Prime
Rafiki yetu Antony, mtego wa Kibrazili unaotembea?

Muktasari:
- Msimu wake wa mwisho kabla ya kwenda Manchester United akiwa na Ajax pale Uholanzi alifunga mabao 12 na kutoa pasi za mabao 11. Nani asingemtamani Antony? Nasikia klabu nyingi zilimtaka. Arsenal yangu pia ilimtaka.
ANTONY? Ndio. Amekaa kimitego sana. Namzungumzia huyu rafiki yetu wa Manchester United aliyepelekwa kwa mkopo kwenda Real Betis ya Hispania. Namtafakari tena na tena na tena.
Msimu wake wa mwisho kabla ya kwenda Manchester United akiwa na Ajax pale Uholanzi alifunga mabao 12 na kutoa pasi za mabao 11. Nani asingemtamani Antony? Nasikia klabu nyingi zilimtaka. Arsenal yangu pia ilimtaka.
Erik Ten Hag ambaye alikuwa kocha wa Antony kule Ajax kwa kutumia uhusiano wake wa karibu na Antony akafanikiwa kumnasa kumpeleka Manchester United. Mashetani Wekundu walitoa Pauni 80 milioni kwa ajili ya kumnasa Bwana Antony. Hii ina maana alikuwa mchezaji wa tatu ghali kwa United.
Kwa kule Uholanzi aliweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi kuuzwa kutoka Ligi Kuu Uholanzi. Na pia hapo hapo ilimaanisha kwamba alikuwa mchezaji ghali zaidi kuuzwa na chuo cha soka cha Ajax. Ukweli ni kwamba Ajax walilamba bingo.
Mechi ya kwanza tu Bwana Antony akatupia dhidi ya Arsenal. Watu wakaona ‘mchezaji ndio huyu’. Mechi ya pili akatupia dhidi ya Man City. Baada ya hapo Antony akaanza kunyanyua mguu mmoja na kuupunga juu ya mpira kisha anapokonywa.

Baada ya hapo usingeweza kujua lengo la Antony kuwepo uwanjani. Manchester United wakajifariji kwamba Antony alihitaji muda kuzoea Ligi Kuu England. Muda gani sasa? Hata sehemu ya kupiga pasi rahisi Antony alijaribu kupiga chenga zisizo na tija.
Mbele ya lango hakuwa na malengo yoyote. United walimvumilia tena na tena mpaka walipohisi kwamba wamepigwa na Ajax. Kadri siku zilivyokwenda mbele ndivyo walivyothibitisha kwamba walikuwa wamepigwa na Ajax.
Wakati unapotafakari kwanini Manchester United waliamua kumfukuza Ten Hag unapata majibu mawili. Kwanza timu ilikuwa inafanya vibaya. Lakini pili kwa kuwatia hasara ya kumchukua mchezaji kama Antony kwa kiasi kile cha pesa.
Kwanini asingemchukua Mohamed Kudus ambaye alikuwa naye palepale Ajax na badala yake akaamua kumchukua Antony? Ukiangalia ambacho Kudus alipeleka West Ham United ni tofauti kabisa na kile ambacho Antony alipeleka Old Trafford.
Mfano, Antony aliwahi kukaa mwaka mzima bila kufunga bao Old Trafford. Kweli huyu ni Mbrazili wa taifa moja na Ronaldo de Lima, Romario, Ronaldinho, Rivaldo na wengineo? Kwamba alikuwa amefikia hadhi ya kucheza timu kubwa Ulaya?

Baadaye maji yaliwafika shingoni Manchester United. Wakaamua kumpeleka kwa mkopo Real Betis. Hapa ndipo Antony aliporudia mitego yake ya Ajax. Hapa ndipo Antony ameanza kuwatamanisha tena vigogo.
Alirudia tena moto wake uleule wa Ajax. Jaribu kufikiria. Akiwa na Manchester United alicheza mechi 96 na kufunga mabao 12 tu, lakini akiwa na Betis ndani ya mechi 26 tu alifunga mabao tisa. Mabao matatu tu nyuma ya yale aliyofunga katika maisha yake yote Old Trafford.
Na kwa jumla Antony amehusika katika mabao 14 ya Betis msimu huu. Ni zaidi ya alivyohusika na mabao yote ya Old Trafford katika maisha yake pale. Huu ni mtego mwingine ambao unaweza kumnasa mtu. Unaweza kujidanganya kwamba labda Old Trafford walikuwa hawajui kumtumia Antony.
Kuna mwezi ambao pale La Liga Antony aliwahi kuteuliwa kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa mwezi. Ungeweza kufikiria kama jambo hilo lingemtokea England? Kule La Liga Antony aligeuka lulu kiasi kwamba hata wakubwa walianza kumfikiria.
Hapa kuna hisia tofauti. Ligi Kuu Hispania ni nyepesi kuliko ya England? Sidhani. Tunaweza kutofautiana wengi. Mbona kina Fernando Torres, Jose Antonio Reyes na wengineo walikuja England na wakatesa moja kwa moja?
Mbona Lionel Messi akiwa na Barcelona amezifunga timu za England mabao mengi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko timu za mataifa mengine? Kwamba Messi asingeweza kung’ara England akiwa katika ubora wake ni wazo la kipuuzi.
Na sasa Betis wanataka kumbakisha Antony jumla. Hata hivyo, wanataka Manchester United wamuuze Antony kwa bei ya hasara. Pauni 35 milioni. Kutoka Pauni 85 milioni hadi Pauni 35 milioni ni hasara ya Pauni 50 milioni. Sidhani kama United wanaweza kumsamehe Ten Hag kwa hili.

Nini kinaweza kutokea mbele? Kuna kitu kinaniambia kwamba labda Antony anaweza kufanya kama kile ambacho Kevin de Bruyne na Mohamed Salah waliwahi kufanya pale Chelsea. Walitua Chelsea, lakini hawakuonyesha thamani zao.
Baadaye De Bruyne akaenda zake Werder Bremen kwa mkopo kisha Wolfburg wakamchukua jumla. Akatesa vilivyo katika Ligi Kuu Ujerumani kisha akatua Manchester City na kutamba kiasi cha kuwa kiungo bora mshambuliaji Ulaya. Chelsea walijuta.
Mo Salah naye aliondoka kichwa chini pale Stamford Bridge akaenda Fiorentina kwa mkopo, kisha Roma kwa mkopo baadaye Roma ikamchukua jumla akaonyesha makali yaliyopitiliza pale Italia akajikuta anaangukia Liverpool akiwa mchezaji staa. Chelsea walikuja kujuta.
Najiuliza kama Antony anaweza kuwa hivi lakini moyo wangu unasita. Wenzake walikosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Chelsea, lakini yeye alikuwa anapewa nafasi. Wenzake walikuwa wadogo walipokwenda Chelsea, lakini yeye amekwenda Manchester wakati amekomaa.
Baada ya kutushtua kidogo pale Betis kiasi cha kuwapeleka katika fainali za michuano midogo ya Europa inayoitwa ‘Conference’, Antony anaweza kufuata nyayo za kina Salah na De Bruyne? Bado akili yangu inagoma. Nadhani amekaa kimitego zaidi. Ukiingia kichwa kichwa kama Manchester walivyoingia wakati ule unaweza kulipukiwa na bomu.