NINACHOKIAMINI: Makufuli ya Simba Msimbazi na jina la Taifa Stars liwe Tembo
Muktasari:
- Ni vitu ambavyo vinatia moyo, vinavyokufanya uendelee kuupenda mpira na ndio maana kila Jumamosi na Jumapili watu hukusanyika katika sehemu mbalimbali kuangalia ligi za nje kwenye televisheni.
ZIMEBAKI kama siku nane kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil huku mataifa 32 yakiwa tayari kushiriki mashindano hayo makubwa katika soka.
Timu hizo zipo katika maandalizi makali, nyingine zipo ziarani zikiwa zinajiandaa na ndio maana tumeona England wakiwa tayari wametua Miami kuendelea na maandalizi hayo kabla ya kuelekea Brazil.
Tunaona pia klabu kubwa za Ulaya zikiwa katika hekaheka za usajili ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji wapya na kuajiri makocha wapya au kuongeza mikataba ya wachezaji na makocha.
Ni vitu ambavyo vinatia moyo, vinavyokufanya uendelee kuupenda mpira na ndio maana kila Jumamosi na Jumapili watu hukusanyika katika sehemu mbalimbali kuangalia ligi za nje kwenye televisheni.
Bila shaka kila mmoja angependa atembelee ofisi za timu yoyote ya Ulaya, labda ni Manchester United, Arsenal au Chelsea na nyinginezo.
Hebu fikiria unafika Carrington au Old Trafford zilizopo ofisi za Manchester United unakutana na makufuli yamefungwa mlangoni huku mashabiki wake wakilinda kwa mapanga, mashoka na mawe!
Hiyo inawezekana Simba tu, sidhani kama inaweza kutokea sehemu nyingine zaidi ya jengo la Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wasio na kazi walilundikana nje ya jengo la Msimbazi wiki iliyopita, wakafunga milango kwa makufuli na kuanza kuyalinda kwa mapanga na mawe ili kudhibiti watu wasiingie. Ni aibu sana.
Unapomzuia Katibu Mkuu wa klabu asiingie klabuni unataka nani afanye kazi za klabu? Yaani unamzuia mtendaji mkuu kuingia ofisini, halafu iweje?
Watendaji wakuu wa klabu ndio wamefanya mpango Arsenal kuingia mkataba na Purma, hawa ndio wamefanya Manchester United kutaka fedha nyingi zaidi katika mkataba mpya na Nike. Hawa ndio wanaajiri na kufukuza.
Anapotokea mtu amevaa kandambili zenye rangi tofauti, halafu anakwenda kufunga milango kwa makufuli chakavu huku akiwa na nyundo mkononi huyo hafai kuwa shabiki.
La ajabu na kusikitisha, kitendo hicho cha kijinga kikaungwa mkono na wapuuzi wengine na kusababisha shughuli zote za klabu kusimama.
Hawa ndio mashabiki ambao wanataka siku mmoja Simba itwae ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Hawa ndio wanaota klabu hiyo iwe na uwanja wa kisasa, hawa ndio wanajidanganya kuwa kuna siku klabu yao inaweza kununua ndege yake.
Kama aina ya mashabiki ndio hii, inayofikiria kuwafungia nje viongozi wake kwa makufuli yaliyochakaa huku wakijilinda kwa mashoka, unadhani kuna siku Simba inaweza kukaa meza moja na wakurugenzi wa Adidas au Nike na kuzungumza lugha inayofanana na Manchester United au Arsenal?
Kwa bahati mbaya zaidi, mashabiki hawa ndio baadaye hugombea nafasi za uongozi katika klabu au katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuendeleza mambo yao haya yasio na mbele wala nyuma.
Usishangae, kusikia TFF wanajifungia chumbani kwa saa kadhaa na unadhani wanajadili mambo makubwa, wanapotoka wanajisifu kuwa kikao kimekwenda vizuri na kwa kauli moja kamati ya utendaji imekubaliana kuwa jina la Taifa Stars libadilike, kisa? Halitishi. Wanataka timu iitwe Tembo au Nyati au Mamba. Duu!