Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tukifumba macho, tukifumbua, mkataba wa Tshabalala upo ukingoni

SHABA Pict

Muktasari:

  • Tuachane na Bocco. Aliendelea na maisha yake kwingine na yupo katika siku za mwisho mwisho kucheza soka katika kiwango cha juu. Tumuangalie Tshabalala. Ina maana alisaini mkataba mwaka huo ukiwa na mwendelezo wa mkataba ambao alisaini labda tufanye mwaka 2017.

NILIKUWA napitia mitandao nikisoma habari za nyuma. Nikakutana na hii habari ya Aprili 2021. Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na John Bocco ‘Adebayor’ wakisaini mikataba mipya ya kuendelea kuitumikia klabu yao ya Simba.

Tuachane na Bocco. Aliendelea na maisha yake kwingine na yupo katika siku za mwisho mwisho kucheza soka katika kiwango cha juu. Tumuangalie Tshabalala. Ina maana alisaini mkataba mwaka huo ukiwa na mwendelezo wa mkataba ambao alisaini labda tufanye mwaka 2017.

Kabla ya hapo inaonekana Tshabalala alisaini mkataba wa miaka mitatu wakati anaingia Simba kwa sababu kwa mujibu kwa Wikipedia inaonyesha aliingia Simba mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar. Ina maana baada ya miaka mitatu ya kwanza ameendelea kusaini mkataba wa miaka miwili miwili kila uchao.

Na sasa kila tukifumba macho na kufumbua ni rahisi kusikia mkataba wa Tshabalala unafika mwisho. Ndio, ni kwa sababu wachezaji wetu wanapewa mikataba ya miaka miwili miwili. Ina maana baada ya hapo alisaini mkataba mwingine wa miaka miwili mwaka 2023. Na sasa mkataba wake unakaribia kumalizika mwishoni mwa msimu.

Ina maana kwa sasa wana vikao tena mezani na Simba. Ina maana kwa muda mrefu Simba imekuwa ikitawaliwa na hofu ya kuona kiwango cha mchezaji kinaporomoka na ndio maana wameendelea kumpa mkataba wa miezi 24 tu.

SHAB 01

Kwanini mwaka 2021 hawakumpa Tshabalala mkataba wa miaka minne au mitano? Hapo katikati kwanini walilazimika kumpa mkataba mwingine? Najaribu kutafakari na kugundua kuwa hofu imekuwa ikizitesa klabu zetu.

Sio Simba tu. Klabu nyingine zinateswa na hofu hii ambayo inalazimisha warudi mezani baada ya miezi 24 tu. Sababu ya kwanza ni kwamba pande zote mbili zinakuwa hazina nia ya mkataba mrefu. Klabu ina hofu kwamba mchezaji anaweza kushuka kiwango au kuumia.

Upande wa mchezaji anaona ni bora achukue shilingi milioni 200 halafu baada ya miezi 24 arudi tena mezani kukomba noti nyingine. Mchezaji anajua kwamba akisaini mkataba wa miaka minne itamchukua muda mrefu kurudi mezani kukomba noti nyingine.

Ukweli mikataba hii inawanufaisha zaidi wachezaji ingawa bado na wao wanakuwa wanajihatarisha katika baadhi ya mambo. Kwa mfano, mchezaji akiumia katika msimu wake wa kwanza tu bado mkataba mrefu unambeba katika malipo yake. Hata uvunjwaji wa mkataba unakuwa mgumu.

SHAB 02

Wachezaji wetu hawapendi kuliona hili kwa sababu wanataka mkataba ambao utawarudishe mezani mara kwa mara. Kwa upande wa klabu nadhani ni wakati pia wa kubadilisha mambo na kujiamini katika masuala ya mikataba.

Mfano, mwaka 2019 Tshabalala alikuwa wa moto kama ilivyo leo na haikuonekana kama alikuwa anakaribia mwisho. Kwanini alipewa mkataba wa miaka miwili? Huwa hakuna utafiti kuhusu tabia binafsi za mchezaji, umri, na utimamu wake wa mwili kabla ya kumpa mkataba mpya?

Ningeweza kuelewa John Bocco kusaini mkataba mfupi wakati ule kwa sababu umri ulikuwa umeanza kumtupa mkono lakini vipi kwa Tshabalala ambaye kwa wakati ule umri wake ulikuwa miaka 22? Hapa ndipo huwa inanishangaza kidogo.

Inawezekana pia hili linatokea kwa sababu klabu zetu hazina nguvu za kiuchumi. Labda wachezaji wetu wanahitaji pesa nyingi kwa mkataba wa muda mrefu. Lakini bado klabu ina nafasi ya kulipa ada ‘sign-on fee’ kwa mafungu mafungu (installments).

SHAB 02 (1)

Katika hali halisi inakuwa rahisi kwa klabu kumpoteza mchezaji mzuri kama unampa mkataba wa miezi 24 tu. Lakini klabu inajiweka katika wakati mgumu wa kutoa mikataba mipya kwa wachezaji wengi klabuni. Mfano ni pale Yanga. Wachezaji wake watano wa kudumu katika eneo la kiungo wanamaliza mikataba yao ndani ya muda mmoja.

Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli wote wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu. Umeona wapi mpira wa hivi? Ni gharama kubwa kwa timu. Ingekuwa tofauti kidogo kama wachezaji wangekuwa na mikataba mirefu.

Hivi tunavyozungumza klabu inaweza kuwapa mikataba mipya wachezaji lakini ndani ya miezi 24 ijayo itakuwa inapambana tena kuwapa miaka mipya. Hofu ni kwamba huenda wachezaji hawa wakashuka viwango lakini kila msimu hali imekuwa hivyo hivyo.

Kila siku kuna hofu kwamba Khalid Aucho anaelekea mwisho lakini baada ya miezi 24 ijayo utamuona vile vile tu na klabu itapambana kumbakisha tena. Ndicho kinachotokea kwa Tshabalala na Simba kwa sasa. Tukifumba macho tukifumbua Tshabalala anajikuta anamaliza mkataba wake.

SHAB 04

Mbinu nyingine ambayo klabu haitaki kutumia ni kuongeza mkataba wa mchezaji wakati akiwa ndani ya mkataba. Wanasubiri mkataba ufike mwisho kabisa waanze kupambana na baadhi ya timu kwa ajili ya kupata saini ya mchezaji wao mwenyewe.

Kwa mfano, unaweza kusikia Simba inapambana na mchezaji wao wenyewe dhidi ya klabu kutoka Libya au Afrika Kusini. Kwanini upambane dhidi ya mchezaji ambaye kila siku uko naye kambini, mazoezini na ofisini?

Sijui kwanini hatuanzi kufuatilia mifumo ya wenzetu katika kusaini wachezaji. Mikataba ya miaka miwili miwili inakwenda hadi kwa wachezaji wenye umri mdogo. Inashangaza. Dickson Job kwa umri wake na nguvu zake kila siku Yanga wana hofu naye na wanampa mkataba wa miaka miwili miwili. Kwanini sio miaka mitatu? Au kwanini hapewi mkataba wa nyongeza baada ya kumaliza mwaka wa kwanza wa mkataba? Ni fumbo ambalo viongozi wanalifahamu zaidi.