NIONAVYO: Matukio uwanja wa taifa yawe funzo

Tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2007 uwanja wa taifa wa Benjamin Mkapa umekuwa na matukio mengi. Matukio mengi ni ya kawaida ya kimichezo lakini yamekuwepo pia matukio kadhaa, japo machache ,lakini yanayoweza kuathiri taswira ya kimichezo na kiusalama kwa uwanja wenyewe na taifa kwa ujumla.

Jambo la kusikitisha lilitokea juma lililopita wakati wa mchezo wa kimataifa wa fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho  Afrika kati ya timu ya Yanga ya Tanzania na USM Alger ya Algeria. Tukio lenyewe,kwa mujibu wa vyombo vya habari, lilitokana na kuchelewa kufunguliwa kwa milango ya kuingia uwanjani hivyo mashabiki kujaribu kuruka ukuta na kisha kutokea mkanyagano baada ya polisi kuingilia kati.   Tukio hilo liligharimu uhai wa shabiki mmoja na kuacha zaidi ya mashabiki 30 wakiwa wamejeruhiwa.

Tukio la juma lililopita linatokea siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupokea nyaraka za maombi ya pamoja ya Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa mashindano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) ya mwaka2027.Matukio kama haya yanaweza kuwa moja ya vigezo vya kuangaliwa wakati wa kuchambua maombi ya kuandaa mashindano ya CAF na hata Fifa.

Shirikisho la mpira duniani (FIFA) limeweka viwango vya kuhakikisha usalama wa wachezaji, wafanyakazi wa uwanja, mashabiki na umma kwa ujumla. Kuvunjika kwa usalama kunaweza kusababishwa na namna utaratibu wa usalama wa tukio ulivyo au namna majengo ya sehemu ya tukio (uwanjani) yalivyotengenezwa. Kwa hiyo suala la usalama wa viwanja linahusisha watu na huduma za uwanjani lakini pia huduma za umma kama polisi na zimamoto. Uratibu wa siku ya tukio usipokwenda sawa unaweza kusababisha kero katika kufanyika kwa mchezo lakini pia maisha ya watu kuwa hatarini.Watumishi wa uwanja wanahitajika kujua viashiria hatarishi vilivyopo uwanjani siku ya mchezo.

Waswahili wanasema kosa si kosa ila kosa ni kurudia kosa. Matukio yanayotokea yanatakiwa kuorodheshwa na kutolewa maelezo ya ni jinsi gani yangeweza kuepukika. Mfano kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuna tukio lilitokea wakati wa mchezo kati ya Taifa Stars na Brazil kwa shabiki kijana mwanafunzi wa shule ya Green Acres Nageri Kombo (21) kuvamia uwanja na kumkumbatia mchezaji wa Brazil aliyejulikana kama Ricardo Dos Santos maarufu kama Kaka. Pamoja na tukio hilo kutoleta madhara ya mwili, lakini lilionyesha udhaifu uliokuwepo katika kulinda usalama. Kijana alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi lakini mpaka leo hatujaambiwa ni nini kimefanyika kutokana na funzo hilo.

Mwaka 2016, wakati wa mchezo kati ya timu za Simba na Yanga mashabiki wa Simba waling’oa viti na kuvirusha uwanjani wakipinga maamuzi ya mwamuzi. Kilichofanyika kwa upande wa TFF ilikuwa ni kuipiga faini ya shilingi milioni 5 kwa utovu wa nidhamu wa mashabiki wake. Kwa mamlaka ya uwanja hatujui kama kuna funzo limepatikana katika tukio hilo na kama hatua zilichukuliwa kuhakikisha tukio kama hili halijirudii.

Tukio jingine ni la kuzimika taa wakati mchezo unaendelea kati ya timu ya Yanga na Marumo Gallants ya Afrika Kusini. Kibaya zaidi tukio hili lilitokea baada ya tukio jingine kama hili wakati Tanzania ikicheza na Uganda. Serikali imechukua hatua ikiwemo kuwasimamisha baadhi ya watumishi wake lakini hakuna anayejua kama funzo limechukuliwa na kufanyiwa kazi ili kuhakikisha halijirudii.

Matukio ya    Uwanja wa Benjamin Mkapa yanawakilisha matukio mengine katika viwanja vingine nchini vyenye matukio kama hayo na hata tofauti ya hayo. Historia ya matukio husaidia watu makini kutengeneza taratibu na hata kanuni kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii.Ukiondoa tatizo la taa ambalo kwa kiasi kikubwa ni la miundombinu,changamoto zilizo nyingi katika viwanja vyetu zinatokana na uzembe au kutokuwa na ufahamu wa kutosha kwa watendaji wa siku ya tukio.

Viwanja vya mpira ni sehemu nzuri kwa familia kwenda kupata furaha, kwa michezo kufanyika kama ilivopangwa na kwa wamiliki na wadau wengine kuingiza kipato. Uwanja wa mpira haufai kuwa sehemu ya matukio ya kuumiza mwili na hata vifo kwa mashabiki  kama ilivyotokea kwa shabiki ambaye familia ilitegemea atarudi salama usiku na kuwasimulia aliyoyaona uwanjani lakini badala yake wanaitwa kuchukua mwili hospitali.

Viwanja na miundombinu yake vimewagharimu walipa kodi au wamiliki binafsi kiasi kikubwa cha fedha hivyo matumizi mabaya yanaweza kuwa na athari hasi ambazo hazitawaathiri wamiliki peke yao bali wadau wote na nchi kwa ujumla.

Hatujachelewa,tujifunze kutokana na matukio yaliyotupata na hata yaliyowapata  wengine ili kuhakikisha viwanja vyetu vinafaa na viko salama kuandaa matukio ya kiwango chochote.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.