao wa Jadi, Simba ilishinda pia 1-0 jioni hii.
Yanga ilipata ushindi huo uliokuwa wa 26 kwa msimu huu kupitia 29 ilizocheza kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar na kuiacha igande kileleni ikiwa na pointi 79 na mabao 81, huku yenyewe ikiruhusu 10 ikiwa ndio yenye ukuta mgumu.
Katika mechi ya leo, hadi inamaliza kipindi cha kwanza, Yanga iliyopumzisha baadhi ya mastaa muhimu ilitoka mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kiungo mshambuliaji Clatous Chama dakika ya nne tu ya mchezo akitengenezewa nafasi hiyo na mshambuliaji Clement Mzize.
Kipindi cha pili wenyeji walikuja na moto na kuongeza mabao menginekupitia kiungo Duke Abuya aliyekwamisha la pili dakika ya 50 akimalizia asisti ya Chama, kufuatia shambulizi kali kwenye lango la Dodoma kabla ya .beki Ibrahim Bacca kufikisha bao la tano msimu huu kwa kufunga chuma ya tatu.
Bacca alifunga bao hilo akimalizia mpira uliopigwa na Maxi Nzengeli ikitokana na mpira wa kona kuzalisha bao hilo.
Ni kama ilikuwa mechi ya aina moja ambapo sio tu wageni walishindwa kufunga bao lolote, ilishindwa hata kupiga shuti lililolenga lango wakati wenyeji wakipiga sita na kutumia matatu kufunga mabao yao kati ya hayo.
Wakati mchezo huo ukielekea mwisho, Dodoma ikajikuta inaruhusu bao la nne dakika ya 90+2, baada ya beki Joash Onyango kujifunga wakati anapambana kuzuia shuti la Farid Mussa aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Chadrack Boka
Yanga ikaandika bao la tano kupitia Nzengeli akimalizia shuti kali lililopigwa na Jonathan Ikangalombo likihitimisha ushindi wao wa mabao 5-0.
Katika mechi ya leo, Yanga iliwapumzisha mastaa kipa namba moja Djigui Diarra nafasi yake ikichukuliwa na Aboutwalib Mshery, beki wa kulia Israel Mwenda akimuachia nafasi Kibwana Shomari.
Wengine ni viungo Khalid Aucho na Mudathir Yahya ambao walilazimika kukosa mchezo huo kutokana na kufikisha kadi tatu za njano na nafasi zao kuchezwa na Abuya na Salum Abubakar 'Sure Boy' na kuendeleza rekodi nzuri ya Yanga mbele ya Dodoma Jiji iliyojikuta ikimaliza nafasi ya 12.
Katika mechi nyingine Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar lililowekwa kimiani na Steven Mukwala dakika ya 17, huku Azam ikitakata ugenini dhidi ya Fountain Gate kwa mabao 3-2, Pamba ikilazimishwa sare ya 1-1 na KMC na Coastal Union ikilazimishwa sare kama hiyo na Tabora United.
Mechi nyingine ilishuhudia Singida Black Stars ikilazimisha sare ya 3-3 na Tanzania Prisons, huku Namungo ikishinda 5-0 mbele ya KenGold na Mashujaa na JKT Tanzania zilishindwa kufungana.
Matokeo hayo yameifanya Fountain Gatre na Tanzania Prisons sasa kuangukia katika mechi za paly-off ikisaka wa kucheza na Stand United ya Ligi ya Championships. Timu inayopoteza mechi hiyo ndiye atakayecheza na Stand na timu ya Ligi Kuu ikifungwa itashuka kuungana na KenGold na Kagera Sugar na Stand kupanda Ligi Kuu kuzifuata Mtibwa Sugar na Mbeya City zilizopanda mapema.