NINAVYOJUA : Pluijm, Yanga iliyobadilika inaweza kuifunga Al Ahly
Muktasari:
Kwa nini tusiwafunge wakati huwa tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini hatuzitumii? Sasa ni wakati wa Yanga na Azam kufunga mikanda kuhakikisha zinashinda michezo yao ya kwanza hapa Dar es Salaam.
BILA shaka Watanzania wapenda soka na siyo mashabiki wenye unazi wa U-Simba na U-Yanga keshokutwa Jumamosi watakuwa wakiomba dua angalau Yanga ishinde mchezo wake wa kwanza dhidi ya Al Ahly.
Kwa nini tusiwafunge wakati huwa tunatengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini hatuzitumii? Sasa ni wakati wa Yanga na Azam kufunga mikanda kuhakikisha zinashinda michezo yao ya kwanza hapa Dar es Salaam.
Lakini Azam ndio itakuwa mara yake ya kwanza kucheza dhidi ya Esperance ya Tunisia.
Yanga huu utakuwa kama mchezo wa marudio tu, ndani ya misimu mitatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika wawakilishi hao wanakutana tena! Al Ahly ilicheza na Yanga Machi, 2014 jijini Dar es Salaam na kurudiana mjini Alexandria kwenye Uwanja wa Jeshi wa Harras El-Hadoud uliokuwa tupu bila watazamaji.
Yanga ile ilicheza soka kali sana kuanzia hapa Dar es Salaam hadi Alexandria na kuwashtua Wamisri hao.
Ilikuwa ni Yanga iliyokuwa inashambulia kwa pamoja na kuzuia kwa pamoja ikionekana kucheza kitimu zaidi, ingawa Yanga ile ya 2014 na hii ya leo utaona kwa nafasi za wachezaji mmoja mmoja, Yanga hii ina wachezaji wenye uwezo mkubwa kuliko waliokuwapo mwaka juzi kwa ulinganifu ufuatao.
Wakati langoni hakuna tofauti sana kwani alikuwapo Deogratius Munishi ‘Dida’ na inawezekana Jumamosi akacheza Ally Mustafa ‘Bartez’, kulia kwale kumeimarika zaidi ni wazi ataanza Juma Abdul mchezaji anayeweza kuzuia kwa ufasaha, kutoa pasi fupi na ndefu za uhakika.
Zaidi ya yote uwezo wake wa kupandisha mashambulizi na kupiga krosi pasi zinazozalisha mabao kila mara ni tofauti na alivyocheza Mbuyu Twite katika michezo ile ya mwaka juzi.
Twite si beki anayeweza kupandisha mashambulizi pia hakuwa mzuri katika kupiga pasi sahihi na nyingi zilikuwa pasi za nyuma.
Kule kushoto alikocheza Oscar Joshua nako hakukuwa kuzuri sana kwani kulikuwa hakuna mtiririko mzuri wa mashambulizi kupitia kushoto, lakini hali hii huenda ikawa tofauti kwani Haji Mwinyi, ndiye atakayeanza na ana uwezo mkubwa wa kutengeneza mashambulizi na kupandisha timu ingawa katika siku za hivi karibuni amekuwa akifanya makosa mengi kila mara, japo anaweza kurekebishika.
Mabeki wa kati , Mtogo Vincent Bossou na Kelvin Yondani wamekuwa na makosa kadhaa ambayo yamekuwa yakiigharimu Yanga. Mabao mengi yamekuwa yakifungwa kupitia katikati ya mabeki hao. Hii ikiwa tofauti na alipokuwa akicheza Nadir Harroub na Yondani!
Tofauti ya Bossou na Nadir ni moja, Mtogo huyo siyo mnyumbufu hasa anapokutana na mshambuliaji anayeweza kumfuata miguuni mwake, hivyo kumfanya Yondani kuwa na kazi nyingine ya ziada ya kumfutia makosa.
Kuna mabadiliko chanya na hasi katika eneo la katikati ambapo katika nafasi ya kiungo mkabaji alikokuwa akicheza, Frank Domayo kumepwaya na hakuna mchezaji aliyekuja kuziba nafsi hiyo kwa ufasaha hadi leo.
Lakini Yanga inafaidika na uwepo wa Thabani Kamusoko, kiungo wa juu ambaye ameleta uwiano mzuri ndani ya kikosi ukilinganisha na jinsi alivyokuwa akicheza Haruna Niyonzima, hali hii inaifanya Yanga iwe na makali zaidi kuanzia eneo hilo.
Kule kushoto alikokuwa akicheza Mrisho Ngassa kwa kweli kupo wazi mno na hakuna mashambulizi ya uhakika kutokea kule anakocheza Deus Kaseke kwa sasa.
Tutaendelea kumkosoa tu hata kama kuna watu wanakasirika! Upande anakocheza Kaseke kumekuwa na matatizo makubwa na ni mara chache kuona mabao yakitengenezwa kutokea kushoto kwa Yanga.
Huyu ni mchezaji mwenye bahati ya kucheza lakini asiye na madhara kwa timu pinzani.
Nafasi za ushambuliaji zimepata watu hasa ukilinganisha Emmanuel Okwi, Hamsi Kiiza na Didier Kavumbagu waliobadilishana na Donald Ngoma na Amissi Tambwe. Hii ni Yanga mpya kiasi inayohitaji kucheza kwa ushirikano mno ili kuifunga Al Ahly Jumamosi.
Kwa timu hii huwezi kutarajia hata mara moja kufungwa na Al Ahly hapa nyumbani na hata kwenda kufungwa ugenini. Tuna imani safu ya ushambuliaji yenye uchu itawasumbua Waarabu.