Prime
Anga za kimataifa... Mastaa wazawa wanakwamia hapa!

Muktasari:
- Pia imeshuhudia Kagera Sugar na KenGold zikishuka daraja zikizipisha Mtibwa Sugar na Mbeya City zikirejea katika Ligi Kuu baada ya kufanya vyema katika Ligi ya Championship, huku Fountain Gate ikipambana na kusalia ligi hiyo ikiizuia Stand United iliyokuwa ikipambana kurejea.
MSIMU wa Ligi Kuu Bara umemalizika kwa kushuhudia Yanga ikitetea taji msimu wa nne mfululuizo, huku Simba, Azam na Singida Black Stars zikiifuata nyuma na kukata tiketi za michuano ya kimataifa kwa msimu ujao, mbili zikicheza Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho Afrika.
Pia imeshuhudia Kagera Sugar na KenGold zikishuka daraja zikizipisha Mtibwa Sugar na Mbeya City zikirejea katika Ligi Kuu baada ya kufanya vyema katika Ligi ya Championship, huku Fountain Gate ikipambana na kusalia ligi hiyo ikiizuia Stand United iliyokuwa ikipambana kurejea.
Lakini wakati ligi ikiwa imefikia tamati, tayari baadhi ya klabu zilishaanza mapema kupiga hesabu za msimu ujao imchukue mchezaji yupi wakati wachezaji nao wakipiga hesabu watimkie wapi.
Wapo wachezaji ambao wanapiga hesabu za kubaki nchini lakini kiu ya wengi ni kuona wachezaji wazawa wakipata nafasi ya kucheza soka nje ya Tanzania hususan Afrika na kwingineko.
Idadi ya wachezaji wa Kitanzania kwenda kucheza soka Ulaya sio kubwa lakini yametajwa mambo saba ambayo yanawangusha kupata nafafasi ya kujiuza kwenda kucheza ligi zenye ushindani zaidi
MAUMBILE
Changamoto ya kwanza ambayo imetajwa kuwaandama wachezaji wa Kitanzania ni maumbile yao, wengi wanaonekana kuwa na maumbile dhaifu au ufupi na hili linatokana na hatua ya ukuaji wao kuanzia nchini.
Hili liliwahi kumkumba winga wa zamani wa Yanga Mrisho Ngassa wakati alipotakiwa kutua West Ham United ya England lakini pia kimekuwa kikwazo cha wachezaji wengi kutokana na maumbo yao.
Wachezaji wengi vijana hawajui kufuata ushauri wa vyakula gani wanatakiwa kuzingati kuvila wakati wako kwenye hatua ya kukuza misuli yao ya mwili na kuwasababisha kudumaa.
KUKABILI CHANGAMOTO MPYA
Wachezaji wengi wanatamani kwenda kucheza Ulaya lakini hawako tayari kujitoa kuvumilia changamoto watakazokutana nazo huko wakati wanajitafuta, wapo wachezaji kutoka Afrika Magharibi wanaweza kutoka nchini kwao wakijua wanakwenda Ulaya na jawana uhakika wa kulipwa kabisa lakini ni rahisi kwao kuvumilia wakijua kujituma kwao kutabadilisha kila kitu. Wapo baadhi ya wachezaji wetu waliwahi kuwenda klabu kubwa Ulaya lakini wakashindwa kukabiliana na changamoto chache na kuamua kurudi nchini.
MTINDO WA MAISHA
Klabu mbalimbali zinapomfuatilia mchezaji zitafuatilia taarifa mbalimbali kuanzia zile za uwanjani na hata binafsi, wapo skauti wa soka ambao wanaweza kuangalia taarifa zinazowekwa kwenye mtandao wa kijamii kisha kuzitumia kutafuta mechi husika.
Mfano mzuri hivi sasa wapo wachezaji kwenye klabu kubwa hutengeneza picha maalumu ya mechi wanayokwenda kucheza siku ya mchezo na kuweka kwenye kurasa zao, hilo linaonyesha namna ambavyo mchezaji husika anajitambua na kurahisisha mawakala kufuatilia mikanda ya mechi husika kujua alionyesha kiwango cha namna gani.
Hapa kwetu imekuwa tofauti, wakala mmoja kutoka Russia aliwahi kuonyeshwa mchezaji wa kutoka klabu kubwa na alipoamua kufuatilia akakutana na video akicheza muziki wa taarabu siku ambayo alikuwa na mechi ngumu.
USIMAMIZI MBOVU
Hii ni changamoto nyingine kubwa wachezaji wengi wameshindwa kujua ni aina gani ya watu sahihi wanaotakiwa kuwasimamia kama meneja au wakala wake, wapo ambao wanawachagua ndugu, kaka, baba wapo wengine wanawachagua marafiki au umaarufu wa mtu.
Changamoto inakuja watu hao wamekuwa wanashindwa kuwasimamia kutafuta nafasi kubwa kwenye klabu kubwa kutokana na kukosa koneshkeni na maskauti au viongozi wakubwa.
Hili limekuwa hatari hata pale inapotokea changamoto ya kimkataba wanashindwa kujua ni namna gani wataweza kuwasaidia kabla ya kusaini mikataba hiyo husika.
REKODI BINAFSI
Wapo wachezaji hawana hata mikanda ya video zake au hata vile vipande (clip) ambazo zitawasaidia kuwaelezea juu ya vipaji au ubora wao, unakuta meneja wake anaulizwqa una takwimu za mchezaji wako? Jibu lake linakuwa hana au hata mchezaji mwenyewe hana.
MALENGO
Ukiwauliza wachezaji wengi utasikia malengo yangu ni kucheza soka Ulaya lakini kwa kiwango anachokionyesha uwanjani hakiakisi malengo ambayo amejiwekea.
Mchezaji mwenye malengo makubwa hujituma kwa nguvu na sio rahisi kukata tamaa kushindana pale anapokutana na changamoto, wachezaji wengi wameamua kuishi na kufifisha hesabu kubwa kutokana na kuamua kuridhika kirahisi.
KUJIENDELEZA
Wako wachezaji wamewahi kupata nafasi kubwa ya kuonekana na maskauti wakubwa lakini lugha tu ya namna ya kujieleza imekuwa ngumu, mchezaji anazichezea klabu kubwa Simba au Yanga lakini anashindwa kutambua kama angeamua kujifunza hata Kiingereza tu cha kuzungumza itamsaidia katika safari yake ya kutimiza malengo.
Wapo wasanii wa muziki wa kizazi kipya hawakusoma elimu ya darasani kwa kiasi kikubwa, lakini walitambua umuhimu wa kujua lugha kama Kiingereza au hata Kifaransa na kuamua kujifunza na ukikutana nao wanazungumza lugha hizo mithili ya watu wenye elimu kubwa, lakini kumbe waliamua kutumia kipato chao kujifunza ili watimize ndoto zao kimataifa.