Nyota ghali wanaisubiri Simba

Wednesday April 21 2021
bei pic
By Mustafa Mtupa

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika inazidi kunoga ikiwa imefikia hatua ya robo fainali huku Tanzania inawakilishwa na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba.
Hatua hiyo ya robo fainali inatarajiwa kupigwa kuanzia Mei 14-15 kwa mechi za mkondo wa kwanza na zile za mkondo wa pili zitapigwa kati ya Mei 21-22.
Timu zilizoingia kwenye hatua hii zipo nane, lakini Simba haitakutana na zile ambazo zimeongoza hatua ya makundi ya kufuzu robo fainali au iliyomaliza nafasi ya pili kwenye kundi lake la A.
Kuna timu tatu ambazo Simba itakutana nazo ni; CR Belouizdad na MC Alger wa Algeria na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Kwenye timu hizi kuna wachezaji wenye thamani kubwa sana katika soko la usajili na Simba inatakiwa iwaangalie kwa jicho la tatu itakapokutana nao.
Mwanaspoti inakuletea orodha hiyo ya nyota ghali wa timu pinzani ambao Simba inaweza kukutana nao, kulingana na droo itakavyopangwa Aprili 30 jijini Cairo.


Khama Billiat
Fundi huyu wa kimataifa wa Zimbabwe na Kaizer Chiefs alipata umaarufu mkubwa kutokana na kiwango chake alichoonyesha akiwa na Zimbabwe kwenye michuano ya Afcon mwaka 2019.
Jamaa anacheza nafasi ya winga na ndio mchezaji ghali zaidi ndani ya kikosi hicho na kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market, ana thamani ya Euro 1.5 milioni, ambayo ni sawa na Sh 4.1 bilioni za Kibongo.
Mbali ya thamani hiyo, jamaa pia anakunja mshahara mrefu wa Sh.134 milioni kwa mwezi.
Kwenye michuano ya CAF msimu huu amecheza mechi tano na kufunga bao moja, lakini amekuwa na mchango mkubwa kwenye kusaidia timu na michezo aliyokosa ilitokana na majeraha aliyokuwa nayo lakini muda huu yupo fiti na ikiwa Simba itapangiwa wababe hawa wa Afrika ya Kusini huyu ni miongoni mwa wachezaji wa kuwachunga.


Itumeleng Khune
Kipa mkongwe ambaye kwenye maisha yake ya soka hajawahi kuichezea timu yoyote zaidi ya Kaizer Chiefs na timu ya taifa ya Afrika ya Kusini, yeye anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wachezaji ghali ndani ya timu hiyo akiwa na thamani ya Euro 775,000 ambayo ni sawa na Sh 2.1 bilioni za Kibongo.
Mbali ya thamani yake pia ndio kipa wao tegemeo hususani kwenye michuano hii ya Ligi ya Mabingwa akiwa amecheza mechi sita hadi sasa.
Kinachomsumbua ni umri wake mkubwa, hivyo huwa hachezeshwi mechi zote na mbadala wake huwa ni Daniel Akpeyi. Khune anakunja Sh 77 milioni kwa mwezi.


Advertisement

Samy Frioui
Mmoja kati ya wachezaji tegemeo sana wa MC Alger na ndio mwenye thamani kubwa zaidi kwenye timu hiyo kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market. Jamaa ana thamani ya Sh 1.6 bilioni za kibongo.
Samy amecheza mechi tisa za Ligi ya Mabingwa kwa msimu huu, kuanzia zile za hatua ya awali hadi makundi akifunga mabao matatu na kutoa asisti moja.


Billel Bensaha
Huyu ni kiungo mshambuliaji wa MC Algiers. Thamani yake ni Sh1.5 bilioni za Kitanzania. Anacheza kwenye kikosi hicho kwa mkopo wa msimu mmoja akitokea Esperance ya Tunisia.
Huyu pia amecheza mechi tisa za Ligi ya Mabingwa akifunga bao moja na kutoa asisti tatu.
Hana mchango mkubwa linapokuja suala la kufunga yeye mwenyewe, lakini huwa msaada kwa timu kwenye kupandisha mashambulizi.


Amir Sayoud
Katika mechi za hatua ya makundi huyu ni miongoni mwa wafungaji watano bora akiwa na mabao matatu aliyoifungia CR Belouizdad, kiujumla ukianza kuhesabu kuanzia hatua za awali hadi sasa, jamaa amecheza mechi tisa akifunga mabao saba na kutoa asisti mbili.
Yeye ndio mchezaji ghali kwenye timu yao akiwa na thamani ya Sh 2.1 bilioni. Kama Simba itapangwa na wababe hawa wa Algeria huyu ni miongoni mwa wachezaji wa kuchungwa kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga.


Sofiane Bouchar
Ni ngumu sana kuona beki anakuwa na thamani kubwa kama huyu jamaa. Kwenye kikosi cha CR Belouizdad yeye anashika nafasi ya pili kwa kuwa mchezaji ghali zaidi mwenye thamani ya makadirio ya Sh 1.8 bilioni kwa pesa za Kibongo.
Amecheza mechi zote 10 kuanzia hatua ya awali, ni beki wa kati, anaweza kucheza pia kama kiungo mkabaji au beki wa kulia.


Advertisement