Natamani kumsikiliza Mecky baada ya mechi za Yanga, Azam
Muktasari:
Unapata raha ya aina yake. Unamsikiliza Hemed Kivuyo wa ITV. Unapata raha hata kama unashindwa kuelewa kuwa anaripoti mechi kama shabiki au Mtangazaji. Unamsikiliza msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru.
SIKU hizi maisha yana burudani sana. ukishamaliza kutazama mpira katika uwanja wowote wa soka nchini, subiri saa moja linalofuata redio zetu zinaanza kuhoji au kuripoti matokeo ya mechi mbalimbali.
Unapata raha ya aina yake. Unamsikiliza Hemed Kivuyo wa ITV. Unapata raha hata kama unashindwa kuelewa kuwa anaripoti mechi kama shabiki au Mtangazaji. Unamsikiliza msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru.
Unamsikiliza msemaji wa JKT, Masau Bwire. Naye anatoa burudani huyu jamaa. Siku moja timu yake ilifungwa mabao 8-0 na Yanga, usiku wake Bwire akasema “Sijaona Yanga ilichokuwa inacheza, mimi naona walikuwa wanakimbiakiambia tu.” Unajikuta unacheka ghafla mbele ya watoto. Bao nane na bado walikuwa wanacheza ovyo?
Bado pia hapo hapo kuna burudani ya makocha. Jamhuri Kihwelo Julio anaendelea kutamba na timu yake ya Mwadui na sijui msimu ujao mambo yatakuaje. Lakini wakati wengine tukianza kumchoka Julio, taratibu Mecky Mexime wa Mtibwa naye anajitokeza kuwa mrithi wake.
Mecky naye ni burudani. Ana maneno yake machafu. Ukisikiliza maneno yake unaishia kucheka tu, hasa baada ya Mtibwa Sugar kutesa sana katika raundi ya kwanza. Siku moja nikamsikia akiwaponda wachezaji wa kigeni wote waliopo nchini. Kwake pale Manungu hakuna wachezaji wa kigeni.
Unaposhinda unaweza kuongea lolote. Bahati nzuri akachagua kuwaponda wachezaji wa kigeni waliopo nchini kwa sababu Mtibwa ilikuwa inashinda bila ya wachezaji wa kigeni.
Kwa mtazamo wangu ni vibaya kuwaponda wachezaji wote wa kigeni. Kuna wachezaji wa kigeni ambao ni wa ovyo na kuna wengine wazuri. Kuna wachezaji wa ndani ambao ni wa ovyo na wengine ni wazuri. Haya ndiyo maisha ya mpira.
Saa 24 baada ya Mtibwa Sugar kucheza mechi yake ya nane bila ya kushinda katika Ligi Kuu ikiwa na mastaa wa ndani waliompa Mecky kiburi dhidi ya Ndanda, wachezaji wa kigeni walikuwa wakizibeba Yanga na Azam katika michuano ya kimataifa. Nilitamani kusikia kitu kutoka kwa Mecky lakini sikusikia.
Mabao yote mawili ya Yanga yalifungwa na Mrundi Amiss Tambwe. Bao moja alifunga kwa krosi ya Mnyarwanda, Haruna Niyonzima. Hakuna haja sana ya kukumbusha ubora wa Tambwe. Msimu uliopita alikuwa mfungaji bora. Wazawa walikuwa wapi? Msimu mmoja kabla ya Tambwe, mfungaji bora alikuwa Kipre Tchetche wa Azam. Wazawa walikuwa wapi?
Wakati Tambwe akimaliza kazi katika pambano la BDF, saa 24 baadaye, watu watatu wa nguvu wa Azam walikuwa wanamaliza kazi Chamazi dhidi ya El Marreikh. Kulikuwa na soka la shoka kutoka kwa Serge Wawa Paschal ambaye hapana shaka alikuwa mchezaji bora wa mechi.
Wawa alikuwa kila kitu kwa Azam. Nadiriki kuamini kuwa bila ya Wawa huenda Azam ingepoteza mechi ile. Alikuwa kila kitu katika mipira ya juu na chini. Alicheza kazi. Alikaba mpaka kivuli. Alipiga vichwa asilimia 80 ya mipira iliyokuwa inaelekea lango la Azam.
Kipindi cha pili akaingia staa wa Mali, Mohamed Traore. Alionekana kuwa hatari sana, lakini Wawa alimficha kabisa kwa kumchezea soka la nguvu na akili. Mpira ulipoisha kila mtu akawa anaimba jina la Wawa uwanjani. Beki wa mwisho wa Tanzania kucheza katika kiwango kile michuano mikubwa kama ile anaweza kuwa Boniface Pawasa alipoisaidia Simba kufika robo fainali ya michuano ya Afrika mwaka 2003.
Achilia mbali Wawa, mbele alikuwepo Didier Kavumbagu. Alifunga bao la kwanza, kisha akatengeneza la pili baada ya kuruka vizuri na kuuparaza vema mpira wa kichwa wa kurushwa wa Erasto Nyoni. John Bocco akamalizia vizuri.
Achilia mbali mchango huu, lakini Kavumbagu ndiye aliyekuwa anawapa wakati mgumu mabeki wa El Marreikh. Yeye ndiye aliyekuwa anawaparamia na kutengeneza nafasi kwa wengine wacheze vema.
Mwingine aliyekuwa shoka ni Kipre Balou. Alikaba kama vile kesho haipo. Alipiga soka la shoka katikati. Kwa aina yake ya mpira, kwa sasa Tanzania kuna kiungo mmoja tu ambaye anaweza kupiga shoka kama lake. Bahati mbaya yupo naye katika timu moja, Himid Mao.
Baada ya kelele nyingi za Mecky kukejeli wachezaji wa kigeni wa Simba, Yanga na Azam, natamani kumsikiliza rafiki yangu Mecky baada ya Mtibwa kucheza mechi nane bila ya kushinda. Lakini pia baada ya Tambwe, Balou, Kavumbagu na Wawa kupiga soka la kazi wikiendi hii.
Nusura nimfanyie hisani ya Mecky kwa kusahau matokeo ya karibuni ya Yanga vs Mtibwa, Azam vs Mtibwa.
Kuna mtu anaweza kunikumbusha nini kilitokea?