Mziki mnene, hii ndo' Yanga Princess mpya

NJINIA Hersi aliahidi kama Yanga haitachukuwa ubingwa lawama zote ziende kwake basi na mimi naahidi kama Yanga Princess isipochukuwa ubingwa kwa msimu ujao basi mnilaumu mimi.”

Hayo ni maneno ya Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji, wakati wa kampeni zake za kuwania kiti hicho miezi michache iliyopita akizungumzia kufanya mapinduzi makubwa kwenye soka la wanawake.

Na kweli baada ya kuchaguliwa akishirikiana na watendaji wengine ndani ya Yanga wameanza kubadili na kuendeleza mambo mazuri yaliyokuwepo kwa matumaini chanya.

Achana na yote hayo, Yanga imeingia sokoni na kuwasajili wachezaji wenye ubora kutoka mataifa mbalimbali ili iweze kupindua meza ya watani zao Simba Queen iliyochukua mara tatu mfululizo, JKT Queens iliyobeba mara mbili mfululizo na Mlandizi Queens iliyobeba mara moja katika msimu wa kwanza kabisa.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea uchambuzi wa kikosi kipya cha Yanga chini ya kocha mwanamke mwenye Lesen A ya CAF, Edina Lema ‘Mourinho’.


NKOR BLESSING AUGUSTINE

Huyu ni mmoja kati ya Wanigeria wapya watano waliosajiliwa na Yanga kwenye dilisha kubwa la usajili na wapo tayari kupeperusha bendera ya njano na kijana.

Nkor ni mshambuliaji aliyejiunga na Yanga akitokea Sunshine Queens aliyoichezea msimu uliopita lakini kabla ya hapo alikuwa akikiwasha Ibom Angels zote za Ligi Kuu Nigeria.


WOGU CHIOMA SUCCESS

Mnigeria wa pili ni kiungo huyu fundi mwenye uzoefu wa kutosha amewahi kucheza soka la kulipwa nchini Belarus kwenye Klabu ya Minsk FK.

Chioma pia amewahi kuzichezea Confluence Queens, Rivers Angels na Edo Queens zote za Ligi Kuu ya Wanawake Nigeria. Fundi huyu anasifika kwa kupiga pasi na kukaba kwa usahihi.


SAIKI MARY ATINUKE

Huyu naye ni kiungo mpya wa kutoka Nigeria aliyesaini kwa Wanajangwani hao akitokea Rivers United ya Ligi Kuu ya kwao. Saiki pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Nigeria na alikuwa kwenye kikosi cha timu U-20 iliyoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2018 Ufaransa.


NADEGE ATANHLOUETO

Huyu Yanga imemnasa kutoka Benin alikokuwa akikipiga ndani ya kikosi cha Dyanamique FC. Nadega ambaye ni nahodha wa Timu ya Taifa ya Benin amewahi kucheza soka la kulipwa nchini Togo katika Timu ya Athleta, Confluence Queens ya Nigeria atakuwa Jangwani akikiwasha kwa takribani miaka miwili.


MAIMUNA HAMIS

Yanga imezama kwa watani zao Simba na kuibuka na staa wao Maimuna. Maimuna anayemudu kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani amesaini Yanga baada ya kuvunja mkataba wake na Simba.


TESSY KESIENA BIAHWO

Huyu ni fundi mwingine Yanga iliyempandisha ndege kutoka Nigeria hadi mitaa ya Jangwani tayari kwa kuwatumikia Wananchi.

Tessy ni kiungo wa kati aliyechezichezea timu zote za taifa za Nigeria za wanawake na sasa yupo kwenye kikosi cha timu kubwa.


MERY MUSHIYA

Wananchi kama kawaida yao, wamefika DR Congo ndani ya Timu ya Taifa ya wanawake na kumsainishaa staa huyu.

Mery anayecheza eneo la ushambuliaji amejiunga na Yanga akitokea katika Klabu ya Amani ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu wanawake nchini DR Congo.


FOSCAH KANENGE

Huyu ni beki kisiki aliyesajiliwa na Yanga akitokea Kenya akimudu kucheza pia eneo la kiungo mkabaji. Foscah pia yupo kwenye Timu ya Taifa ya Kenya na amejiunga na Yanga akitokea Zatech Sparks.


PAULINE KUTHURUH

Huyu ni kipa mpya wa Yanga raia wa Kenya aliyesaini kandarasi ya miaka miwili kusimama kwenye milingoti mitatu ya Wananchi.

Pauline ni mahiri langoni amejiunga na Yanga akitokea Gaspo FC lakioni pia aliwahi kuichezea BlueStars Diaspora zote za kwao Kenya.


KAARI WINCATE

Huyu ni beki mwingine Mkenya aliyesajiliwa na Yanga katika dirisha hili la usajili akitokea Thika Queens ya nchini kwao.

Wincate anayecheza beki ya kushoto na kati pia ni miongoni mwa wachezaji wanaounda Timu ya Taifa ya Kenya.


PRECIOUS ONYINYECHI

Huyu ni Mnigeria wa tano kusajiliwa na Yanga Queens katika maboresho ya kikosi chao.

Precious ni kiungo wa kati mwenye mambo mengi akitumia mguu wa kushoto pia anacheza kama winga wa kushoto. Yanga sasa inasubiri msimu uanze ili mafundi wake hao waanze kuonyesha makali yao.