NOMA: Hawa jamaa walitushika

JICHO LA MWEWE: Aucho anatufundisha kucheza mpira rahis, tumuige

YAPO mengi ya kuyazungumza kwa mwaka huu wa 2021, lakini kwa leo makala hii inakuletea baadhi ya usajili wa makocha na wachezaji waliotikisa Tanzania Bara kwenye michuano mbalimbali.


KHALID AUCHO

Yanga wanajivunia usajili wa Mganda Khalid Aucho kutokana na kile ambacho ameanza kukifanya akiwa na jezi ya njano na kijani ambazo Wananchi wamekuwa wakitamba nazo mitaani.

Jamaa amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu yao ya kiungo ambayo awali ilikuwa ikimtegemea, Mukoko Tonombe.

Usajili wake ulitikisa na kuna kipindi aliwahi kuhusishwa kujiunga na Simba. Haikuwa kazi nyepesi kwa Yanga kupata saini ya Mganda huyo ambaye alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Misri katika timu ya El Makkasa.


PETER BANDA

Mashabiki wa Simba walikuwa wakimtaja Peter Banda kama mrithi sahihi wa Luis Miquissone aliyetimkia zake kwa mabingwa wa Afrika, Al Ahly. Wakati huo Banda alitoka kufanya vizuri akiwa na timu ya taifa la Malawi.

Bado hajaanza kuonyesha makali yake japo keshatupia nyavuni bao moja, lakini ni miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wakizungumzwa zaidi wakati wa usajili kabla ya kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.


DJIGUI DIARRA

Baada ya Yanga kuachana na Farouk Shikhalo na Metacha Mnata, minong’ono ilikuwa mingi kwa mashabiki wa timu hiyo huku wengi wakiwa na hofu juu ya uamuzi huo.

Mabosi wa Yanga kumbe walikuwa na jambo lao. Walikuwa tayari wamemalizana na Djigui Diarra ambaye amekuwa akichezea timu ya taifa la Mali. Ndani ya michezo sita ya ligi ambayo kipa huyo amewatumikia Wananchi ni kama amewasahaulisha mashabiki wa timu hiyo kile kilichotokea.

Diarra alibamba katika usajili wake na kwa muda mfupi mashabiki wa Yanga wanaonekana kuwa na imani naye. Wamekuwa wakipamba kuwa ana uwezo wa kudaka hadi mishale ikiwa ni sehemu ya kunogesha ubora wake uwanjani.


PABLO FRANCO

Mhispania Pablo Franco alishtua maana haijawahi kutokea kocha aliyewahi kuinoa timu iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) kutua nchini. Kila kona alikuwa akizungumziwa. Wapo ambao walikuwa wakiponda usajili huo kwa kusema hawezi kuchukua muda na kibarua chake kitaota nyasi.

Kwa wana Simba wao ilikuwa ni shangwe tu maana waliona pira lao sambusa linarejea tena baada ya kuuanza msimu huu kwa kusuasua.

Katika maisha yake ya ufundishaji soka Pablo aliwahi kuinoa Getafe na pia kapita Real Madrid.


HERITIER MAKAMBO

Ulikuwa urejeo wa kishindo kufuatia kufanya makubwa akiwa na Yanga msimu wa 2018/19 ambapo alifunga mabao 21 kwenye mashindano yote ikiwemo 17 kwenye ligi.

Makambo alishtua tofauti na Fiston Mayele maana alikuwa mchezaji ambaye Wananchi walikuwa na kumbukumbu naye nzuri. Mayele ndiye mara kwa mara alikuwa akiingia vichwani mwao licha ya kwamba mshambuliaji huyo toka DR Congo aliondoka akiwa moto wa kuotea mbali.


AMISS TAMBWE

Hakuna ambaye alikuwa anatarajia kuona jina kubwa kama Amiss Tambwe akicheza Championship. Ilikuwa kama sapraizi kwa wadau wa soka nchini kwani wana kumbukumbu nzuri za mshambuliaji huyo kwa kile ambacho alikifanya nchini kwa nyakati tofauti akiwa na timu za Simba na Yanga.


EDWARD MANYAMA

Usajili wa beki huyu wa kushoto wa Azam ulikuwa na mvutano. Kuna kipindi alikuwa akitajwa kuwa amemalizana na Simba mara ghafla ikatangazwa kuwa amejiunga na Azam. Ni zaidi ya umafia uliofanywa kwenye dili hilo kiasi cha kuwa gumzo.