Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MWASHINGA: Kiungo aliyewakataa Khalid Aucho, Kagoma

MWASHINGA Pict

Muktasari:

  • Kiungo huyu wa kazi amekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya timu hiyo kwa msimu mzima, akiwa na uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, kiungo mchezeshaji, nyuma ya mshambuliaji na beki wa kati na kuonyesha kiwango cha hali ya juu kila alipopewa nafasi.

KATIKA orodha ya wachezaji waliotamba kwenye kikosi cha Pamba Jiji msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Bara, jina la James Mwashinga haliwezi kukosekana.

Kiungo huyu wa kazi amekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya timu hiyo kwa msimu mzima, akiwa na uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, kiungo mchezeshaji, nyuma ya mshambuliaji na beki wa kati na kuonyesha kiwango cha hali ya juu kila alipopewa nafasi.

Akivaa jezi namba 23, Mwashinga amecheza mechi 26 kati ya 30 za ligi akizidiwa na Keneth Kunambi (27) na kipa, Yona Amosi aliyecheza mechi 28.

Katika mechi hizo, alifunga mabao mawili na kutoa asisti moja, lakini kubwa zaidi ni bao lake la ushindi dhidi ya Tabora United Aprili 5, 2025, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, lililomfanya atangazwe mchezaji bora wa mechi.

MWASH 01

Licha ya nafasi anayocheza kuwa ngumu kuonekana katika idadi ya mabao, kiwango alichoonyesha na uwezo wa kutumika sehemu tofauti uwanjani vilimfanya kuwa hazina kubwa kwa timu.

Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalum na kufunguka mambo mbalimbali kuhusu msimu wake, mipango ya baadaye, maisha nje ya uwanja na tathmini ya wenzake kwenye ligi.


MSIMU WA KUKUMBUKWA

Akielezea tathmini yake binafsi kwa msimu huu, James anasema umekuwa mzuri kwa sababu malengo ya klabu yametimia na kuiwezesha kubaki Ligi Kuu huku akiamini uwezo alioonyesha utaamua hatma yake kwenye dirisha la usajili.

“Msimu umekuwa mzuri kwa sababu karibu robo tatu ya malengo yangu niliyojiwekea nimeyatimiza, namshukuru Mungu tumemaliza salama mengine yote yataendelea baada ya msimu kuisha, nadhani baada ya hapo ndiyo nitajua malengo yangu mimi ni haya,” anasema Mwashinga.

MWASH 02

SIRI YA UHAKIKA WA NAMBA

Mwashinga anafichua siri ya kuaminika na kupata namba kwenye kikosi cha Pamba, hata mbele ya wachezaji wa kigeni ni kutokana na kuitekeleza kwa mafanikio mipango ya mwalimu na kufuata anachokuelekeza.

“Uhakika wa namba unatokana na kazi. Kila mwalimu anapenda mchezaji anayemfanyia kazi, mimi najituma na hiyo ndiyo siri ukifanya kazi kwa usahihi kila mtu anakupenda,” anasema kiungo huyo na kuongeza;

“Kwahiyo nahisi kutokana na kazi ninayofanya ndiyo maana nimekuwa kipaumbele cha kocha, kwahiyo siri ni kujituma tu kwa sababu kila mtu anataka mtu ambaye anafanya kazi kwa usahihi, na ukijituma kila mtu anakupenda.”

Akiangalia nyuma, James anakiri licha ya msimu huu kuwa mzuri, kipindi chake bora zaidi kilikuwa alipokuwa na Biashara United ikiwa Ligi Kuu Bara na kufanikiwa kumaliza nafasi ya nne msimu wa 2020/2021.

“Nilipata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa. Huo ndiyo ulikuwa wakati bora kwangu naamini bado nitapata tena hiyo nafasi,” anasema Mwashinga.

Ingawa hakupitia changamoto za kukatisha tamaa, anasema maisha ya mpira ni ya kupanda na kushuka.

“Kila njia ina changamoto zake, haikuwa rahisi lakini hazikuwa mbaya kiasi cha kunizuia kufika nilipo sasa. Sijawahi kushuka baada ya kupanda, nilipopanda ni mwelekeo mmoja hadi leo,” anasema kiungo huyo.

MWASH 03

SI AUCHO WALA KAGOMA

Wachezaji wengi nchini ukiwauliza viungo wao bora kwa sasa watawataja Khalid Aucho wa Yanga, Yusuph Kagoma wa Simba au Mudathir Yahya (Yanga), Fabrice Ngoma (Simba), Feisal Salum wa Azam FC ama Duke Abuya (Yanga), lakini hali ni tofauti kwa Mwashinga ambaye anataja wachezaji ambao wengi hawawafikirii kabisa.

