MZEE WA KUTIBUA: Basena akitumika vizuri Simba itatoka hapo ilipo
Muktasari:
- Matokeo ya kuvuruga benchi la ufundi kwa kukurupuka bila ya kutokuwa na mipango maalum au kutabiri ya kesho imeigharimu Simba, kwani kila aliyekuja amekuja na yake na mwisho wa siku kila mmoja yuko pembeni akiangalia tu kwa vile kila kitu kimefika mahali kimegoma, inabidi kusarenda.
NI wazi kwamba mbio za nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania zimebaki kwa Azam, Yanga na Mbeya City.
Simba imetetereka na haina chake mwaka huu, inachofanya sasa ni kulinda heshima, tena ina mchezo mmoja tu wa kufanya hivyo dhidi ya Yanga Aprili 19.
Yapo mambo mengi yaliyoivuruga Simba, benchi la ufundi, uongozi na hata wachezaji wenyewe bila kuwasahau wanachama ambao walikuwa wakilea baadhi ya mambo kwa kuwaonea aibu viongozi wao au kutokujua madhara yake.
Matokeo ya kuvuruga benchi la ufundi kwa kukurupuka bila ya kutokuwa na mipango maalum au kutabiri ya kesho imeigharimu Simba, kwani kila aliyekuja amekuja na yake na mwisho wa siku kila mmoja yuko pembeni akiangalia tu kwa vile kila kitu kimefika mahali kimegoma, inabidi kusarenda.
Pamoja na hayo, Simba imeanza kufanya kitu cha msingi na kikipewa umuhimu kinaweza kuirudisha katika hadhi yake msimu ujao.
Simba ilimuajiri kocha wake wa zamani, Mosses Basena kama mkurugenzi wa ufundi tangu mwaka jana, aliletwa ili kulipa nguvu benchi la ufundi lakini mambo yakawa tofauti.
Waliomleta hawakutengeneza mfumo mzuri wa utendaji kazi baina yake na benchi la ufundi hususan lililokuwa chini ya makocha wazalendo, Abdallah Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’.
Makocha hao walishindwa kumtumia na hakukuwa na uhusiano mzuri baina yao ndio maana mwisho wa siku ripoti zilizowasilishwa kwa viongozi zilikuwa ni vituko vitupu na kujaa aibu, upande mmoja unawasilisha uhalisia na mwingine unapeleka vituko.
Mcroatia, Zdravko Logarusic anajua umuhimu wa mkurugenzi wa ufundi ndani ya klabu ndio maana ameanza kumtumia Basena kuitengeneza Simba mpya.
Kwa nyakati tofauti amekuwa akimtanguliza Basena kwenye viwanja kwa lengo la kuisoma timu pinzani kabla Simba hawajacheza nayo, jambo ambalo linafanyika hata katika timu kubwa za Ulaya.
Kama vile haitoshi, Basena ameanza kazi ya uskauti kutafuta wachezaji wapya wa Simba, ametumwa Uganda wiki chache zilizopita na hata katika timu za ligi kuu amefanya hivyo na Logarusic amekiri kuona orodha aliyopewa na mkurugenzi huyo.
Inachofanya Simba ni sahihi kama kikiheshimiwa.
Timu inapaswa kusajiliwa hivyo, matumizi sahihi ya mkurugenzi wa ufundi na kocha ndio kitu pekee kinachoweza kuifufua Simba.
Wapewe mwanya wafanye kazi yao watengeneze Simba kitaalam zaidi, Simba ilisajili kimazoea sana ndio maana imefika hapo ilipo.
Awali ilisajili wachezaji 30 kati yao 26 wote ni viungo, unategemea nini hapo?
Uwepo wa mkurugenzi wa ufundi hauisaidii timu uwanjani tu, bali mwenye nafasi hiyo anakuwa kiungo muhimu baina ya timu na uongozi, baina ya benchi la ufundi na wachezaji ili kuhakikisha kwamba mambo yote yanakwenda sawa na kuzingatia mawasiliano mazuri kwa chochote kinachotokea.
Umuhimu mwingine wa mkurugenzi wa ufundi, anaweza kuwa kocha wa muda pindi ikitokea kocha aliyepo ataacha kazi au kufukuzwa.
Hakuwezi kuonekana athari yoyote kwenye timu kwa vile aliyekuwepo alikuwa anafanya kazi kwa karibu zaidi na Mkurugenzi wa ufundi ambaye kitaaluma anapaswa kuwa na mafunzo ya juu ya ukocha.
Simba itanufaika na mfumo wake kama itakuwa siriazi.