Osama Korosho; Aikimbia Mtwara, anajitafuta Dar

Muktasari:
- Bondia huyo chipukizi katika mchezo huo ukubwa wa jina lake katika mitaa hiyo ulianza kuonekana mwaka 2022 wakati wa pambano la Mtwara Ubabe Ubabe 2 ambalo lilifanyika chini Kampuni ya promosheni Peaktime Media inayoongozwa na Meja Seleman Semunyu.
Mitaa ya Mkanaredi, Soko la Chuno, Coco Beach, Stendi zamani hadi Mikindani mkoani Mtwara imekuwa mitaa muhimu kwa bondia chipukizi wa ngumi za kulipwa nchini Osama Arabi lakini maarufu zaidi kama Osama Korosho kwani ndio imemkuza.
Bondia huyo chipukizi katika mchezo huo ukubwa wa jina lake katika mitaa hiyo ulianza kuonekana mwaka 2022 wakati wa pambano la Mtwara Ubabe Ubabe 2 ambalo lilifanyika chini Kampuni ya promosheni Peaktime Media inayoongozwa na Meja Seleman Semunyu.
Bondia huyo kwa sasa ndiyo amebeba nembo ya mkoani wa Mtwara kutokana na kupewa jina la Osama Korosho kuendelea kulimulika zao kubwa la kibiashara katika kanda ya mikoa ya kusini.
Bondia huyo mpaka sasa amecheza mapambano matano katika ngumi za kulipwa, akishinda mapambano matatu huku akiwa amepigwa katika mapambano mawili.
Katika mahojiano maalum na Mwananchi, Korosho anaweka wazi kuwa ukubwa wa jina lake umetokana na pambano lake alilocheza mwaka dhidi ya bondia mkongwe Emilian Polino licha ya kupoteza kwa kupigwa kwa pointi lakini lilibadili baadhi ya mambo muhimu kwake.

“Binafsi pambano langu dhidi ya Polino mwaka 2022 ndiyo lilinitoa na kuniweka kwenye ramani na watu wengi wakiwemo hadi viongozi wa serikali kunishika mkono kutokana na uwezo ambao niliweza kuuonyesha.
“Unajua wakati naenda kwenye lile pambano nilikuwa sijulikani, wengi walikuwa wanasikia Osama lakini hakuna ambaye alikuwa ananijua zaidi ya wale ambao walikuwa wanahudhuria mapambano ya mtaani,” anasema bondia huyo.
Safari ya kuja Dar es Salaam
“Kwanza nikwambie kwamba haikuwa rahisi kuweza kuja Dar kwa sababu katika huu mchezo kama huna dhamira ya dhati pamoja na kuwa na watu sahihi huwezi kufikia ndoto zako. Lakini nashukuru sana juu watu wangu kwa kuweza kuniongoza hadi kupata mtu sahihi ambaye yeye ndiye ameamua kunichukua kuwa chini yake.

“Unajua nilikuwa nakuja naangalia ngumi na kuondoka Mtwara lakini namshukuru meneja wangu ambaye ndiyo baba yangu kwa hapa Dar es Salaam, Salum Msangi kuweza kubeba jukumu la kunihamisha kutoka Mtwara hadi Dar.
“Sasa hivi naishi Manzese, meneja amenipangia chumba cha kukaa na kunipa vitu muhimu ili niweze kufikia malengo yangu kuwa bondia mkubwa na siyo jambo jepesi mtu kuweza kufanya, ukweli namshukuru sana,” anasema bondia huyo.
Anasema baada ya kuja Dar es Salaam aliunganishwa na bondia Idd Pialali.

“Yeye ndiyo amenifanya niwe karibu na kaka yangu na nahodha wangu, Idd Pialali kwa sababu meneja wetu amekuwa mmoja na tunafundishwa na mwalimu mmoja kitu ambacho kinaniongezea baraka za kuweza kufika mbali,” anasema Osama.

Yapi malengo yake 2025
“Binafsi nalenga kufika mbali lakini bado nahitaji sapoti ya mkoa wangu wa Mtwara kwa sababu naweza sema ndiyo mwakilishi pekee ambaye angalau nimefikia sehemu katika mchezo wa ngumi na bado nataka kufanya makubwa kupitia uongozi wangu unaonisimamia.
“Kitu kikubwa ni kupata nafasi ya kucheza mikanda mikubwa kwa sababu ndiyo ndoto ya bondia yoyote mwenye malengo ya kufika mbali kimataifa kama mabondia wengine wakubwa wanavyokuwa duniani,” anasema Korosho.