NINAVYOJUA : Kuna upotoshwaji mkubwa mechi ya Yanga na Coastal Union
Muktasari:
Mchezo huo ulivunjwa na mwamuzi Abdallah Kambuzi dakika 15 kabla ya muda wa nyongeza kumalizika katika mchezo uliopaswa kuchezeshwa kwa dakika 120, ambao mpaka unavunjika matokeo yalikuwa mabao 2-1 Yanga wakiwa mbele.
GUMZO na mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka ni matukio ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA kati ya Coastal Union dhidi ya Yanga ambalo lilichezwa Mkwakwani, Tanga na kushindwa kumalizika kutokana na kuvunjika.
Mchezo huo ulivunjwa na mwamuzi Abdallah Kambuzi dakika 15 kabla ya muda wa nyongeza kumalizika katika mchezo uliopaswa kuchezeshwa kwa dakika 120, ambao mpaka unavunjika matokeo yalikuwa mabao 2-1 Yanga wakiwa mbele.
Timu hizo zilimaliza dakika 90 matokeo yakiwa bao 1-1 na ndipo zikaongezwa dakika 30, lakini mara baada ya kufungwa kwa bao la pili la Yanga ndipo matukio ya kurusha mawe kutoka kwa baadhi ya mashabiki kuelekea kwa wachezaji wa Yanga na mshika kibendera yalianza na kumjeruhi mwamuzi huyo wa pili msaidizi.
Kifupi halia mbaya ya kiusalama kwenye Uwanja wa Mkwakwani baada ya vurugu hizo ndizo zilizosababisha kuvunjwa kwa pambano.
Baada ya mchezo huo kuna mengi yamesemwa na kuandikwa baadhi ya wadau wakidiriki hata kuwasifia wafanya vurugu bila kutahadharisha na mengine yakiwa hayana ukweli wowote zaidi ya kubeba sura ya kishabiki zaidi.
Mambo kadhaa yamepotoshwa kwa kutosemwa kweli yake, hivyo kuonyesha kama yanasaidia kuhalalisha vurugu michezoni.
Mwamuzi si chanzo cha vurugu
Unaweza kujiuliza ni namna gani mashabiki wa Coastal Union walivyoghadhabika hadi kufikia kurusha mawe, huku wachezaji waliokuwa uwanjani hawakumzonga mwamuzi kupinga goli la pili la Yanga! Hakuna shaka wachezaji wa Coastal walielewa uzembe walioufanya na kosa kubwa la mlinzi wao kumrudishia kipa mpira mfupi huku, kipa huyo akiliacha lango na kumfanya Tambwe afunge kirahisi. Hata baada ya Tambwe kufunga kwa wale wanaosema alitumia mkono bado wachezaji wa Coastal waliokuwa karibu hawakumlalamikia mwamuzi kwamba Tambwe kafunga kwa mkono! Kinyume chake mashabiki waliokuwa pembeni kushoto mwa lango la Coastal ndio walioonekana kukerwa zaidi hadi wao sasa kuanza kurusha mawe.Sioni kwa nini tumtupie lawama mwamuzi kuwa chanzo wakati mashabiki wa Coastal tatizo
Mmoja wa viongozi wa Coastal, amenukuliwa akisema waliompiga jiwe mwamuzi ni mashabiki wa Yanga. Unajiuliza mara mbili mbili hivi viongozi wa Coastal wa ngazi kubwa ya Ukatibu, tena kiongozi mzoefu kama Salum Bawazir anawezaje kubadili macho ya Watanzania tuliokuwa tukiangalia mchezo huo kuona mashabiki wa Yanga sehemu walikokaa ni alikokuwa mwamuzi msaidizi aliyejeruhiwa ambaye alikuwa mbele ya mashabiki tata wa Coastal. Unaweza pia kujiuliza hivi mashabiki wa Yanga waanze kumpiga mwamuzi huyo kwa kosa gani? Huu ni upotoshwaji mkubwa wa ukweli halisi wa mchezo huo ulivyokuwa. Kocha Ally Jangalu naye anamlaumu mwamuzi badala ya wachezaji wake. Ukishakuwa kocha tena wa kiwango kikubwa cha kusimamia timu inayocheza Ligi Kuu unatakiwa unapolalamika juu ya maamuzi ya refa utoe ushahidi mkubwa.
Kocha Jangalu hakutakiwa kumlaumu mwamuzi kwanza badala yake alitakiwa kutupia mzigo wa lawama kwa wachezaji wake, ilikuwaje timu yake ilifanikiwa kuishika Yanga kila idara na kutengeneza nafasi zaidi ya saba lakini walitumia nafasi moja tu kufunga! Coastal walifaidika na uchovu wa wachezaji wa Yanga zaidi wakafaidika kutokana na jinsi kocha wa Yanga alivyopanga plani yake kwa kuwaweka walinzi watano nyuma, kuwaweka viungo wawili, mshambuliaji mmoja kati na mawinga wawili waliocheza mbali na mshambuliaji huyo Donald Ngoma.
Hapo sasa unaanza vipi kumlaumu mwamuzi wakati hakuna mabao yaliyofungwa na vijana wake angalau ya wazi yaliyokataliwa?
Goli la Tambwe
Inashangaza kwa kumsikia mdau wa soka aliye mjini Dar es Salaam, anaposema bao lililofungwa na Amissi Tambwe wa Yanga lilitumia mkono! Katika kona gani mtu huyo kaliona bao vizuri, kwani picha ya marudio za kituo cha Azam TV zilishindwa kabisa kuonyesha Tambwe kutokea mbele badala yake ilikuwa ikionyesha kutokea mgongoni mwake.
Mwamuzi kachemsha?
Mwamuzi Abdalah Kambuzi aliyechezesha mchezo ule alilaumiwa sana kuhusiana na kutotoa kadi nyekundu kwa Oscar Joshua, lakini akaja kutoa kadi ua pili ya njano na mwisho nyekundu kwa Adeyum Saleh wa Coastal!
Ni kweli yalikuwa makosa kwa kutotoa kadi nyekundu, lakini bado kwangu ukiondoa kasoro hizo chache aliweza kulimudu pambano. Mwamuzi alimudu pambano.