PUMZI YA MOTO: Tuzo za soka Tanzania zimejaa ukakasi mtupu
Muktasari:
- Baada tu ya kutangazwa, mijadala ikawa mingi sana kutoka kila sehemu, kwa mashabiki hadi wachambuzi.
MOUSSA Camara, kipa wa Simba, alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo wa Dabi ya Mzizima kati ya Azam FC na Simba.
Baada tu ya kutangazwa, mijadala ikawa mingi sana kutoka kila sehemu, kwa mashabiki hadi wachambuzi.
Hoja kubwa kwao ilikuwa moja, inawezekana vipi Camara akawa mchezaji bora wa mechi ilhali mechi yenyewe haikumpa pilikapilika zozote?
Hadi mpira unaisha, Camara alidaka shuti moja tu, tena la dakika ya 84, muda ambao tayari mchezaji bora wa mechi alikuwa ameshapatikana, kwa sababu nyota wa mchezo wa mechi ile alitangazwa katika dakika ya 86, yaani dakika mbili baada ya Camara kudaka shuti pekee ndani ya dakika 90.
Kimsingi katika ule mchezo, Camara alipigiwa mashuti mawili, la kwanza ni lile la Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambalo lilimshinda na kugonga mwamba.
La pili ndilo hilo la dakika ya 84 lililopigwa na Cheikna Diakite ambalo lilikuwa jepesi mno.
Matukio haya mawili hayawezi kumfanya kipa kuwa mchezaji bora wa mechi; kwa vigezo vyote, kwa duniani na hata mbinguni.
Ndiyo maana hata kocha wa Simba, Fadlu Davids, alishangaa.
“Ilikuwa mara ya kwanza kuona kipa anakuwa mchezaji bora wa mechi bila kuzuia michomo mikali mitatu au minne,” alisema kocha huyo kutoka Afrika Kusini.
Nyota wa Mchezo hupatikana kwa kutimiza vyema majukumu yake ya msingi halafu anafanya na ziada.
Kwa kipa, majukumu yake ya msingi ni kudaka, au kuokoa hatari langoni mwake na ndio maana anaitwa mlinda lango.
Majukumu mengine kama kupiga pasi nzuri au kuhusika vizuri kwenye kuanzisha mashambulizi, ni ya ziada.
Baadhi ya watu wanaotetea tuzo ya Camara wanasema eti alipiga pasi nzuri.
Kwanza hakukuwa na pasi yoyote ya maana aliyopiga kuweza kumfanya ashinde tuzo.
Lakini la pili, hata kama alipiga hizo pasi lakini hiyo haitoshi kumfanya awe mchezaji bora wa mechi kwa sababu mchezaji bora wa mechi hapatikani kwa kigezo cha kufanya majukumu ya ziada pekee bila ya yale yake ya msingi.
Kwenye Kombe la Dunia la 2018, Ufaransa walikuwa na mshambuliaji aliyeitwa Olivier Giroud.
Alicheza mechi zote hadi timu yake kuwa Mabingwa wa Dunia.
Lakini hakufunga hata bao moja na wala hakutoa hata pasi moja ya bao.
Kama mshambuliaji, hakutimiza majukumu yake ya msingi.
Lakini alifanya mambo mengi sana ya ziada.
Aliongoza kwa kupokonya mipira katika eneo la ushambuliaji.
Aliongoza kwa kuipata mipira ya juu. Aliongoza kuingilia pasi za wapinzani.
Hayo yote aliyafanya vizuri sana katika eneo lake la ushambuliaji.
Lakini hayo hayakuwa majukumu yake ya msingi kwa hiyo hakupata tuzo yoyote.
Kumpa tuzo kipa kwa sababu ya kupiga pasi ni kumkosea, yaani unamhukumu kwa majukumu yasiyo ya kwake.
Kinyume chake ni kwamba kipa anaweza akaokoa mashuti mengi na ya hatari, lakini akanyimwa tuzo kwa sababu hakupiga pasi nzuri.
Na huu ndiyo umekuwa utamaduni wa tuzo za Tanzania.
Tuzo zimekuwa zikitolewa aidha kwa ushawishi au hisia lakini siyo vigezo.
Hata tuzo za meneja bora wa uwanja.
Utakuja meneja wa uwanja fulani wa mikoani akashinda tuzo ya mwezi, lakini katika mwezi huo uwanjani kwake hakukuwa na maji vyooni na hata baadhi ya vyoo havifanyi kazi.
Mfano wa uwanja wa aina hii ni Sokoine Mbeya.
Vyoo pekee vinachokuwa vina na vyenye maji ni vya jukwaa la VIP.
Vile vyoo za mzunguko ambavyo vipo upande wa kulia wa jukwaa la VIP, siku zote vimeziba na havina maji.
Lakini utakuta meneja wa uwanja anashinda tuzo ya meneja bora.
Tatizo la kutokuwa na maji vyooni hata Uwanja wa Mkapa hutokea mara kadhaa wakati wa mechi.
Lakini kwa mikoani hili ni tatizo sugu. Utakuta hata miundombinu ya maji hakuna, kwa hiyo vyooni kunakuwa na ndoo za maji ambazo hazina makopo ya kuchotea au maji yameisha kwenye ndoo na hayawekwi mengine.
Halafu utasikia meneja wa huo uwanja ameshinda tuzo ya meneja bora wa mwezi.
Miaka inapita lakini suala la tuzo halipiti, liko pale pale.
Unaweza kudhani waandaaji wa tuzo hawana vigezo vya kitaalamu vya kuwaongoza kupata washindi wanaostahili.
Fainali ya Kombe la Shirikisho la msimu uliopita kati ya Yanga na Azam, mchezaji bora wa mechi akawa Ibrahim Bacca katika mchezo ambao kipa wa Azam, Mohamed Mustafa alifanya maajabu.
Kila mtu alishangaa, hata Bacca mwenyewe.
Hizi tuzo za mchezaji bora wa mechi ambazo zimeanza msimu huu pia zimekuwa na malalamiko tangu mwanzo.
Rejea tuzo ya mchezaji bora wa mechi kati ya Kagera Sugar na Yanga, Nassor Kapama wa Kagera Sugar.
Ilibidi mamlaka kumuondoa kwenye orodha yao yule mtu aliyepewa majukumu ya kuchagua mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Mexime, aliwahi kuhoji kama tuzo hizi ziliwekwa maalumu kwa ajili ya timu iliyo nyumbani.
Baada ya hapo ndipo wachezaji wa timu iliyo ugenini nao wakaanza kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi.
Tumekuwa tukitoa hizo tuzo kwa muda mrefu na matarajio ni kwamba tungekuwa tayari tumeshajifunza vya kutosha na kutoa ufafanuzi pale panakuwa na ukakasi kwenye jambo lolote.
Lakini sisi sisi tunafanya hizi tuzo kama jambo fulani la kiroho ambalo waumini wanapaswa kulichukua kama lilivyo.
Kila mtu anaangalia mpira na anaona wachezaji -- aliye bora anajulikana tu.
Wazo la tuzo ni jema sana lakini tuliboreshe kwa kuwa na vigezo stahiki vitakavyowaongoza majaji ili kuepuka malalamiko yasiyo ya msingi.