NYUMA YA PAZIA: Messi kituo kifuatacho ni pensheni au nyumbani

KUTAKUWA na sherehe ya 'birthday' tarehe 24 mwezi huu. Antonela Ruccuzzo atalishwa keki. Mateo atalishwa keki. Thiago atalishwa keki. Ciro atalishwa keki. Nani mlishaji? Lionel Messi. Tatizo hatujui atailisha familia yake keki ya kusheherekea siku yake ya kuzaliwa akiwa wapi.

Juzi imetangazwa na klabu yake PSG kwamba ataondoka klabuni hapo sasa hivi baada ya mkataba wake kumalizika. Kwahiyo hatujui kama keki hiyo ataikata akiwa Rosario pale Argentina, au Ibiza Hispania akiwa likizo, au wakati anatambulishwa katika klabu yake mpya.

Hili chaguo la mwisho ndio swali la msingi. Messi anaachana na PSG anakwenda wapi? Anataka nini katika maisha ya soka? Ni swali la msingi. Juni 24 mwaka huu atakuwa anatimiza miaka 36. Ameshinda kila kitu alichokuwa anawania katika soka. Miezi michache iliyopita alikuwa analibusu Kombe la Dunia pale Doha. Anataka nini zaidi?

Tatizo kubwa kuna vijana wengi ambao hawafikii ubora wa Messi hata wakati huu ambao anatimiza miaka 36. Hii inaweza kusababisha Messi akaendelea kucheza Ulaya. Katika maisha halisi ukweli ni kwamba Messi amemaliza muda wake wa kucheza Ulaya. Anaweza kufuata nyayo za swahiba wake Cristiano Ronaldo kwenda kucheza nje ya bara la Ulaya. Hata hivyo, hauwezi kujua.

Huu ni muda sahihi wa Messi kwenda kusaka pensheni yake Asia au Marekani. Unapozungumzia Asia basi ni muda sahihi zaidi kwa sababu anaweza kupata mkataba mnono ambao hajawahi kuupata katika maisha yake ya soka. Na itafurahisha katika ukweli kwamba ataupata mkataba huu katika umri wa miaka 36. Ronaldo aliupata mkataba kama huu katika umri wa miaka 37.

Huu utakuwa ni uamuzi wa kibiashara zaidi na hakuna ambaye atamlaumu Messi. Amebakiza nini Ulaya? Kuna vijana ambao waliwahi kukimbia Ulaya wakiwa na miaka 28 tu kwa ajili ya kwenda kucheza Asia. Mmoja wapo ni Mbrazil Oscar ambaye aliondoka kwenda China akiwa bado wa moto Ulaya huku akihalalisha uamuzi wake kwa kudai kwamba alitoka katika maisha ya shida Brazil kwahiyo uamuzi wake ulizingatia zaidi pesa.

Kama Messi akiondoka Ulaya leo katika umri wa miaka 36 hakuna ambaye ataweza kumlaumu. Amefanya kila kitu Ulaya. Kama tunaamini kwamba Ulaya ndio mahala pekee mchezaji anaweza kuhesabiwa kwamba alitamba duniani kwa kucheza kiwango cha juu basi Messi amefanya hivyo.

Kama Messi angeondoka zake Ulaya akiwa na miaka 27 na kwenda Asia tungeweza kumlaumu kwamba amefanya hivyo kwa sababu ya tamaa ya pesa iliyopitiliza. Lakini hatuwezi kufanya hivyo katika umri wa miaka 36 na ndio maana hata Ronaldo hatukumlaumu kwa kwenda Saudi Arabia. Tulikuwa tunamlaumu kwa kugombana na Erik Ten Hag pale Old Trafford.

Inawezekana Messi akaamua kurudi zake Argentina kucheza katika klabu iliyowahi kumlea kabla hajapevuka, Newell Boy's. Sidhani kama utakuwa ni uamuzi sahihi kwake. Nadhani Messi anapaswa kuwa na kituo cha mwisho kabla ya kurudi Argentina.

