Ndonga Zenji zilipotoka, zilipo na zinakokwenda

JAPO wanasema hakuna mahali imeandikwa moja kwa moja, lakini baadhi ya wazee wamekuwa na maelezo tofauti kuhusu ngumi kuzuiwa kuchezwa visiwani Zanzibar. 

Rais wa kwanza, Abeid Amaan Karume inaelezwa alizuia mchezo huo ambao aliuona ni wa kitwana na kulazimika kutoa tamko la kuuzuia kuchezwa visiwani humo.

Ilikuwa ni kabla ya kifo chake mwaka 1972, wakati huo akiwa madarakani, ndipo inaelezwa Rais Karume alipiga marufuku hiyo visiwani Zanzibar.

Wakati Wazanzibar wakijiandaa kusherehekea kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi, moja ya sikukuu kubwa za visiwa hivyo, mchezo wa ngumi maarufu kama Ndonga a.k.a Vitasa au Masumbwi nao unaingia kwenye historia hiyo, ulipotoka kabla ya Mapinduzi, ulipo na unakokwenda.

“Ulikuwa ukichezwa kabla, lakini nakumbuka Rais Karume aliuzuia baada ya mmoja wa mabondia kupigana na kuvunjwa mbavu,” anasimulia mmoja wa wazee visiwani humo.

Anasema aliwaambia ni mchezo wa kitwana, hautaki tena na hapo ndipo ngumi zikaachwa kuchezwa Zanzibar, haikuandikwa popote, lakini ndivyo ilikuwa hivyo na marais wengine waliofuatia waliendeleza marufuku hiyo hadi alipoingi Dk Hussein Ali Mwinyi.

Mzee mwingine anasema, kabla ya Mapinduzi, walikwenda Wacuba visiwani humo na kuwa wanawafundisha watu kucheza ngumi.

“Mpira wa miguu ndiyo ulikuwa ukichezwa hapa, ikawa wale waliojifunza ngumi wengi wao ukiwakorofisha kwenye mpira wanatumia ubondia wao kupiga wenzao kavu kavu.

“Ilienda hivyo, hadi baadae ndipo Rais akaona ni mchezo wa kikatili na kuuzuia kuchezwa hapa Zanzibar,” anasema mzee mwingine.

Bondia wa zamani ambaye sasa ni kocha wa ngumi visiwani humo, Salum Juma anasema wakati wa kukusanya maoni kuhusu mchezo huo kurejeshwa hawakupata muafaka wa kwa nini ulifungiwa.

“Ni kweli wazee walisema, lakini hakuna sehemu imeandikwa sababu na chanzo cha Rais Karume kupiga marufuku ngumi kuchezwa, miaka ya nyuma kidogo kuna watu walitaka kuzichapa kavu kavu bila glovu, hii pia ilikuwa ni hatari.

“Zilipigwa marufuku akiwa madarakani, tangu kifo chake (1972) ni miaka zaidi ya 50, awamu zote baada yake zimepita hadi Rais Mwinyi alipozirejesha.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ),  Said Marine ambaye pia marufuku hiyo aliikuta, anasema historia inaonyesha zamani ulichezwa bila kufuata sheria ikiwamo ya uzito na nyinginezo.

“Ulionekana ni hatari, Rais wa wakati ule akaufungia, baadae ikaanzishwa kickboxing na mashabiki wengi walijitokeza kuangalia, lakini nao ukapigwa marufuku hivyo mwamko ukaendelea kuwepo kwa mabondia kujifua na kwenda kucheza Bara.

“Alipoingia madarakani DK Mwinyi, ilionekana ipo haja ya kulitizama hili upya, ilipelekwa hoja Baraza la Wawakilishi, kisha Baraza la Mapinduzi ambao waliamuru ufanyike utafiti kuona ni jinsi gani mchezo utarudi.

“Asilimia 65 walisema uchezwe, wanawake wakiwa ni wengi zaidi wakitaka ngumi zirudishwe kuchezwa Zanzibar, Mheshimiwa mwenyewe alipitisha katika Baraza la Mapinduzi na ngumi zikarudishwa Zanzibar,” anasema.

Anasema, baada ya kuondolewa marufuku hiyo, BTMZ ilikuja na miongozo ikiwamo kuwepo kwa Kamisheni ambayo hivi karibuni watafanya uchaguzi wao baada ya uongozi wa muda.


KABLA YA KUREJESHWA ILIKUWA HIVI

Kocha Juma aliyejifunza ngumi miaka ya 1980 hadi 1990 akiwa skuli ya Mtambweni kisha sekondari ya Boza Pangani anasema wakati huo ngumi haukuwa mchezo rasmi.

“Ilikuwa ni mazoezi tu, baadae kuna mtu anaitwa Said Masatu alikuwa akicheza karate, akanipeleka gym kwake nikaanza kuwabadilisha wachezaji waliokuwa pale na kuwafundisha ngumi na kick boxing (ngumi na mateke).

Anasema Masatu alikuwa na pesa kidogo, wakaweka ulingo nyumbani kwa mtu na kuanza kuwapiganisha mabondia ambao alikuwa akiwapa kifuta jasho cha Sh2000 na 3000 kwa pambano kama mazoezi ya kupigana ana kwa ana (sparing).

“Ilikuwa tunafanya hivyo kwa kibali maalumu, hayakuhesabika kama mashindano, bali mazoezi, sheha ndiye aliruhusu kwa maombi maalumu pia.”

“Mabondia kutoka Zanzibar iliitubidi kutoa hela ili tununue mapambano tuweze kucheza kule Bara kama tulitaka kuingia kwenye renki za Boxrec (mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia).

Agosti 27, kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 50 ya marufuku ya ndondi, mabondia walizichapa  kwenye uwanja wa Mao Tse Tung, Rais, Dk Hussein Mwinyi ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Katibu wa Kamati ya ufundi na mashindano kwenye Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Zanzibar (ZaPBC), Hamis Said Seif ‘Mkali Swahiba’ anasema baada ya kurejeshwa klabu 48 zimesajiliwa.

“Mabondia ni wengi sana hapa Zanzibar, ukiachana na klabu hizo, pia kuna wanawake 15 katika kipindi hiki kifupi wanacheza ngumi, wanaume ni wengi zaidi, pia kuna wageni kutoka mataifa ya Ulaya nao wanapenda na tunao hapa gym (Zan City Unguja) wanajifua.

“Ambacho tunakikosa ni mapambano, tangu ufunguzi wa ngumi wa Agosti, hakuna pambano jingine lililochezwa, viongozi wetu wajipange kwenye hilo vyema, mabondia wanapojifua basi wapatikane mapromota ngumi zichezwe hata kila mwezi itasaidia kuwainua mabondia wa Zanzibar.”