NINAVYOJUA : Mwinyi ni wakati wa kuiacha miguu yako iongee
Muktasari:
- Mwinyi amekuwa amezoeleka kuonekana kila timu hiyo ya Stars ichezapo dhidi ya mataifa mengine iwe ni kwenye michezo ya kirafiki.
JUZI tu nilimuona kwa mara ya kwanza beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein akipata namba na kucheza katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa mara ya kwanza na kumweka benchi Haji Mwinyi wa Yanga aliyezoeleka kikosini.
Mwinyi amekuwa amezoeleka kuonekana kila timu hiyo ya Stars ichezapo dhidi ya mataifa mengine iwe ni kwenye michezo ya kirafiki.
Ni baada ya kazi ya ziada na kiwango kizuri anachoendelea kukionesha Hussein ndani ya Simba sasa kimemhakikishia namba Stars kwa sasa, ingawa katika mchezo huo dhidi ya Harambee Stars beki huyo hakucheza kwa ufasaha sana. Lakini ni wazi kwa alichokionyesha Moi Kasarani, kinaweza kumfanya Kocha Boniface Mkwasa kumfikiria yeye kuanza kwenye kikosi cha kwanza kuliko Mwinyi.
Hii inatokana na ukweli kuwa kwa sasa kiwango cha Mwinyi kinatia shaka mno na imejidhihirisha hivyo kwani hata kwenye kikosi cha Yanga anayefikiriwa kuanza kila mara kwenye nafasi hiyo ya beki ya kushoto ni Oscar Joshua aliyekuwa akicheza kwa uzuri kiasi ukimlinganisha na Mwinyi,
Ndio maana tumekuwa tukimuona kocha Hans Pluijm akimpanga kila mara Oscar kuanza kwenye michezo yote mikubwa ya Ligi Kuu na ile ya kimataifa toka nusu ya mwisho ya msimu huu ilipoanza.
Kitu ambacho hakikuwa rahisi toka mwanzoni mwa msimu ulipoanza kiasi cha wadau wa soka kuanza kudhani kuwa safari ya Oscar kuondoka Yanga ilikuwa imewadia.
Niliwahi kuandika kuhusu bahati iliyoipata nchi yetu pale tunapoanza kuzungumzia nafasi za mabeki wa kushoto kupatikana wakiwa wenye uwezo mkubwa wa kuicheza kwa ufasaha nafasi hiyo nikiwazungumzia Mwinyi na Hussein.
Kipindi hicho Mwinyi alikuwa kwenye kiwango cha uchezaji cha hali ya juu! Kijana huyo alibahatika kupata namba haraka mwanzo tu mwa msimu wake akitokea KMKM Zanzibar na kuingia katika vikosi vya kwanza vya Yanga na Taifa Stars.
Kwa hakika alikuwa akicheza vizuri kwenye michezo mikubwa ya timu yake ya Yanga dhidi ya Azam, Simba, Mtibwa na nyingine, pia aking’ara Stars katika michezo dhidi ya Malawi, Nigeria na Algeria akifanikiwa kwa kiasi kikubwa kunyang’anya mipira kwa staili yake ya kulaza ‘tackling’. Pia alikuwa anapandisha mashambulizi huku akijiamini sana, kupiga krosi pasi zilizozalisha mabao kumbuka bao lililofungwa na Thomas Ulimwengu dhidi ya Malawi, Bao alilokosa Mrisho Ngasa dhidi ya Nigeria na bao lililofungwa na Elias Maguli dhidi ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa zote hizo zilikuwa krosi pasi zilizotoka kwenye miguu ya Mwinyi.
Kipindi hiki ni miguu yake tu ndio ilikuwa inaongea. Mwinyi huyo wa miezi minne mitano ya mwanzo mwa msimu wa 2015/2016 si Mwinyi wa leo! Huyu amepoteza uwezo mkubwa wa kujiamini, hawezi tena kupandisha mashambulizi mfululizo bila kuchoka na kupiga krosi kila akipanda. Kwa sasa beki huyo hawezi kukokota mpira hatua ndefu bila kunyang’anywa! Mwinyi anapoteza pasi kila mara na hana nguvu nzuri za kupiga kama ilivyokuwa awali, siku hizi anaweza kurusha mpira halafu mpira usirushwe mbali badala yake unadondoka mikononi. Huyu mdogo wetu sijui kapatwa na nini? Lakini Mwinyi hataki kukubali hali hii, kisha ajiulize kunani kwake yeye ameanza kurusha lawama kwamba hapendwi na wapenzi kadhaa na ambao wameanza kumzushia maneno ya kuwa anamatumizi mabaya ya vitu visivyokubalika michezoni na hivyo ndivyo vinavyompotezea nguvu!
Mwinyi ameanza kulalamika akisikika kuwa hana raha pale klabuni na tayari anataka kuanza kukata tamaa, huyu si mpiganaji wa kweli. Kwa sasa Mwinyi anatakiwa kugeuka nyuma pia upande wake wa kushoto awaangalie kaka zake waliopita hapo Yanga na Stars kama kin Riffat Said, Abdi Kassim ‘Babi’ na yupo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ waliocheza hapo kwa mafanikio makubwa huku wakivilinda viwango vyao kwa muda mrefu bila kuchuja.
Amuulize Cannavaro ni maswahibu na changamoto ngapi wamepitia lakini wakifanikiwa kucheza kwenye ubora kwa muda mrefu huku wakivilinda viwango vyao?
Hawa hawakuwahi kutetereka na wala kubabaika na na maisha ya jiji la Dar es Salaam, yaliyoweza kujaribu kuua viwango vyao siku zote waliiacha miguu yao iongee na kila mdau alikuwa akikubali uwezo wao.
Kucheza na kupata namba kwenye vikosi vya timu kubwa kama Yanga, Azam na Simba kunahitaji uwezo mkubwa wa kujituma, huku ukicheza wa kiwango bora siku zote.
Kuwa mchezaji wa timu ya Taifa na kufanikiwa kuaminiwa mbele ya Watanzania wengi tena kwenye michezo mikubwa kunamhitaji mchezaji kujilinda katika hali zote zinazoweza kumtoa kwenye uchezaji bora alionao.
Wachezaji wengi hupata maumivu na majeraha yanayoweza kuwaweka nje ya uwanja kwa muda, lakini pale wanapofanikiwa kupona huweza kurudi kwa kasi wakicheza kwa kiwango kile kile pengine na zaidi kwa sababu ya utunzaji mzuri wa miili yao wanapokuwa nje.
Kinyume na hapo ndio inayowakuta wachezaji wetu ambao huanza kulalamika na kusingizia mambo ya giza yaliyo nje ya ufundi wa mpira wa miguu, bila shaka Mwinyi atajiuliza vizuri na akubali kukoselewa ili aweze kurudi kwenye kiwango chake cha mwanzo.
Kwa sababu nchi bado inamhitaji Stars bado inamhitaji na klabu yake inamhitaji zaidi akae chini aiache miguu yake itoe majibu.
Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz