Prime
NYUMA YA PAZIA: Alexander Isak, ni mpapai chini ya mgomba
Muktasari:
- Mshkaji anayeitwa Teame alifanikiwa kutoroka Eritrea, nchi moja maskini Kaskazini Mashariki mwa Afrika na kwenda zake Sweden. Huyu ndiye baba yake Alexander Isak. Ndiye ambaye alituletea Alexander Isak, mchezaji ambaye anasumbua Ligi Kuu England kwa sasa.
KUKIMBIA vita katika nchi yenye vumbi, njaa, umaskini uliotopea na kila kitu unachokifahamu, sio kazi rahisi. Wazazi wawili kutoka Eritrea mwishoni mwa miaka 1980 walifanikiwa. Wazungu wanadai ‘against all odds’.
Mshkaji anayeitwa Teame alifanikiwa kutoroka Eritrea, nchi moja maskini Kaskazini Mashariki mwa Afrika na kwenda zake Sweden. Huyu ndiye baba yake Alexander Isak. Ndiye ambaye alituletea Alexander Isak, mchezaji ambaye anasumbua Ligi Kuu England kwa sasa.
Isak anafunga kadri anavyojisikia. Mzuri hewani, mzuri chini, mzuri akiwa na mpira. Kuna mambo yamenifikirisha kuhusu Isak katika mchezo wa soka. Wazazi wake wametokea wapi? Eritrea. Moja kwa moja yeye ni Mueritrea.
Likizo zake huwa anambeba baba yake pamoja na kaka yake kwenda katika mitaa ya Asmara pale Eritrea kwa ajili ya kushuhudia umaskini mkubwa ambao wazazi wake waliutoroka na kwenda katika dunia ya kwanza, Sweden.
Kaitazame Eritrea ipo katika nafasi ya ngapi ya ubora wa Fifa. Wapo nafasi ya 195 katika ubora. Wapo mwisho mwisho kabisa. Lini umewahi kusikia kwamba Eritrea wanashiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika katika soka. Najua haujawahi kusikia.
Lini umewahi kusikia Eritrea wanashinda walau pambano la kufuzu Kombe la Dunia achilia mbali kushiriki michuano yenyewe? Haujawahi kusikia. Lakini ndio taifa lililotuletea Alexander Isak ambaye anasumbua katika Ligi Kuu England kwa sasa.
Ni muda wa kutafakari tofauti. Ni muda wa kutafakari bahati. Ndio, Alexander ana bahati ya kuzaliwa Ulaya. Kama baba yake, Teame, asingetoroka vita pale Eritrea ina maana kipaji cha Alexander kingezaliwa katika mitaa yenye vumbi ya Asmara na kisha kuishia palepale Asmara.
Bahati nzuri Wazungu wamefanikiwa kumtengeneza Alexander awe kama alivyo leo hii. Amezaliwa katika hospitali nzuri. Akiwa mtoto hakusikia milio ya mabomu. Alianza kucheza katika viwanja vizuri na alipoingia katika ujana alijikuta katika mikono salama ya kutimiza kile ambacho alijaliwa na Mwenyezi Mungu. Kipaji cha soka.
Mambo kutoka kwa Isak. Kwanza anatukumbusha namna ambavyo tumepoteza vipaji vingi kwa bahati mbaya ya kuzaliwa katika mataifa maskini. Ndiyo. Kuna vipaji katika ukanda huu ambavyo kama vingezaliwa Ulaya vingeweza kufika mbali zaidi.
Lakini Isak anatukumbusha namna ambavyo bado kuna uwezekano mkubwa wa kuokota papai ukiwa umesimama chini ya mgomba. Ndiyo. Sio kila taifa ambalo sio la kisoka basi haliwezi kutoa mchezaji mahiri ambaye atatingisha dunia. Sio kweli.
Mifano ni mingi. Katika nchi zote mahiri kisoka Afrika nani aliamini kwamba taifa la Liberia lingetoa mwanasoka bora wa dunia kama George Opong Weah? Mpaka leo Ivory Coast, Misri, Senegal, Nigeria, Morocco na mataifa mengine makubwa kisoka Afrika yameshindwa.
