Nabi, Robertinho wote ngoma nzito

KAZI inaanza. Ni wikiendi ya burudani. Achana na huko Ulaya, Afrika sasa kinawaka na miamba ya soka Simba na Yanga inashuka uwanjani kupepetana kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika zote ikianzia ugenini Guinea na Tunisia.
Simba inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Yanga inashiriki Kombe la Shirikisho. Patamu hapo.

Leo Jumamosi, Simba itakuwa wageni wa Horoya ya Guinea kabla ya kesho watani zao, Yanga kushuka uwanjani dhidi ya US Monastir ya Tunisia.

Miamba hiyo ya soka hapa nchini kulingana na maandalizi yao kabla ya kupanda ndege kwenda nchi hizo, ina matumaini ya kufanya vyema kutokana pia na aina ya matokeo na mafanikio waliyopata hivi karibuni ukiwamo usajili bora zilizofanya.

Hata hivyo, kazi kubwa iko kwa makocha wa timu hizo, Oliveira Robertinho wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga na watatakiwa kuhakikisha wanatimiza malengo ya timu hizo kama zilivyojiwekea ya kufika mbali kwenye michuano hiyo. Wataweza?

Kutinga robo fainali
Kulingana na mafanikio iliyopata Simba katika mashindano hayo ya kimataifa kwenye kipindi cha miaka minne iliyopita ukifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali mara tatu, msimu huu imejiwekea malengo zaidi ya hapo.
Lengo la kwanza ni kuvuka hatua ya makundi na kutika robo fainali. Hata hivyo, kuanzia viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki hawatakuwa na la kujivunia kwani haitakuwa mara ya kwanza.

Wakati Kocha Robertinho anapewa kazi Simba, mabosi wake walimweleza matamanio yao ya kuiona timu yao inafika nusu fainali na hapo watakuwa wamefanikiwa.
Kwa upande wa Yanga, Nabi ana kibarua cha kuhakikisha timu inafika robo fainali baada ya msimu uliopita na michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu kushindwa kufanya vizuri. Sasa wapo makundi na anasubiriwa kuona atafanya nini.

Mechi za nyumbani
Simba ni moja kati ya timu ambazo zimekuwa zinahakikisha zinashinda mechi za nyumbani kwenye hatua ya makundi. Utamaduni huu umekuwa kwao kwa muda mrefu na hata ikikutana na timu kubwa Afrika kama Al Ahly, RS Berkane na nyinginezo na ugenini inakuwa ya kawaida.

Msimu huu hatua ya awali, imefanya vizuri na imeshinda nyumbani na ugenini, dhidi ya Primeiro de Agosto bao 1-0, Nyasa Big Bullets 2-0 chini ya Kocha Juma Mgunda ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi.
Hivyo, kibarua kikubwa kwa Robertinho ni kuendeleza rekodi hiyo pamoja na kuhakikisha inashinda mechi za nyumbani kama kawaida yao.

Kazi ni nzito zaidi kwa Nabi ambaye tangu ametua Yanga hajawa na mwendelezo mzuri kimataifa na hajapata matokeo mazuri nyumbani. Ugenini ana sifa ya kuitoa Club Africain. Hivyo, atatakiwa ahakikishe Yanga inashinda mechi tatu za nyumbani na kupata pointi zote tisa ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kutokana pia na matokeo ya ugenini na inaweza kufanya vizuri.

Miamba ya Afrika
Simba na Yanga zimepangwa na timu ngumu katika makundi yao na kuna vigogo wanaopigiwa hesabu za kufanya vizuri katika makundi hayo.
Yanga itarudi nyumbani kucheza na TP Mazembe baada ya kumalizana na US Monastir na Nabi atakuwa na mtihani wa kuhakikisha inapata matokeo mazuri katika michezo yote miwili kutokana na rekodi nzuri ya miamba hiyo ya DR Congo.

Hata hivyo, Mazembe kwa kipindi cha hivi karibuni imekuwa na wakati mgumu na inaweza isiitishe sana Yanga.
Kesho Jumapili, Yanga itaanza dhidi ya US Monastir ukiwa ni mtihani mwingine kwa Nabi ugenini na itakipiga na Real Bamako ya Mali baada ya kukutana na Mazembe nyumbani.

Simba itakutana na miamba Raja Casablanca ya Morocco na ni mtihani kwa Robertinho kuhakikisha anapata pointi tatu mchezo wa kwanza wa nyumbani.
Kocha huyo anaanza kazi yake kimataifa leo dhidi ya Horoya ya Guinea na Vipers ya Uganda iliyotinga hatua hiyo wakati ikinolewa naye.

Rekodi zao CAF
Simba ilimchukua Robertinho baada ya kuwa na rekodi nzuri ya kuivusha Vipers hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipata ushindi ugenini dhidi ya TP Mazembe ambayo ina rekodi nzuri ya kutwaa taji hilo mara tano.
Mabosi wa Simba wana imani na kocha huyo ya kuipa matokeo mazuri timu hiyo ikiwamo kushinda dhidi ya vigogo hasa ugenini.
Hata Robertinho mwenyewe amekuwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Kocha wa Yanga, Nabi tangu ameichukua timu hiyo ameiongoza kwenye mechi nane za mashindano ya CAF, akipata ushindi katika michezo mitatu, kufungwa mitatu na kutoka sare miwili.
Alianza kwa kupoteza michezo miwili ya CAF 2021 dhidi ya Rivers United ya Nigeria kabla ya msimu huu kushinda michezo miwili ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini.

Hata hivyo, alishindwa kuivusha Yanga hatua ya makundi baada ya sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Al Hilal ya Sudan kabla ya kwenda kufungwa bao 1-0 ugenini.
Kutinga hatua ya makundi, Yanga ilitoka suluhu dhidi ya Club Africain nyumbani kabla ya kwenda kuifunga  1-0 ugenini.
Hivyo, kutokana na ubora walionao msimu huu ukiwamo usajili mzuri, mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wanatamani kuona kocha huyo anawavusha hatua hiyo na zaidi kwani itakuwa ni furaha kwao kutokana na muda mrefu kupita wakiishia hatua za awali.

Wasikie hawa
Ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe anasema malengo yao ni kuhakikisha kikosi hicho msimu huu kinavuka hatua ya makundi na kutinga robo fainali na hilo linawezekana kutokana na maandalizi yao.

“Kwanza tunahitaji kuvuna pointi zote tisa kwa kushinda michezo mitatu ya nyumbani baada ya hapo ni kuangalia namna gani tunaweza kupambana ugenini ili kupata pointi za huko,” alisema Kamwe na kuongeza;

“Ukiangalia kundi letu lilivyo kuna aina ya timu ambazo tunaweza kupata pointi zote tisa kwenye uwanja wetu wa nyumbani na hata ugenini tunaweza kupata hasa sare na tukavuka hatua hii.”
Mchezaji wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema kwenye mashindano hayo ya CAF, kabla ya kufikiria pointi za ugenini Simba na Yanga kila mmoja inatakiwa kuwa na uwezo wa kushinda mechi zote tatu za nyumbani.

“Ukiangalia aina ya timu zilizopo kwenye makundi yote ya Simba na Yanga zitaweza kupata pointi tisa nyumbani, basi hazitaweza kukosa hata moja ugenini na zikasonga robo fainali,” anasema Pawasa na kuongeza;
“Michezo ya ugenini inakuwa na mambo mengi kuanzia ushindani mkali ndani ya uwanja kutoka kwa wapinzani kwani