Prime
Wasauzi wafika bei kwa Mukwala

Muktasari:
- Akizungumza leo Julai 10, 2025 jijini Dodoma, Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Inspekta Frank Lukwaro, amesema uongozi wa timu hiyo umejiridhisha na uwezo wa Makatta, hasa kutokana na historia ya kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu msimu wa 2018/2019.
MABOSI wa Simba wanaendelea kusuka kikosi hicho kimyakimya kwa mapendekezo ya kocha Fadlu Davids, aliyepo mapumziko kwa sasa, lengo likiwa ni kurudi katika msimu mpya wa mashindano wakiwa wa motoo.
Hata hivyo, mabosi hao kwa sasa wanasikilizia dili la fedha ndefu kutoka kwa klabu mbili maarufu Afrika zinazotaka kumng'oa straika wa mabao wa klabu hiyo Steven Mukwala aliyeitumikia timu hiyo msimu uliiopita na kuifungia mabao 13.
Straika huyo raia wa Uganda aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Asante Kotoko ya Ghana inadaiwa huenda asiwe sehemu ya kikosi hicho kwa msimu wa 2025-2026 baada ya klabu za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na RS Berkane ya Morocco kupeleka ofa Msimbazi wakitaka kumnasa.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba Wasauzi wamewasilisha ofa ndefu kwa Simba ikihusisha Dola 350,000 ( zaidi ya Sh 900 milioni) ikiizidi ile ya Wamorocco walioweka Dola 300,000 ( zaidi ya Sh 780 milioni) ili kumsajili Mukwala na mabosi wa klabu hiyo inadaiwa kuridhia kumuacha.
Inaelezwa hesabu za mabosi wa Simba ni kukutumia mauzo ya Mukwala ili kuleta mashine nyingine mpya katika eneo hilo ikiwa ni pendekezo la kocha Fadlu aliyetaka aongezewe straika mkali zaidi kuliko alikuwa nao akiwamo Mukwala, Leonel Atena na mzawa Valentino Mashaka.
Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa Kaizer Chiefs wamefika dau la kumnunua mshambuliaji huyo na dili hilo linatajwa huenda likakamilika kabla ya Simba kutimkia nje ya Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya msimu huu.
"Ni kweli tumefikia makubaliano ya kumuuza Mukwala kwenda Kaizer na dili hilo linatarajia kukamilika kabla ya sisi kuondoka nchini Julai 25 kwa ajili ya kuingia kambini kujiandaa na msimu mpya," alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
"Mukwala tulimnunua kwa dola 150,000 lakini sisi tumepokea ofa ya dola 350,000 hii imepanda baada ya RS Berkane pia kuonyesha nia ya kumhitaji mshambuliaji huyo na wao wakiweka mezani dola 300, 000 ili kutushawishi tuweze kuwauzia nyota huyo."
Inaelezwa wakati Berkane ikiendelea na mazungumzo ya kuhitaji huduma ya Mukwala, Wasauzi waliamua kuingilia kati dili hilo kwa kuweka dau nono ili kumchomoa nyota huyo kutoka kwenye viunga vya Msimbazi kutokana na kuvutiwa naye kupitia mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo Siomba ilifika fainali na kupoteza kwa mabao 3-1 mbele ya Berkane.
Mukwala aslisajiliwa Simba msimu uliomalizika hivi akribuni kwa mkataba wa miaka mitatu, tayari ametumikia mwaka mmoja akiwa amefunga mabao 13 na asisti tatu katika Ligi Kuu Bara ambapo timu hiyo ilimaliza nafasi ya pili nyuma ya Yanga iliyotetea taji kwa msimu wa nne mfululizo.
"Makubaliano ya pande zote mbili kati yetu sisi Simba na Kaizer Chiefs yamekamilika kilichobaki ni fedha za mauzo kuingia katika akaunti ya klabu kabla ya timu kuanza safari ya kuelekea katika kambi ya kujiandaa na msimu mpya."
Alisema timu inatakiwa kuondoka kamili ikiwa imekata tiketi za nyota watamaliza maandalizi kuanzia mwanzo hadi mwisho huku akithibitisha kuwa hadi Julai 25 nyota ambao hawana mpango nao watakuwa wamekamilisha makubaliano.
NOUMA NDO BASI
Katika hatua nyingine, Simba imeachana na beki wa kushoto wa Simba, Valentin Nouma kwa mapendekezo ya pande mbili na tayari beki huyo raia wa Burkina Faso ameshawaaga mashabiki wa klabu hiyo aliyoitumikia kwa mwaka mmoja tangu alipotoka FC Lupopo ya DR Congo.
Beki huyo alitumia ukurasa wake wa instagram kuweka bayana kwamba hatakuwa sehemu ya kikosi hicho, huku taarifa nyingine zikielezwa sababu hasa ya kuondoka Msimbazi ni kukosa nafasi ya kucheza, lakini mmoja wa viongozi wa Simba alisema beki huyo hakufikia malengo.
"Ni mmoja ya wachezaji walioshindwa kufikia malengo waliyowekewa wakati wanasajiliwa mwanzoni mwa msimu uliopita. Simba ina malengo na kila mchezaji amesajiliwa ili kuhakikisha anaipigania timu na kuonyesha ushindani kwa wchezaji wenzake, ndio maana tumeanza kuwafyeka baadhi yao," alisema mmoja wa viongozi wa Simba alipoulizwa juu ya taarifa za kutemwa kwa beki huyo.
Kabla ya kutua Simba, Nouma amewahi kukipiga AS Douanes na Rahimo FC za Burkina Faso kabla ya kutua FC Lupopo mwaka 2023 na Julai mwaka jana ndipo akanyakuliwa na Wekundu wa Msimbazi.