MZEE WA UPUPU: Injinia Hersi Said alipoishi kiinjinia

JUNI 11 ilikuwa siku ya kutangaza majina ya wagombea waliopita kwenye mchujo wa awali wa uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga. Muda mfupi kabla majina hayajatoka zikaanza kusambaa picha za mmoja wa wagombea, Injinia Hersi Said zikimuonyesha akiwa na Stephane Aziz Ki, mmoja wa wachezaji wanaotamaniwa sana Tanzania.

Ukiunganisha nukta kwenye matukio haya mawili utaona Hersi Said alicheza karata zake ‘kiinjinia’ kwelikweli. Ukitaka kupata picha halisi ya matukio haya rudi kwenye tafsiri ya neno injinia katika muktadha wa maisha ya kawaida. ‘Ni mtu anayebuni au kuunda jambo au tukio’.

Lakini hata tafsiri ya kisayansi haipo mbali sana na hiyo ya maisha ya kawaida. Toa tu neno jambo au tukio weka injini au mashine...mengine ni yaleyale. Sasa rejea kwenye matukio hayo mawili ya mchujo wa wagombea na picha ya Hersi Said halafu weka neno injinia katika tafsiri ile ya kwanza.

Kwa historia ya chaguzi zote duniani mara nyingi siasa hutawala hasa kwenye nyakati hizi za mchujo. Hutokea wagombea wanaopewa nafasi kubwa wakakatwa na kujikuta walikosa pa kutokea. Hali hii Hersi aliijua na kuinjinia ajali ya kipropaganda.

Siku ya kutangazwa majina yaliyoingia kwenye mchujo iende sambamba na picha zake akiwa na ‘wild card’, Aziz Ki. Endapo jina lake lingekatwa hizi picha zingeamsha hasira za mashabiki wengi sana wa Yanga na kuutia presha uongozi unaosimamia mchakato. Ni shabiki gani ambaye angeelewa kukatwa kwa jina la Hersi mtu anayetaka kuwajengea timu kwa kumleta fundi kama Ki? Hapo Hersi aliinjinia kitu kikubwa - tena sana.

Na hii ndiyo maana ya kuwa injinia unatakiwa kuiona kesho tangu jana. Injinia siyo mtu wa kushtukizwa na mambo wala siyo mtu wa kuandaliwa mambo. Yeye ndiye anatakiwa kuyaandaa na kuwashtukiza watu. Na hiki ndicho alichokifanya Hersi.

Ukirudi nyuma kwenye historia za uchaguzi wa Yanga mara nyingi umekuwa ukigubikwa na mizengwe ya hali ya juu. Mwaka 2010 uchaguzi uliomuingiza madarakani Lloyd Nchunga pale PTA Sabasaba ulishuhudia Francis Kifukwe akichinjwa hivi hivi bila aibu.

Sidhani kama Hersi alikuwa anaijua Yanga wakati huo, lakini kama injinia wala hatakiwi kukumbushwa na mkasa wa Kifukwe anatakiwa kukumbushwa na uinjinia wake tu, basi. Ukiachilia mbali kukwepa mkasa kama wa Kifukwe, Hersi pia alikuwa anatafuta nguvu ya umma endapo jina lake lingekatwa.

Nguvu ya umma ingelazimisha mchakato uanze upya kama kilichotokea kwenye uchaguzi uliopita ambao ulimuingiza madarakani rais anayemaliza muda wake, Dk Mshindo Msolla 2019. Uchaguzi huo ulitakiwa kufanyika 2014 lakini mwenyekiti wa wakati huo, Yusuph Manji akauahirisha hadi 2015.

Manji ambaye aliingia madarakani 2012 katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi ya Lloyd Nchunga aliyejiuzulu alitakiwa aitishe uchaguzi mkuu 2014, lakini akasema kuna mambo mazuri ya Yanga hajayamaliza hivyo akawaomba wanachama wamuongezee muda wa mwaka mmoja. Ilikuwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika pale Police Officers’ Mess, Oysterbay, Dar es Salaam.

Mwaka alioomba ukaisha na uchaguzi ukatakiwa kufanyika 2015, lakini ukaahirishwa tena ikielezwa haiwezekani Yanga ifanye uchaguzi wake katika mwaka ambao pia nchi inafanya uchaguzi mkuu. Hoja hii pia ilishawahi kutolewa na Kanali Mstaafu Idd Kipingu pale Police Officers’ Mess katika ile siku Manji anaomba aongezewe mwaka mmoja.

Japokuwa baadhi ya wanachama waliipinga siku ile, hata Manji mwenyewe pia aliipinga, lakini akaja kuitumia ule mwaka aliouomba ulipoisha. Haya 2015 ikapita uchaguzi unatakiwa kufanyika 2016 ukashindikana. Mwaka 2017 serikali ikaingilia kati kulazimisha uchaguzi na kupanga ufanyike mwaka huo.

Kwa kuwa Manji alikuwa kipenzi cha wana Yanga wakaungana kuipinga serikali. Kila mchakato ukianza unavurugwa makusudi ili ukwame. Waziri aliyekuwa na dhamana, Dk Harrison Mwakyembe alicharuka na kutangaza kuwafungia maisha baadhi ya wanachama wa Yanga kwa kuingilia mchakato.

Lakini mwisho wa siku nguvu ya umma ikashinda na mchakato uliolazimishwa na serikali ukakwama. Serikali ikawaachia Yanga wenyewe wafanye uchaguzi wao ndipo 2019 ukafanyika na Dk Mshindo Msolla kuingia madarakani. Ni nguvu hii ndiyo injinia Hersi aliilenga. Alijua fika kwamba endapo zengwe kama la Kifukwe lingemtokea, ile picha yake akiwa na Aziz Ki ingeamsha nguvu ya umma na kuvuruga uchaguzi hadi awemo.

Na akisharejeshwa tu, basi ndiyo tiketi ya moja kwa moja hadi ushindi wa kishindo. Hata hivyo, licha ya kwamba hakukutana na mkasa wa Kifukwe ili mtego wa nguvu ya umma ufyatuke, lakini ile picha imerahisisha uchaguzi kwa njia nyingine. Umaarufu wa injinia umekuwa maradufu kiasi kwamba watu wamesahau kabisa kuwa huyu ndiye Hersi aliyesema ameshamalizana na Kapteni Tshishimbi na Bernard Morrison. Lakini hiyo ndiyo kazi ya injinia ni mtu anayebuni au kuunda jambo au tukio.