Sio tu mataifa makubwa kisoka Afrika, bali hata mataifa makubwa kisoka duniani yameshindwa kutoa mwanasoka bora wa dunia. Hata hivyo, kwa Weah kuwa mwanasoka bora akitokea Liberia lilikuwa fundisho tosha kwamba mtu yeyote anaweza kufanya jambo lolote katika dunia hii.
Kuna wakati nilikuwa natazama kipaji maridhawa cha Dwight Yorke akiwa na Manchester United. Usingeamini kwamba alikuwa anatoka katika nchi ambayo ilikuwa haijulikani kisoka, Trinidad & Tobago. Lakini hivi ndivyo mpira ulivyo. Ungependa kuona Yorke anatokea Brazil lakini alitokea Trinidad.
Zipo nyakati nilikuwa natazama kipaji maridhawa cha staa wa Arsenal na baadaye Barcelona, Alexander Hleb. Usingeweza kuamini kwamba alikuwa anatokea katika nchi ya Belarus. Moja kati ya nchi ndogo zaidi kisoka barani Ulaya.
Mifano ni mingi. Vipi kuhusu Henrikh Mkhitaryan ambaye alitamba na Borussia Dortmund, Arsenal, Manchester United, Roma na sasa hivi Inter Milan. Usingeweza kuamini kwamba alikuwa anatoka katika nchi inayoitwa Armenia, lakini huko ndipo alikotokea.
Wakati mwingine unaweza hata kuikashfu nchi ya India ukiamini kwamba ni nchi ya watu wasiojua mpira. Hata hivyo imewahi kutupa fundi wa mpira aliyezaliwa Ufaransa, Vikash Dhorasoo ambaye wazazi wake walihamia Ufaransa wakitokea India.
Kama Isak angekuwa anatoka Brazil, England, Ufaransa au Ujerumani isingeniacha mdomo wazi. Kama angekuwa amezaliwa na wazazi wa Kinigeria pale Sweden isingeniacha mdomo wazi. Ingekuwa kama tu Bukayo Saka alivyozaliwa na wazazi wa Kinaijeria pale London. Nigeria ni taifa kubwa kisoka.
Lakini kwa Isak kuzaliwa na wazazi wa Eritrea pale Sweden ni sawa tu na kusikia mwanasoka staa anayetamba duniani ambaye amezaliwa na wazazi wa Kisomali pale Ujerumani. Huwa ni kitu nadra lakini kumbe huwa inatokea.
Na tunaporudi kwa Isak sasa hivi anatuachia swali la mwisho la msingi. Nini kinafuata baada ya moto huu ambao ameuwasha pale Newcastle United? Nadhani Isak ni kipimo cha sisi kujua uwekezaji wa Newcastle United unataka nini?
Wengi wetu tulidhani kwamba Newcastle ingewekeza katika kiasi kilekile cha Manchester City na PSG. Kama kuna klabu itafanikiwa kumng’oa Isak kutoka Newcastle kama ambavyo amekuwa akihusishwa kuondoka, basi tutajua tu kwamba uwekezaji wa Newcastle sio mkubwa sana licha ya kuchukuliwa na Waarabu.
Labda kwa kubanwa na kanuni za fedha za Uefa, lakini tunaamini kwamba Newcastle ilipaswa kukusanya hawa mastaa wakubwa wote wanaotamba Ulaya kwa sababu tajiri wao ana pesa nyingi zaidi kuliko matajiri wengine pale England na Ulaya.
Isak atakuwa kipimo chao. Lakini sio tu Isak isipokuwa mara nyingi tumekuwa tukisikia mastaa wakubwa wa Newcastle wakihusishwa na timu nyingine kama vile Bruno Guimaraes. Wakifanikiwa kuchomoka, basi tutajua kwamba uwekezaji wa Newcastle ni wa wastani tu.