Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Utamaduni wa Kombe la Shirikisho ulindwe

HIVI majuzi tulishuhudia mubashara upangwaji wa ratiba ya mwisho ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) 2022/23. Ni ratiba ambayo kwa kiasi kikubwa ilisifiwa na wawakilishi wa klabu waliokuwepo walipopata nafasi ya kutoa maoni yao. Hata hivyo, miongoni mwa watazamaji na mashabiki kuna maswali yaliibuka. Maswali haya yalitokana na mabadiliko katika upangaji na uendeshaji wa mashindano haya hasa katika ngwe ya mwisho ambayo imebaki na klabu nane za Ligi Kuu.

Mmiliki wa bidhaa ana haki ya kuibadilisha na kuiboresha kadri anavyotaka, hilo halina shaka. Hata hivyo, hilo halizuii walaji na hata wasio walaji kushtuka na kuuliza kulikoni kuhusu mabadiliko hayo. Vivyo hivyo, mabadiliko kama ya kupanga timu kwa kuangalia nafasi zao katika ligi (seeding) na viwanja vitakavyotumika viliwashtua wafuatiliaji wa mpira wa miguu.

Mashabiki wanauliza iwapo lengo la ratiba hii ilikuwa kupata bingwa wa mabingwa (Super Cup)? Wanasema kuepusha timu nne za juu kwenye ligi kukutana katika ngwe ya robo fainali ni kama upendeleo au mpango fulani wa kuhakikisha timu za juu hazitolewi katika hatua hii. Ni kama jaribio la kunakili picha ya msimamo wa Ligi Kuu na kuibandika katika msimamo wa Kombe la Shirikisho.

Wadau wanauliza ni kwa nini timu nne za juu zilizopewa nafasi ya kukwepana wao kwa wao kukutana pia zinapewa upendeleo wa kutumia viwanja vyao vya nyumbani?

Wadau wanaona kuwa timu zilizo nje ya timu nne za juu kwenye msimamo wa ligi ambao kimsingi ni picha ya ulinganifu wa msuli wa kifedha zinapewa mzigo zaidi wa gharama za kuzifuata timu nne za juu zenye uwezo kiuchumi.
Wadau wanauliza, vipi ile falsafa ya kupeleka mpira ‘nchini’ kwa kutumia mashindano haya imekufa?

Kama nilivyosema awali, wamiliki wa shindano ambao ni shirikisho wana haki ya kufanya mabadiliko kadri wanavyoona ni sawa, lakini wajue heshima au hadhi ya bidhaa au chapa hutoka kwa walaji kutegemea watakavyochukulia au kueleweshwa kuhusu kiini cha mabadiliko. Mwendelezo na kutabirika (consistency and predictability) ni jambo la muhimu sana katika kulinda bidhaa. Mpaka msimu uliopita, mashindano haya yalikuwa yanakwenda vizuri na kuonekana ni mashindano ya watu. Jiulize kwa mfumo wa leo Coastal Union wangepata nafasi ya kucheza ile fainali ya dhahabu dhidi ya Young Africans?

Kuhusu uwanja utakaotumika kwa fainali nako kuna maswali mengi. Wadau wanauliza kwa nini Tanga wakati falsafa ya mashindano haya ni kupeleka mpira nchini kwa kucheza fainali kwenye mikoa isiyo na timu za Ligi Kuu? Lengo hapa ilikuwa ni kuipa nafasi mikoa hiyo kuzinduka na hata kuboresha miundombinu ya kuchezea mpira. Alipoulizwa kuhusu hili, mwakilishi wa TFF alisema kuwa wameanza mfumo mpya wa mikoa kuomba kuwa wenyeji (hosts) wa mashindano na kwamba Tanga (CCM Mkwakwani) ilishinda miongoni mwa mikoa iliyoomba. Vema, kama shirikisho limefanya mabadiliko kuhusu wenyeji ni bora yakawa wazi na vigezo vikawekwa wazi ili anayekosa ajue amekosa katika mazingira ya usawa na uwazi na anayepata asinyooshewe vidole. Njia mbadala ni kuweka uwanja maalum (mfano Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa) kwamba ndio utakuwa uwanja wa fainali kwa Kombe la Shirikisho.

Nionavyo mimi, ni vizuri mashindano ya Kombe la Shirikisho yakajikita katika falsafa na makusudi yake bila kuathirika sana na matokeo kwenye mashindano mengine. Shindano hili ambalo liliwahi kukwama na kufufuliwa miaka isiyozidi kumi huko nyuma lilichangamsha sana mpira na kutoa nafasi za uwakilishi hata kwa timu zisizokuwa juu kwenye Ligi Kuu.

Walio wa zamani tunakumbuka namna Kombe la Taifa (Taifa Cup) lilivyokuwa likipeleka furaha mikoani. Zikumbuke timu kama Mzizima United (Dar es Salaam), Mazengo Warriors (Dodoma), Igembe Nsabo (Shinyanga), Lweru Eagles (Ziwa Magharibi/Kagera), Tanga Stars (Tanga), Mount Meru Warriors (Arusha) na mingine mingi. Ilikuwa ni nafasi ya mpira kuchezwa kwenye mikoa yote hata isiyokuwa na timu za Ligi Kuu. Mashindano haya yaliibua pia vipaji ambavyo vilikuwa havijaonekana kwenye Ligi Kuu.

Mathalani, nchini Uingereza na Kombe lao la FA. Sisi tulio mbali tunashabikia sana timu za Uingereza na Ligi Kuu (EPL) hata kuliko wenyeji. Kwa wenyeji wanapenda sana mashindano ya Kombe la Chama cha Soka (FA Cup) kwa sababu ni nafasi muhimu sana ambapo timu za daraja la juu zinaweza kusafiri kwenda kucheza na timu kutoka miji midogo. Mfano Manchester United inasafiri kwenda kucheza na Yeovil Town mbele ya mashabiki wenyeji wasiofika 10,000. Mashindano haya hupeleka hamasa na maendeleo ya mpira nchini hasa kwa maeneo yasiyokuwa na timu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.

Ni wakati sasa wa wahusika kujadili mwelekeo wa Kombe la Shirikisho ikiwa ni pamoja na uendeshaji ili kuhakikisha chapa yake inakuwa tofauti (unique) na hivyo kuchangia katika kutoa burudani, maendeleo ya mpira wa miguu na pia kumpa thamani ya fedha yake mdhamini wa shindano. Ni muhimu Ligi Kuu ikaachwa kuwa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho likabaki Kombe la Shirikisho.

Mwandishi wa makala hii ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kijamii la Life Coaching Organisation (Lico) na Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).