NINAVYOJUA : Tunakosea kuwauliza wasemaji masuala ya ufundi
Muktasari:
Wasemaji wa klabu wanajulikana mno na mashabiki wa soka wa Tanzania hasa wale wanaofuatilia ligi zetu kiasi cha kuweza hata kupangwa katika orodha ya 10 bora miongoni mwao na hii inatokana na namna ya uzungumzaji wao wenye utani mwingi.
INAWEZEKANA ikawa Tanzania pekee ndiko ambako wasemaji wa klabu wanajulikana zaidi kuliko makocha wa timu husika.
Wasemaji wa klabu wanajulikana mno na mashabiki wa soka wa Tanzania hasa wale wanaofuatilia ligi zetu kiasi cha kuweza hata kupangwa katika orodha ya 10 bora miongoni mwao na hii inatokana na namna ya uzungumzaji wao wenye utani mwingi.
Imekuwa hivyo hadi watu wote tumeukubali mfumo huo ambao TFF waliuasisi na sasa umekuwa na nguvu na vurugu kwenye klabu nyingi. Sijui walitoa wapi utaratibu huu wa kuwafanya watu wa habari wa klabu kuwa wazungumzaji kwa kila kitu. Hii ni tofauti na nchi za wenzetu ambako huwezi kumsikia msemaji wa klabu hata mtendaji wa klabu wakizungumzia masuala ya mchezo utakaochezwa au uliochezwa.
Ni kawaida kumsikia Deo Kaji Makomba msemaji wa Stand United, mara utamsikia Thobias Kifaru wa Mtibwa, Masau Bwire kadhalika Jerry Muro na Haji Manara.
Wasemaji hao wamekuwa wakizungumzia mambo yanayohusu klabu zao na mengine yasiyoingia kwenye dhana nzima ya usemaji wa klabu. Kwenye nchi za wenzetu tena klabu kubwa duniani huwezi kuukuta mfumo huo! Sijui nani anayemjua msemaji wa Manchester United, Arsenal, Chelsea, Real Madrid na nyinginezo nadhani hakuna, ila ni rahisi kuwajua watendaji wakuu wao na wengi tunawafahamu. Lakini hapa Tanzania ni rahisi kumjua msemaji wa Ruvu Shooting kuliko kumjua kocha wake au katibu. Pia, ni rahisi kumjua msemaji wa Coastal Union kuliko kumfahamu kocha na wengi pengine wanamjua zaidi Oscar Assenga kuliko Ally Jangalu.
Kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi ya jinsi ya kuwauliza wasemaji hao kuhusu masuala ya kiufundi na wachezaji kwa jumla. Mara zote maisha ya wachezaji ndani na nje ya uwanja yamekuwa yakifuatiliwa kwa ukaribu sana na waalimu au ‘coaches/managers’ wa timu.
Ni rahisi kwa kocha kuzungumzia masuala yanayomhusu mchezaji kwa sababu tayari anamjua kwa mchezaji wake tofauti na taarifa itakavyofikishwa kwa mtu aliye mbali na wachezaji.
Ni rahisi mchezaji kumzungumza na kocha na kumueleza masuala ya ndani kabisa ya maisha yake kuliko msemaji wa klabu. Ni kawaida kwa mwalimu kuongelea afya ya mchezaji mfano aliyetoka kuumia ghafla uwanjani na daktari wa timu kumpa taarifa ambazo mwalimu ndiye anayeweza kuzitoa. Hii ni tofauti na baada ya mchezaji huyo kuwa amekaa nje ya uwanja kwa matibabu ya muda klabu inaweza kutoa taarifa kuelezea nini kinachoendelea kuhusiana na mchezaji huyo hii sasa ndiyo kazi ya wasemaji ambao kitaaluma ni wanahabari tu.
Lakini kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi pale watangazaji wa Radio, TV na hata wanahabari wa magazeti kuwahoji wasemaji wa klabu masuala ambao yanatakiwa kuzungumziwa na makocha kabla na baada ya michezo kufanyika. Mfano Jerry Muro alipoulizwa baada ya timu yake ya Yanga kuifunga JKT Mlale mabao 2-1 kwenye Kombe la FA na sasa Yanga ikawa inajianda na mchezo wake dhidi ya Cercle de Joachim kuwa ‘mbona Yanga mmeonekana kusumbuka sana kuwafunga vijana hao’. Alichojibu Muro ni kwamba :“Hii ndio Yanga ya kimataifa inamaliza huku na sasa ndege ina’take off’ kuelekea kwenye mchezo wa kimataifa sisi wa kimataifa bwana.”
Kwa ufupi aina ya maswali haya yaliyohusu kuisemea Yanga iliyocheza mchezo wake wa FA na kuelekea kucheza Ligi ya Mabingwa yalitakiwa yajibiwe na kocha wa Yanga ama msaidizi wake.
Haji Manara aliulizwa baada ya mchezo wao na Yanga, jinsi alivyouona mchezo, bila shaka alikuwa hajatulia huku akiwaza jinsi walivyopoteza mchezo huo, kwake ilikuwa rahisi kumtuhumu mwamuzi moja kwa moja badala ya kuelezea yaliyotokea uwanjani.
Ndio maana kulikuwa na tofauti ya majibu ya Kocha wake Jackson Mayanja na yale ya Manara. Kocha Mayanja alijibu kwa ufupi; “Wachezaji wangu walikosa utulivu wakafanya makosa langoni ndiyo yaliyotufanya tupoteze mchezo ingawa kadi nyekundu aliyopata mchezaji wangu ilichangia sana kupoteza.”