NIONAVYO: Uwanja wa Mkapa ni kielelezo cha utunzaji wetu

TIMU ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ inasafiri wiki ijayo kuelekea Kaskazini mwa Afrika kule Misri, kwa ajili ya mchezo wao wa kimataifa wa kundi F wa kufuzu kwa fainali za Afrika, Afcon 2023, dhidi ya majirani zao Tanzania.

Baada ya mchezo huo utakaofanyika Machi 24, The Cranes itasafiri hadi Dar es Salaam kucheza na Taifa Stars kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa siku nne baadae.
Habari hi yo hapo juu inaweza kumshangaza msomaji. Ukiangalia kwenye ramani, Uganda iko umbali wa kutembea kwa miguu mpaka kufika Tanzania. Inakuwaje Uganda na ndugu zao Tanzania wanaenda kucheza Misri? Ukweli ni kwamba Uganda  haina uwanja wenye hati ya kuandaa michezo ya hadhi ya juu (Tier 1) ya FIFA na CAF   hivyo imechagua Misri kama nyumbani.

Yawezekana Uganda walifikiria kucheza Dar Es Salaam kama nyumbani lakini bahati mbaya katika mashindano haya Tanzania ni mahasimu wao pamoja na kwamba ndio pekee wenye uwanja wenye sifa miongoni mwa majirani zake.Yawezekana waliogopa kuwapa Tanzania faida ya uenyeji mara mbili.
Hili siyo jambo geni kwa siku za karibuni.Tumeona vilabu na timu za taifa za nchi jirani na nchi za mbali zikiomba kutumia Uwanja wa Mkapa kama uwanja wao wa nyumbani.Hali hii limechochewa na kupandishwa kwa viwango vya viwanja vya mashindano ya shirikisho la soka la dunia na lile la Afrika.Usalama,sehemu ya kuchezea n ahata mwonekano katika televisheni ni mambo yanayopewa umuhimu kwa sasa.

Kadhia wanayopata majirani zetu Uganda inaweza kutupata na sisi kama hatutachukua hatua kwa kuongeza nidhamu katika kutunza miundombinu ya viwanja.Ziara ya hivi karibuni ya maafisa wa CAF iliibua wasiwasi kuhusu hali ya sehemu ya kuchezea (pitch) katika uwanja huo.Ilishauriwa kupunguzwa kwa michezo inayofanyika katika uwanja huo.Kufuatia ushauri huo,michezo ya ligi kuu inayozihusu Yanga na Simba iliondolewa katika Uwanja wa Mkapa na hivyo vilabu husika kulazimika kutafuta viwanja vingine kwa baadhi ya michezo yao ya Ligi kuu na kubaki kutumia uwanja wa Mkapa kwa mashindano ya CAF na pia mchezo wa marejeano kati ya Taifa Stars na Uganda.

Nikiwa kwenye utumishi wa mpira wa miguu,nilibahatika kuwa mjumbe wa kundi maalum (study group) la Fifa la kuangalia miundombinu ya mpira wa miguu na miradi ya kuingiza kipato nikiwakilisha mataifa ya Afrika yanayoongea kiingereza.Katika matatizo makubwa ya Afrika tuliyoyaona hayako tu kwenye uwezo wa kupata miundombinu ya mpira wa miguu lakini yako zaidi katika nidhamu ya utunzaji wa miundombinu hiyo.

Ukitaka kujua tusivyokuwa na nidhamu ya utunzaji angalia maeneo yaliyotengwa mtaani kwa ajili ya kuchezea au kupumzikia,yamechukuliwa na kubadilishwa kuwa makazi na kama yamebaki basi yamekuwa njia za wapiti kwa miguu,bodaboda na hata wanyama na magari.Maeneo mengine sasa yamegeuzwa kuwa sehemu ya kukusanyia bidhaa chakavu za plastiki na vyuma.Hakuna anayeuliza na hakuna anayependa kuulizwa.Kiongozi wa mtaa anaonekana muungwana kwa kuruhusu watu kujenga au kutumia miundombinu hii wanavyotaka kuliko ilivyokusudiwa.

