Prime
Camara, Hamza waibua kipengele Simba

Muktasari:
- Pambano la Simba na Yanga limepangwa kupigwa Juni 15 Kwa Mkapa baada ya awali kushindwa kufanyika Machi 8 mwaka huu baada ya kuahirishwa kiutata na Bodi ya Ligi ikichangiwa zaidi na madai ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho.
WAKATI bado kukiwa na sintofahamu ya Dabi ya Kariakoo kama itachezwa au haichezwi Juni 15, nyota watatu wa Simba, kipa Moussa Camara na mabeki Shomari Kapombe na Abdulrazak Hamza wameibua kipengele ikiwa ni wiki kama moja na ushei kabla ya siku ya pambano hilo.
Pambano la Simba na Yanga limepangwa kupigwa Juni 15 Kwa Mkapa baada ya awali kushindwa kufanyika Machi 8 mwaka huu baada ya kuahirishwa kiutata na Bodi ya Ligi ikichangiwa zaidi na madai ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho.
Hata hivyo, Yanga imetishia kutoicheza mechi hiyo kwa madai ya kutoridishwa na kuahirishwa kwa pambano la awali, lakini kama mechi hiyo itapigwa Juni 15 basi Simba huenda ikawakosa wachezaji watatu kwa mpigo wa kikosi cha kwanza akiwamo kipa Camara.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema, Camara ambaye ni kipa tegemeo wa timu hiyo bado ni majeruhi tangu alipoumia katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida Black Stars ambapo Mnyama alipoteza kwa mabao 3-1 na kuondoshwa michuanoni.

Mbali na Camara anayemiliki clean sheet 17 hadi sasa katika Ligi Kuu akiwa kinara mbele ya Diarra Djigui wa Yanga mwenye 15, pia Shomari Kapombe naye anadaiwa ni majeruhi na ana wiki mbili za kurejea uwanjani, wakati dabi ikisaliwa na siku kama tisa tu kuanzia sasa.
“Camara na Kapombe bado ni majeruhi, japo kujua wanaweza kurejea lini tena kikosini ni suala la daktari wa timu, lakini ni kati ya wachezaji walio katika hatihati ya kuicheza Dabi ya Juni 15, sambamba na beki Abdulrazack Hamza ambaye alionyeshwa kadi tatu za njano zinazomnyima kucheza mechi moja,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba.
Hamza ni mmoja ya nguzo imara ya mabeki wa kati wa Simba, akishirikiana na kina Chamou Karaboue na Fondoh Che Malone ambao wameifanya timu hiyo kuwa imara ikifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.
Daktari wa Simba Edwin Kagabo, alipotafutwa jana kutoa ufafanuzi juu ya taarifa za Kapombe na Camara, hakuweza kutoa majibu kwa maelezo alikuwa chumba cha upasuaji akimhudumia mgonjwa.
“Nipo theatre kwa sasa,” alijibu kwa ujumbe mfupi wa maneno na hakupatikana tena hewani.

Kwa Hamza kadi ya tatu iliyomtibulia kukipiga dabi kama itachezwa ni ile aliyoonyeshwa katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) ambapo Mnyama alitolewa kwa mabao 3-1.
YANGA WAWILI
Wakati Simba ikiwa na hatihati ya kuwa na nyota watatu, kwa upande wa Yanga kuna taarifa itawakosa wachezaji kama watano akiwamo Stephane Aziz Ki ambaye amekuwa na kismati ya kuifunga Simba katika mechi za dabi, aliyeuzwa Wydad Casablanca ya Morocco.
Pia itamkosa beki wa kulia, Yao Kouassi ambaye kwa muda mrefu ni majeruhi akiwa amerejea kutoka Tunisia alikoenda kufanyiwa upasuaji wa goti.
KIPENGELE CHA DABI
Zikiwa zimebaki siku tisa tu kufikia Dabi ya Kariakoo kati ya wenyeji Yanga na Simba iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Juni 15, timu hizo zina rekodi tofauti kwa mechi zao tano zilizopita hivi karibuni.
Mechi hiyo ya raundi ya pili awali ilitakiwa kupigwa Machi 8, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, japo ilishindikana kwa kile kilichoelezwa makomandoo wa Yanga kuizuia Simba isifanye mazoezi na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), kuiahirisha rasmi mechi hiyo.

Timu hizo zinakutana tena baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Oktoba 19, 2024, ambayo Yanga ilishinda kwa bao 1-0, ingawa safari hii miamba hiyo inaenda kukutana na rekodi tofauti za mashindano mbalimbali, jambo linalosubiriwa kuona ni kitakachojiri.
Katika mechi tano zilizopita, Yanga imekuwa tishio kitakwimu tofauti na wapinzani wao Simba, ambapo kikosi hicho Wananchi kimeshinda zote zikiwa ni za mashindano tofauti, huku safu ya ushambuliaji ikiwa pia hatari zaidi kutokana na idadi kubwa ya mabao.
Yanga imecheza mechi tano za mashindano mbalimbali, ambapo tatu kati ya hizo ni za Ligi Kuu Bara ikiifunga Azam FC mabao 2-1, ikaichapa Fountain Gate 4-0, huku ya mwisho ni ushindi wa 3-0, dhidi ya kikosi cha ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo FC.
Mechi mbili nyingine ni za Kombe la Shirikisho (FA), ikianza na kuichapa Stand United ‘Chama la Wana’, mabao 8-1, katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, kisha nusu fainali ikaitandika maafande wa JKT Tanzania 2-0 na kutinga fainali.
Katika mechi hizo tano zilizopita kwa Yanga, timu hiyo imekuwa na balansi nzuri kuanzia safu ya ushambuliaji hadi ile ya mabeki, ambapo washambuliaji wa kikosi hicho wamefunga mabao 19, huku ikiruhusu pia nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Kwa upande wa Simba, katika mechi tano zilizopita imeshinda mbili, ikipoteza pia mbili na kutoka sare moja, ambapo kati ya hizo ilizoshinda zote ni za Ligi Kuu Bara, ikiifunga KMC mabao 2-1, kisha kuichapa pia Singida Black Stars bao 1-0.
Mechi nyingine mbili ni za fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya RS Berkane ya Morocco, ambapo ilianza ugenini kwa kichapo cha mabao 2-0, kisha marudiano kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar ikatoka sare ya bao 1-1.
Mechi nyingine moja ambayo ni ya mwisho kwa timu hiyo kucheza, ilikuwa ya hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), ambapo kikosi hicho kilichapwa mabao 3-1, na Singida Black Stars, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara.
Timu hiyo imekuwa haina uwiano mzuri wa kufunga kwani imefunga mabao matano tu, ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kwa kila mechi kati ya hizo tano zilizopita, huku safu ya mabeki ya kikosi hicho ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.
Licha ya hayo pia, ila tangu mara ya mwisho Simba ichapwe bao 1-0 na Yanga, Oktoba 19, 2024, timu hiyo imekuwa na rekodi nzuri katika Ligi Kuu Bara, kwa sababu hadi sasa imefikisha jumla ya mechi 21, mfululizo bila ya kuonja kichapo.
Katika mechi hizo zote 21, ilizocheza Simba tangu mara ya mwisho ilipochapwa na Yanga, imeshinda 19, huku mbili ikitoka sare, ikianza ya bao 1-1, dhidi ya Fountain Gate, Februari 6, 2025 na ya mabao 2-2, mbele ya Azam FC, Februari 24, 2025.
Rekodi pia zinaonyesha, mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga katika Ligi Kuu ilikuwa ni ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na Henock Inonga katika dk2 na Kibu Denis dk32, Aprili 16, 2023, hivyo, kuanzia hapo haijashinda tena hadi leo.
Kwa upande wa Yanga, tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 3-1, na Tabora United katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Novemba 7, 2024, kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, haijapoteza tena hadi leo ikiendeleza rekodi nzuri.
Tangu Novemba 7, 2024, Yanga imecheza mechi 17 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza ambapo kati ya hizo imeshinda 16, huku mmoja ikiisha kwa suluhu (0-0), ambayo ilikuwa ni dhidi ya maafande wa JKT Tanzania Feb. 10, 2025.
Mechi hiyo ya JKT Tanzania iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo Mbweni, ilikuwa ya kwanza kwa kocha mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi tangu atambulishwe kukiongoza kikosi hicho, Februari 4, 2025, akichukua nafasi ya Mjerumani Sead Ramovic.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema sababu kubwa ya mwenendo wa timu hiyo kwa sasa ni kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo bila ya kupumzika, japo anatumia kipindi hiki cha mapumziko kurekebisha changamoto mbalimbali.
“Tumejitahidi kufanya mabadiliko ya mara kwa mara, lakini kama ulivyoona, wachezaji wametumia nguvu kutokana na mahitaji kwa wakati husika, naamini kipindi hiki ni kizuri kwetu kwa ajili ya kurejesha miili katika hali ya kawaida,” alisema.