Akiulizwa kuhusu viungo anaowakubali Ligi Kuu, Mwashinga hakusita kuwataja Azizi Andambwile (Yanga), Michael Samamba ‘Arteta’ (Pamba Jiji), Geofrey Manyasi (Kagera Sugar) na Paschal Mussa wa KMC.

“Wachezaji niliowataja kwangu hawana kasoro, wamekamilika nikicheza dhidi yao najua leo kuna kazi,” anasema Mwashinga kwa ujasiri mkubwa na kuongeza;

“Wachezaji wa Simba na Yanga wapo lakini kila mtu ana mitazamo yake, mimi siwezi kuwaona bora kwa macho yangu lakini wengine labda wao wanaona.”


KIKOSI BORA

James ametaja kikosi bora kwake chenye wachezaji kutoka timu mbalimbali, akiamini ndiyo wangeunda timu bora msimu huu huku akiwaacha nje makipa Moussa Camara (Simba) na Djigui Diarra (Yanga) pamoja na kiungo Yusuph Kagoma (Simba) na mshambuliaji, Clemet Mzize (Yanga).


Kipa: Yona Amosi, Mabeki: Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Dickson Job, Abdulrazack Hamza.


Viungo: James Mwashinga, Max Nzengeli, Mudathir Yahya.


Washambuliaji: Prince Dube, Jean Ahoua, Pacome Zouazoua.


Kocha: Fredy Felix  ‘Minziro’.

MWASH 04

MINZIRO KAMA MZAZI

Akizungumzia kocha wake, Mwashinga anatoa sifa kwa Fredy Felix ‘Minziro’ kwa jinsi alivyobadilisha mwenendo wa timu hiyo na kuisaidia kubaki Ligi Kuu.

“Minziro ni kocha mzuri sana ametutoa tulipokuwa pabaya hadi kutufikisha mahali salama. Anaishi kama mzazi nidhamu yake ni kubwa na hiyo ndiyo sababu watu wanamheshimu, uhusiano wake na wachezaji umetufanya tubadilike na kupambana zaidi,” amesema Mwashinga.

Mwashinga ametoa shukrani kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kuwaunga mkono katika nyakati nzuri na mbaya na kupambana kwa pamoja kufikia malengo ya klabu hiyo.

“Nawapongeza mashabiki wetu kwa kuwa na sisi wakati wote tulipitia kipindi kigumu sana lakini hawakutuacha, mwisho wa msimu wametuonyesha kuwa wanaipenda timu yao, na hiyo ndiyo ilitupa nguvu,” anasema Mwashinga.


ISINGEKUWA SOKA

Kwa asili, James anatokea Kyela, Mbeya, na anasema kama si mpira, basi angekuwa mkulima wa mpunga.

“Ningekuwa mkulima mzuri wa mchele, napenda kupumzika nyumbani lakini kama shughuli za shamba zipo nipo kule kwa sababu maisha ya kesho ni muhimu unaweza kuacha mpira ukaingia kwenye kilimo,” anasema kiungo huyo na kuongeza;

“Kwa sasa nina shughuli zangu za kilimo cha mpunga huko Kyela (Mbeya).”

MWASH 05

TAIFA STARS

Mpaka sasa, Mwashinga hajawahi kuitwa kwenye timu ya taifa, lakini bado ana matumaini ya kulitumikia taifa lake kwa miaka ijayo.

“Hiyo ni ndoto ya kila mchezaji, muda ukifika nitaitwa lakini kwa sasa nawapa heshima waliopo kwa sababu wanaliwakilisha taifa wakati wangu ukifika nitakuwa tayari kuipambania nchi yangu,” anasema Mwashinga.


MSIKIE MDAU

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William kiungo huyo ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa na msimu mzuri mwaka 2024/2025.

“James ni mmoja wa wachezaji bora kwenye kikosi chetu msimu huu wale tatu bora jina lake lipo. Ukibakiza wawili kwenye orodha basi ni yeye na Yona Amosi, lakini James ni muhimu zaidi kwenye timu,”  anasema William na kuongeza;

“James ametumika kama kiungo mkabaji, kiungo wa juu, namba 8, hata mshambuliaji wa pili. Alicheza beki wa kati mechi moja na alifanya vizuri kwahiyo ni mchezaji wa aina yake.”

Anasema upambanaji wa mchezaji huyo ni wa hali ya juu kwani akiwepo uwanjani unajua mwanaume yupo, na utendaji na utekelezaji wa majukumu uwanjani ni mkubwa kuliko mchezaji mwingine yeyote, hivyo, anakiri kuwa Mwashinga alikuwa na msimu bora.

“Kiufundi James ameleta vitu vingi sana vya tofauti ametumika kwenye maeneo mbalimbali, ni mchezaji ambaye kiufundi ametusaidia kila ambapo mwalimu akitengeneza timu yake jina la James lazima ulione kiwanjani,”  anasema William.