Uwanja wa taifa (Benjamin Mkapa) ni uwanja mpya na unatakiwa kuonekana hivyo.Mchezo wa kwanza katika uwanja huo ulifanyika Septemba 2007 kwa mechi ya kirafiki kati ya Tanzania na Uganda.Mwaka 2017 uwanja huo ulifungwa kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho kwenye eneo la kuchezea.Hii ilikuwa ni juhudi  ya Sport Pesa na uwanja ulipofunguliwa ulikuwa mpya kwani nyasi zilionekana kijani kabisa na haukuwa tofauti na viwanja tunavyoviona kwenye mataifa yaliyoendelea.Kwa kumbukumbu,naodha wa zamani wa England,Manchester United na Everton alifunga goli katika uwanja huo kwenye mchezo wa Sport Pesa kati ya Everton  na Gormahia. Timu ya Taifa ya Brazil ilicheza mchezo wa kirafiki na Taifa Stars kwenye uwanja huo mwaka 2010.

Tangu uwanja uanze kutumika,nakumbuka katika mechi ya kwanza kulikuwa na malalamiko ya uharibifu na wizi wa vifaa vya maji na umeme.Upungufu wa nidhamu katika utunzaji wa viwanja unaweza kuwa upande wa watumiaji lakini wajibu ni wa menejimenti.Watendaji wa uwanja wanatakiwa kujua kuwa matunzo ya uwanja,hasa sehemu ya kuchezea,si ya lelemama.Nyasi zinahitaji chakula,zinahitaji maji ya kunywa na kuoga,zinahitaji kupumzika na zinahitaji kukatwa au kupunguzwa kwa utaratibu wa kitaalam.Hiki ni kiumbe hai.

Tukiangalie Wembley ulioko Uingereza na ulianzishwa mwaka 1923.Uwanja huo unameza watazamaji 90,000 waliokaa ukimilikiwa na chama cha mpira (FA) na kuendeshwa na Kampuni ya Wembley National Stadium Ltd.Tangu mwaka 2022 iliamuliwa kwamba kwa mwaka uwanja utakuwa mwenyeji wa matukio 46 tu.Kati ya matukio hayo 24 ni yale yasiyo ya kimichezo na 22 ni ya kimichezo basi.Wanawezaje kuenenda na mpango huo? Jibu,nidhamu.

Tukirudi hapa nyumbani,matumizi ya uwanja wa mkapa na viwanja vingine vya michezo yamekosa nidhamu na weledi.Yeyote,wakati wowote anaweza kuutumia uwanja kadri anavyotaka.Mara ngapi ratiba ya michezo ya ligi imekuwa ikibadilishwa ili kupisha tamasha,ibada nk.? Tuko tayari kuitoa kafara kesho endelevu kwa ajili ya pesa za tamasha au kufurahisha watu au kikundi Fulani katika jamii.

Wakati serikali imeeleza adhima yake ya kuongeza miundombinu ya michezo,ni jukumu la wamiliki,iwe ni serikali,halmashauri,Chama cha Mapinduzi na taasisi nyingine binafsi kuimarisha nidhamu katika kutunza miundombinu ambayo tunayo tayari.Bila kujenga nidhamu ya utunzaji,ujenzi wa viwanja vipya itakuwa ni kumwaga maji kwenye pakacha.
Tutajenga viwanja vingi lakini tusipojenga nidhamu yatatupata ya Uganda na juhudi za Hayati Mkapa aliyepambana kuhakikisha tunajenga uwanja wenye hadhi ya michezo ya daraja la kwanza la FIFA zitakuwa zimepotea bure.Waswahili wanasema “kitunze kidumu”

Mwandishi wa makala hii ni Afisa Mtendaji mkuu wa Shirika la kijamii la Life Coaching Organisation (Lico) na Katibu mkuu mstaafu wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF)