MZEE WA UPUPU: Tuanzishe Ligi mpya ya maendeleo

Rais wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) , Wallace Karia.
KIUFUNDI mtalaa wa akademi ya soka kwa watoto wa miaka saba na mwisho wake ni miaka 17.
Kuanzia miaka 18 mtoto anatakiwa kuingia kwenye soka la ushindani kama mchezaji wa kulipwa...anasaini mkataba rasmi.
Lakini darasa moja la akademi linaweza kuwa na watoto 15 waliohitimu. Hakuna timu inayoweza kuwaingiza hawa wote kwenye kikosi chao cha kwanza. Kwa hiyo itabidi wasubiri nafasi yao huku wakiendelea kukua.
Watoto hawa wanaungana na wengine 15 waliomaliza mwaka jana, ambao sasa wana miaka 19.
Na wale wengine waliomaliza mwaka juzi ambao sasa wana miaka 20. Na wale wa mwaka ule wa nyuma kabla ya mwaka juzi ambao sasa wana miaka 21.
Ukifuatilia mfululizo huu utaona kuna wachezaji wengi sana wamezalishwa hapa kati lakini hawapati nafasi ya kucheza.
Katika hali ya kawaida, mtoto wa miaka 18 hadi 23 anaweza akawa hajapevuka vya kutosha kuweza kuingia kwenye mikikimikiki ya ushindani wa Ligi Kuu.
Ligi za vijana tulizonazo zinaishia chini ya miaka 20, maana yake mwisho ni miaka 19.
Sasa hawa wengine wanacheza wapi, ikiwa bado hawajapata nafasi kwenye timu kubwa? Sasa chukua hao changanya na hawa hapa.
Balama Mapinduzi aliumia na kukaa nje kwa muda mrefu sana. Baadaye akapona, lakini hadi leo hajapata nafasi ya kucheza kwenye timu yake.
Wachezaji wenye hali kama ya Balama Mapinduzi wako wengi sana. Hawa wanapata wapi muda wa kucheza ili kulinda vipaji vyao? Makundi haya mawili yanatakiwa yaandaliwe ligi yao, ndiyo hiyo inayoitwa ligi ya maendeleo.
Ligi kama hizi zipo sana kwa wenzetu walioendelea na zinasaidia kulinda na kuendeleza vipaji vya wachezaji. Mchezaji kama Idd Nado wa Azam FC ambaye ameumia na atakuwa nje kwa takriban mwaka mzima atakapopona na kurudi uwanjani, angetakiwa aanzie huko kwanza.
Ligi kama hizi huhusisha wachezaji kuanzia miaka 18 hadi 23 pamoja na wale wenye umri uliozidi hapo lakini waliokuwa majeruhi kwa muda mrefu au hawapati nafasi kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao.
Kiufundi ligi kama hii huitwa LIGI YA MAENDELEO yaani ipo kwa ajili ya kuwaendeleza wale ambao hawajawa tayari kucheza katika ushindani wa Ligi Kuu, lakini wameshavuka ngazi za akademi.
Ligi kama hizi zipo hata kwenye michezo mingine kama mpira wa kikapu (NBA) ambako huitwa D-League. Hasheem Thabeet, Mtanzania wa kwanza kucheza NBA alipelekwa kwenye ligi kama hii mara kadhaa akiwa na timu mbalimbali kubwa zinazocheza NBA.
Kuanzisha mashindano ni gharama, hasa kama haya ambayo hayavutii sana wadhamini, lakini hiyo ndiyo gharama ya maendeleo.
Mahitaji ya soka la kisasa yametusukuma kutunga kanuni mbalimbali ikiwemo ulazima wa kila klabu ya Ligi Kuu kuwa na timu za vijana.
Sasa vijana hawa wakishaendelezwa ndiyo wanaleta ulazima mwingine wa kuwa na ligi zao - ndizo hizi zinazoitwa ligi za maendeleo.
England kwa mfano, kuna ligi ya aina hii inayoitwa Professional Development League (PDL) na ilianzishwa mwaka 2012 kuchukua nafasi ya ligi nyingine kama hiyo iliyoitwa Reserve League yaani ligi ya wachezaji wa akiba.
Ni muhimu kuwa na ligi kama hii, kama siyo sasa basi hata baadaye kidogo...lakini iwemo kwenye mipango na malengo.