Mwamnyeto anavyotembelea njia ya Terry

Muktasari:
- Hali hiyo imekuwa ya kawaida kwa wachezaji wengi wakubwa duniani, na pia inajidhihirisha kwa wachezaji wa ndani kama vile nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto.
KATIKA soka mara nyingi wachezaji hupitia mabadiliko kwenye majukumu yao hasa wanapokutana na ushindani mkubwa wa namba.
Hali hiyo imekuwa ya kawaida kwa wachezaji wengi wakubwa duniani, na pia inajidhihirisha kwa wachezaji wa ndani kama vile nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto.
Mwamnyeto (29), ambaye alikuwa akicheza mara kwa mara kwenye nafasi ya beki wa kati mwanzoni mwa maisha yake ya soka Jangwani ambako alitua Juni Mosi 2028, kwa sasa anapambana na ushindani mkubwa kutoka kwa wachezaji Ibrahim Hamad, 27, na Dickson Job, 24, ambao ndio wamekuwa sehemu ya kikosi kinachoaza Yanga kwa muda mrefu.

Hali hiyo inafanana na ile aliyokuwa akikutana nayo John Terry, mchezaji wa zamani wa Chelsea ambaye alikumbana na ushindani kutoka kwa wachezaji kama David Luiz, Andreas Christensen na Gary Cahill akiwa beki wa kati. Hata hivyo, licha ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, Terry alibaki kuwa kiongozi muhimu na alipewa heshima kama nahodha kwa kubeba ubingwa wa mwisho wa timu hiyo kwenye Ligi Kuu England msimu wa 2016/17, jambo ambalo pia kalifanya Mwamnyeto pale Yanga chini ya makocha watatu tofauti.
Terry alikuwa mchezaji muhimu Chelsea kwa zaidi ya miaka 17, akiwa kiongozi na beki wa timu hiyo. Hata hivyo, katika misimu ya mwisho ya safari yake kuanzia 2014/15, alikutana na ushindani kutoka kwa wachezaji vijana na wenye uzoefu kama Luiz, Christensen na Cahill, nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza ilianza kuwa ngumu kwake.
Terry alijua majukumu yake hayakuishia uwanjani pekee. Ingawa alikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, alijitolea kwa namna nyingine ili kusaidia timu kufanya vizuri.
Aliendelea kuwa kiongozi muhimu, akiungana na wachezaji vijana katika vyumba vya kubadilishia nguo na kuhakikisha kuwa hali ya uongozi inabaki imara. Muda mwingi alitumia kutoa ushauri kwa wachezaji chipukizi na kuwa mfano wa uongozi na kujituma wakiwa kwenye changamoto.

Katika kikosi cha Yanga, Mwamnyeto ambaye ametumika kwa dakika 907 katika michezo 15 ya ligi, anapitia hali inayofanana na ile ya Terry. Kama Terry alivyokutana na ushindani kutoka kwa kina Luiz na Cahill, Mwamnyeto pia anakutana na ushindani kutoka Ibrahim Hamad na Dickson Job ambao wamekuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Yanga kwa muda mrefu. Hata hivyo, Mwamnyeto anabaki kuwa kiongozi ndani ya timu, licha ya kuwa nafasi yake ya kucheza mara kwa mara ni ndogo.
MSIKIE KOCHA
Akizungumzia nafasi ya nahodha huyo kwenye kikosi chake, kocha Miloud Hamdi anasema Mwamnyeto atabaki kuwa nahodha na kucheza mara kwa mara ni suala la nafasi, lakini umakini na uwezo wa kuongoza timu ni muhimu.
“Ana ufanisi mkubwa na kila wakati tunahitaji wachezaji kama yeye ambao wanajua kuwa uongozi siyo tu kucheza, bali pia kuhamasisha wengine na kuhakikisha timu inakuwa na nguvu hata inapokutana na changamoto,” anasema kocha huyo.

Mwamnyeto ameonyesha kuwa uongozi hautegemei kucheza kikosi cha kwanza, bali ni ule mchango unaotoka nje ya uwanja. Anajua kuwa nafasi ya kucheza inategemea mambo mengi, lakini haachi kufanya kazi ya kuwa kiongozi wa timu. Hiyo inadhihirisha kuwa hata wachezaji waliopo benchi wana mchango mkubwa kwa timu, hasa wanapokuwa na roho ya kujitolea na kuhamasisha wachezaji wenzao.
MIFANO MINGINE
Katika soka la kimataifa, kuna mifano mingine ya wachezaji ambao walikubali mabadiliko ya nafasi na kuwa viongozi, hata pale walipoachwa benchi. Mmoja wa wachezaji hao ni Ryan Giggs ambaye alicheza kwa muda mrefu katika timu ya Manchester United. Giggs alikuwa na umri mkubwa wakati wa mwisho wa safari yake, lakini aliendelea kuwa kiongozi muhimu katika timu. Hata alipoanza kucheza mara chache, aliendelea kuwa msaada mkubwa kwa wachezaji vijana na alikuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio ya timu. Giggs alijua kuwa uongozi wake hauchaguliwi kwa nafasi ya kucheza, bali na jinsi alivyokuwa msaada kwa timu hata alipokuwa benchi.

Mfano mwingine ni wa Francesco Totti wa Roma, ambaye alidumu kwenye klabu hiyo kwa miongo mingi na kuna wakati alikuwa na nafasi ndogo ya kucheza kwenye misimu ya mwisho ya maisha yake ya soka, lakini alibaki kuwa mfano wa uongozi kwa vijana na alijivunia kuwa sehemu muhimu ya timu.