Ndoto yake ni kumalizia soka katika klabu hii. Hajawahi kucheza katika Ligi Kuu ya Argentina. Hajawahi kucheza katika klabu yoyote kubwa ya Argentina kati ya Boca Juniors au River Plate. Hata hivyo, sidhani kama utakuwa ni uamuzi sahihi kwake kurudi Argentina kwa sasa. Messi ana kituo kimoja kikubwa cha kukusanya pesa kabla ya kurudi zake Argentina.

Anaweza kurudi Argentina baadaye na kucheza msimu mmoja tu kisha akastaafu soka lakini muda huo sio sasa. Kama anaweza kwenda Saudia akacheza kwa misimu miwili yenye mabilioni ya dola kabla ya kurudi Argentina kwanini isiwezekane?

Kuna hili wazo la Messi kurudi Barcelona. Sidhani kama ni wazo sahihi. Mwandishi mahiri wa zamani wa vitabu vya hadithi kutoka Tanzania, Ben Mtobwa aliwahi kutuusia katika moja kati ya vitabu vyake kwamba kuna maisha huwa ni kama ndoto au simulizi. Huwa yanaishia sehemu nzuri. Haupaswi kumuamsha mtu na kumwambia kwamba ilikuwa ni ndoto.

Maisha ya Barcelona na Messi yalikuwa matamu mpaka mwisho. Yaachwe kuwa kama yalivyo. Hakuna ulazima wa kumuona Messi aliyechoka akirudi Barcelona. Hakuna ulazima wa kumuona Messi akiwa amekaa katika benchi la Barcelona huwa vijana wengine wakicheza. Hakuna ulazima wa kumuona Messi akiingia uwanjani katika dakika ya 78 akitokea benchi katika pambano muhimu la Barcelona.

Acha simulizi ya Messi na Barcelona iendelee kuwa ile ile tu ambayo tuliwahi kuiona mwanzo. Hata kitabu hiki cha PSG hakijasisimua sana kuliko kitabu kile cha Barcelona lakini imebidi tuafiki tu kwa sababu hakukuwa na namna. Barcelona walikuwa lazima waachane na Messi kwa sababu hawakuwa na pesa ya kuendelea kuwa naye.

Vipi kuhusu klabu nyingine za Ulaya? Sijawahi kufikiria sana. Kwamba Messi achezee Newcastle? Kwamba Messi achezee Manchester United? Kwamba Messi achezee Chelsea? Kwamba Messi achezee Arsenal? Hapana. Sijawahi kuwaza vizuri. Inawezekana lakini sijawahi kufikiria vizuri.

Zaidi ya yote ni kwamba katika soka kama la Uingereza Messi anaweza kuanza kudhalilika. Umri wa miaka 36 unapoanza kukutana na mabeki wanaobana meno wa Brighton and Hove Albion wanaweza kujikuta ni mashujaa kumbe walimbana Messi wa uzeeni. Sidhani kama utakuwa umri sahihi wa Messi kucheza England.

Baada ya mashabiki wa soka wa England kumsubiri Messi kwa hamu katika umri wa miaka 24 itakuwa ngumu kumuona katika ubora wake akiwa na umri wa miaka 36. Itakuwa uongo. Itakuwa wizi pia. Sawa, kuna baadhi ya mambo ataonyesha kuliko vijana kina Eddie Nketiah lakini haitakuwa katika ubora ule ambao tuliwahi kumfahamu.

Nadhani mwisho wa siku Messi anaweza kwenda Saudia. Ni kituo kizuri kwake kukifanya kama sehemu ya pensheni yake ya mwisho ya soka. Itakuwa pensheni hasa. Atapokea pesa nzuri ambayo hajawahi kupokea maishani lakini pia atajikuta anacheza na koni. Atapiga chenga kadri anavyoweza.