Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Novatus kaanza na moto uefa

ELIYA SOLOMON


NYOTA wa Kitanzania, Novatus Dismas ambaye anaichezea FC Shakhtar Donetsk, amemwagiwa sifa huko Ujerumani na mashabiki wa timu hiyo baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto.

Licha ya  Shakhtar kuanza vibaya michuano hiyo ya Ulaya kwa kupoteza nyumbani kwa mabao 3-1, Novatus alikuwa kivutio kwa mashabiki wa timu hiyo kwa kupata nafasi ya kumwona kwa mara ya kwanza akiwatumikia kwenye mchezo huo mkubwa.

Novatus alicheza kwa dakika zote 90 huku akiwa ndiye beki aliyepata alama kubwa zaidi 3.7 chini ya tano ikiwa ni za ufanisi wa mchezaji uwanjani, sambamba na Yukhym Dmytrovych Konoplya aliyekuwa akicheza beki ya kulia huku Mtanzania huyo akifanya vizuri upande wa kushoto.

Kwa mujibu wa Mtanzania, Anthony Kavunde ambaye alikuwa mmoja mashabiki zaidi ya 50,000 ambao walishuhudia mchezo huo kwenye uwanja wa Volksparkstadion, Hamburg alisema mashabiki wenzake hawakutarajia kumwona akianza. 

“Kundi kubwa la mashabiki ambao nilikuwa nao uwanjani hawakutegemea kabisa kumwona akianza, walikuwa na shauku ya kuona uwezo wake, kiukweli walimfurahia kwa sababu ni mwepesi na uwezo wake wa kuzuia ni mkubwa, nilikuwa nikimshangilia kila ambapo alikuwa akigusa mpira,” alisema Anthony.

Kwa upande wake, Novatus alisema alikuwa tayari kwa nafasi hivyo alipoelezwa kwamba atakuwa sehemu ya kikosi ambacho kitaanza alilipokea hilo vizuri kwani ilikuwa shauku yake kuwa sehemu ya mchezo huo japo matokeo hayakuwa mazuri upande wao.

“Hisia zilikuwa kubwa, nilihitaji kuonyesha vile ambavyo naweza kusaidia timu japo ndio hivyo matokeo hayakuwa mazuri, nilicheza mno kwa kufuata kile ambacho nilipaswa kufanya, naamini kuwa huu ni mwanzo na nitaendelea kupata nafasi zaidi,” alisema.

Mara baada ya mchezo huo, kocha wa Shakhtar, Patrick van Leeuwen aliulizwa kuhusu kuanza kwa Novatus kwanini aliamua kutoa nafasi kwa mchezaji huyo wa Kitanzania mwenye miaka 21.

“Tuna zaidi ya wachezaji kumi na mmoja, ndiyo maana wakati fulani tunafanya chaguzi tofauti,” alijibu kocha huyo.

Je, kulikuwa na sababu yoyote ya ziada kucheza mechi yao hiyo ya nyumbani huko Hamburg? Patrick alisema,”Uwanja ulikuwa umejaa, kwa hivyo ninaamini kuwa kuja hapa ilikuwa ni uamuzi mzuri kwa Shakhtar. Watu wengi hapa wanaonyesha kupendezwa na michezo ya kimataifa. Nimeridhika na eneo na kwamba mashabiki walikuja. Kwa maoni yangu, ndiyo, Hamburg ni chaguo zuri.”

Takwimu zinaonyesha ndani ya dakika 90 za mchezo huo, Novatus alikuwa na usahihi wa asilimia 80 katika utoaji wake wa pasi kwa walengwa, alicheza kwa nidhamu ya hali ya juu katika kushambulia na kuzuia, hakuonyeshwa kadi yoyote.

Katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Ukraine ambao Shakhtar ilikuwa nyumbani kucheza dhidi ya Obolon, Novatus alikuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba huku kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Blago-Youth akipata nafasi ya kucheza kwa mara yake ya kwanza.

Shakhtar sio wanyonge licha ya kuanza kwa kipigo kwenye soka la Ulaya kwani 2009, ilikuwa timu ya pili ya Ukraine kushinda taji la Ulaya (na ya kwanza tangu uhuru), na ya kwanza kushinda Kombe la UEFA baada ya kuwashinda Werder Bremen katika fainali, kwa mabao ya Wabrazili Luiz Adriano na Jadson.

Ushindi huo ulimpa mchezaji Mariusz Lewandowski tuzo ya mwanasoka bora wa Kipoland 2009. Hii pia iliwafanya washindi wa mwisho wa Kombe la UEFA kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Europa League.


NOVATUS AFUATA NYAYO

Novatus amekuwa mchezaji wa nne wa Kitanzania kucheza michuano mikubwa ya soka barani Ulaya nyuma ya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye alifanya hivyo akiwa na KRC Genk kwa kucheza Europa League na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa sasa Samatta ambaye anaichezea PAOK ya Ugiriki yupo kwenye michuano ya Europa Conference League.

Miaka ya nyuma Sunday na Kassim Manara walicheza michuano ya Ulaya.