Mwambusi aliyebeba hatma ya Wagosi

Muktasari:
- Lakini kabla ligi hiyo haijasimamishwa, Coastal Union iliwasapraizi mashabiki wa Wagosi wa Kaya a.k.a Wanamangushi kwa kumtangaza kocha maarufu nchini aliyewahi kuzinoa timu mbalimbali ikiwamo Yanga, Mbeya City na Azam FC na Ihefu, Juma Mwambusi.
LIGI Kuu Bara kwa sasa imesimama kwa muda wa kama wiki mbili kupisha kalenda ya Fifa kwa mechi za kimataifa za timu za taifa, huku zikiwa zimeshachezwa jumla ya mechi 81 na kufungwa mabao 164.
Lakini kabla ligi hiyo haijasimamishwa, Coastal Union iliwasapraizi mashabiki wa Wagosi wa Kaya a.k.a Wanamangushi kwa kumtangaza kocha maarufu nchini aliyewahi kuzinoa timu mbalimbali ikiwamo Yanga, Mbeya City na Azam FC na Ihefu, Juma Mwambusi.
Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara msimu wa 1988 walifanya uamuzi huo baada ya kushuhudia jahazi la timu hiyo iliyomaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita na kuiwakilisha nchi kimataifa kwa mara nyingine tangu ilipoishiriki mwaka 1989, likielekea kuzama na kumuondoa kocha Mkenya, David Ouma.

Tangu kutua kwa kocha huyo wa zamani wa Moro United, kuna mabadiliko yaliyoanza kuonekana na kuwapa matumaini makubwa Wanamangushi na kuamini kwa sasa Coastal ipo katika mikono salama.
MKALI WAO
Kocha Mwambusi ana historia na rekodi tamu akiwa mzoefu wa soka la Tanzania na kufanya makubwa, ikiwamo kuipandisha Ligi Kuu, Mbeya City 2013-14 na kutikisa ikimaliza ligi katika nafasi ya tatu ikichuana na Yanga na Azam iliyobeba ubingwa, huku ikiizidi ujanja Simba iliyomaliza nyuma yake ikiwa ya nne.
Msimu wa pili wa Ligi Kuu, Mbeya City ilimaliza ndani ya Nne Bora ikitanguliwa na Yanga, Azam na Simba, lakini akiifanya timu hiyo kuwa tishio kwa soka la nguvu na kuvikimbiza vigogo hivyo kwa muda wa dakika 90 uwanjani, huku timu ikiundwa na wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kiufundi wa kocha huyo.

Pia amefanya makubwa akiwa na Yanga kama kocha msaidizi na kutwaa nao mataji na hii inampa hazina kubwa ya uzoefu wa kufundisha timu zenye viwango tofauti na zenye malengo mbalimbali katika ligi. Katika msimu akiwa na Yanga, Mwambusi alihusika katika kuandaa timu yenye ushindani mkubwa, huku akifanikiwa kuwajenga wachezaji chipukizi kuwa nyota wanaong’ara kwenye ligi.
Mbali na kazi yake kama kocha, Mwambusi ni mshauri na mlezi wa wachezaji wengi chipukizi, jambo linalomfanya awe kipenzi cha vijana wenye ndoto za kucheza soka la ushindani.
Uwezo wake wa kuelewa soka la ndani na jinsi anavyowaongoza wachezaji kukabiliana na changamoto za ligi umemfanya awe miongoni mwa makocha wanaoheshimika sana katika soka la Tanzania.

CHANGAMOTO NA FURSA
Coastal Union ni moja ya timu kongwe nchini, lakini miaka ya hivi karibuni imekumbwa na changamoto kadhaa, ikiwamo hali ya kifedha na ushindani mkubwa kwenye ligi.
Timu hiyo inahitaji ushawishi wa kocha mwenye mbinu na mikakati bora ili kuweza kuhimili presha ya ligi na kupata matokeo bora.
Kuwa na Mwambusi kama kocha ni hatua muhimu kwa Coastal. Kwanza, uzoefu wake unaweza kuwa msaada mkubwa katika kujenga timu yenye nidhamu na umahiri uwanjani. Pia, ni kocha anayejua jinsi ya kushughulika na changamoto za timu ambazo zinakutana na changamoto za kifedha na miundombinu kama Coastal Union. Kwa mwongozo wake, Mwambusi anaweza kuwaunganisha wachezaji kwenye falsafa ya timu, ili wawe na nia moja ya kufanikisha malengo.

KUIBORESHA COASTAL
Moja ya mambo yanayotarajiwa kutoka kwa Mwambusi ni kujenga mfumo wa uchezaji unaozingatia nidhamu na umakini katika kila nafasi. Akiwa na ujuzi katika kuimarisha safu ya ulinzi, Mwambusi anatarajiwa kujenga timu inayozingatia zaidi mbinu za kujilinda wakati wa mashambulizi na kushambulia kwa haraka.
Kwa Coastal Union, ambayo mara nyingi imekuwa ikipoteza mechi kwa makosa ya ulinzi, Mwambusi anaweza kutengeneza safu imara ya mabeki ambayo itapunguza idadi ya mabao wanayofungwa.
Pia, kutokana na historia yake ya kuwapa fursa vijana, Mwambusi anaweza kusaidia timu hiyo kuwajenga wachezaji wenye vipaji kuwa na ufanisi zaidi, na hivyo kusaidia katika kuongeza ushindani uwanjani.

UJIO WAKE
Ujio wa Mwambusi umeibua matumaini mapya kwa mashabiki wa Coastal Union. Wanategemea kuona timu yao ikionyesha mabadiliko katika kiwango na matokeo. Mashabiki wanaamini kuwa mwalimu huyu anaweza kuibadilisha Coastal Union na kuwa timu yenye kujiamini zaidi, huku ikipambana na timu nyingine kubwa kama Yanga na Simba kwa ushindani mkubwa.
Kwa wadau wa soka Tanga, ujio wa Mwambusi ni fursa kwa mkoa kuwa na timu imara itakayowakilisha vyema kwenye ligi na kuleta heshima kwa jamii ya wapenda soka Tanga.
Ushirikiano kati ya uongozi wa Coastal Union na Mwambusi utakuwa muhimu katika kufanikisha malengo haya, na kama mashabiki na viongozi watajenga mazingira mazuri ya ushirikiano, Coastal Union inaweza kushuhudia mafanikio makubwa msimu huu.
Katika mechi tatu tangu alipotangazwa na Coastal kuwa kocha mkuu, Mwambusi amepoteza mchezo dhidi ya Yanga kwa kulala 1-0, lakini akashinda kwa idadi kama hiyo mbele ya Kagera Sugar na kutoka suluhu na waliokuwa vinara wa ligi hiyo, Singida Black Stars kabla ya kushushwa na Simba.
Mwambusi anasema: “Tutafanya kazi kwa bidii kuhakikisha tunajenga kikosi chenye ushindani na kinacholeta furaha kwa mashabiki.”