Mussa anavyopiga pesa nje ya soka

Muktasari:
- Mussa alianza kuwa midomoni mwa wapenzi wa soka nchini baada ya kusajiliwa na Simba 2023 alipoonekana katika michuano ya Kombe la Mapinduzi akiwa na Malindi ya Zanzibar.
KAMA ukibahatika kupiga stori za hapa na pale na mshambuliaji wa Mashujaa FC, Mohamed Mussa utagundua mwonekano wake ni tofauti na maisha yake nje ya uwanja anakotambulika kuwa na shughuli nyingine za kusaka kipato.
Mussa alianza kuwa midomoni mwa wapenzi wa soka nchini baada ya kusajiliwa na Simba 2023 alipoonekana katika michuano ya Kombe la Mapinduzi akiwa na Malindi ya Zanzibar.
Mchezaji huyo anafichua kwamba Simba ilianza kuhitaji huduma yake muda mrefu akiwa na Mbeya City na baada ya kuumia mpango huo ukasitishwa kabla ya dili hilo kutiki 2023.
Mshambuliaji huyo kupitia gazeti la Mwanaspoti amejibu kitendawili cha wengi waliokuwa wakijiuliza kipi kilimpata hadi akashindwa kufanya vizuri Simba na baada ya kuondoka hakuonekana uwanjani takriban mwaka mzima.
"Mwonekano wa mwili wangu wengi wao wananichukulia poa ila mimi ni mtu ambaye natumia muda wangu mwingi kufanya shughuli za kuingiza pesa. Ndiyo maana huwezi ukaniona hovyo katika mitandao ya kijamii kuposti posti picha," anasema.
"Kijana wa kiume lazima niwe mkakamavu nje na kucheza Bara nimecheza Oman daraja la pili kilichonirudisha ni kipindi kile cha Covid 19."

MAISHA YAKE SIMBA
Japokuwa alicheza mechi chache baadhi akizitaja dhidi ya Al Hilal ya Sudan mechi ya CAF, Geita Gold (Ligi Kuu) na Coastal Union (FA), na alifunga bao aliloshangilia hadi akavua jezi, hakuambulia patupu bali alitoka na somo la namna gani mchezaji mkubwa anapaswa kuwa.
"Kwanza wengi walishangaa kwa nini nilishangilia sana hadi nikavua jezi. Kuna wakati mchezaji anaweza akapitia ugumu, nakumbuka nilikuwa nacheza mechi za kirafiki tu kuna wakati nilikuwa naona za ligi naweza nikasaidia ila nilikuwa sipati nafasi. Baada ya kucheza na Coastal nikafunga ndiyo maana nilishangilia sana," anasema.
"Ingawa Simba sikutimiza ndoto zangu za kucheza kwa kiwango kikubwa, lakini nilijifunza vitu vingi kutoka kwa wachezaji wenye uzoefu na waliofanya makubwa, makocha na viongozi, ambavyo hadi sasa vinanisaidia kuendelea na maisha yangu mengine."
Na alipoulizwa na Mwanaspoti kipi kilimfanya ashindwe kuonyesha kiwango? Anajibu,"nilipitia changamoto ngumu ya kumuuguza baba yangu, vitu ambavyo vilifanya nishindwe kufanya mazoezi kama inavyotakiwa. Baada ya kufariki nikatoka mchezoni kabisa.
"Baba alikuwa kila kitu katika utafutaji wangu. Nakumbuka wakati nasajiliwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again ndiye aliyezungumza na mzee hadi nikajiunga na timu hiyo.
"Ilinichukua mwaka mmoja akili yangu kutulia maana nje ya mpira nilikuwa nafanya biashara na baba ambazo zilikuwa zinatunza familia.
"Changamoto hizo viongozi wa Simba walikuwa wanazijua ndio maana walinipeleka kwa mkopo Kagera Sugar, ila nilienda nikiwa bado sipo sawa, nikaa mwezi mmoja nikaondoka, nilikuwa nikifikilia familia ambayo nilikuwa nahusika kila sekta nikawa naona nachoka baada ya mzee kufariki."
Anasema jambo analoshukuru alimalizana kwa amani na viongozi wa Simba na anawasiliana na baadhi yao, wachezaji na makocha, hivyo kupitia Mwanaspoti anaamini mashabiki wa wekundu wa Msimbazi waliokuwa wanadhani kapotezwa na starehe, basi watakuwa wanaelewa changamoto ambazo zilikuwa zinamuumiza.
"Kuna wakati ukipitia magumu unaamua kunyamaza. Haikuwa mara yangu ya kwanza kucheza Bara, kwani nimechezea Mbeya City nikiwa chini ya kocha Juma Mwambusi aliyenisajili kutoka Zanzibar baada ya hapo nikaenda Gwambina, hivyo sikuona kigeni cha kunizuzua hadi kuacha majukumu yangu," anasema Mussa ambaye mechi yake ya kwanza msimu huu kaifunga Kagera Sugar iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

ANAPIGA MISHE HIZI
Mchezaji huyo hachagui biashara ilimradi isiwe haramu kwani anananua mawe maarufu Tangastone mkoani na kwenda kuyauza Zanzibar ambayo yanatumika kujengea nyumba zinazopendwa na watalii.
Pia anauza vitu mbalimbali vya majumbani.
"Mbali na hiyo nafanya biashara mbalimbali ambazo ni ndogondogo siyo lazima nizitaje zote. Ila mimi ni mpambanaji tofauti kabisa na watu wanavyonichukulia," anasema.
"Nilianza kufundishwa na baba yangu tangu nikiwa mdogo licha ya mimi (kuwa) ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya 10, hivyo ndiye nahusika kwa kila kuitunza familia."
Ukiachana na hilo Mussa ni mwalimu wa madrasa, hivyo anapokuwa mapumziko anafanya mambo ya dini zaidi.
"Nimesomea mambo ya dini nafundisha madrasa. Ni kitu ambacho nakipenda zaidi ndio maana huwezi kunikuta sana vijiweni kama ilivyo kwa vijana wengine."

FAMILIA YA DINI
Mussa anasema katika familia yao ni kawaida kutenga siku moja kwa wiki kuhakikisha wanakwenda kusaidia vituo vya wahitaji, jambo ambalo tangu anakua anaona linasimamiwa na wazazi.
"Familia yetu ni ya dini sana kutoa kwa wahitaji ni kitu tunachokifanya tangu tukiwa wadogo. Ukiachana na hilo mama yangu anakwenda kupalilia makaburi ya watu mbalimbali na baada ya mzee kufariki anafanya zaidi.
"Imani ya Kiislamu inatuagiza unapotoa mkono wa kushoto usishuhudie maana yake ni kuwastili wenzetu wahitaji. Ndio maana huwezi kuona naposti popote na sipendi kushinda mitandaoni kwani sijafunzwa hivyo na wazazi wangu nimefundishwa kufanya kazi kwa bidii."
Anasema kitu ghari anachoweza kununua kwa gharama yoyote katika maisha yake ni mswala na msahafu ambavyo anakuwa anagawa katika misikiti kwa ajili ya watu kuswalia.
"Ndoto yangu ni kuchimba kisima katika msikiti mmojawapo Zanzibar ili watu wakienda kuswali maji yapatikane bila shida. Naomba sana Mwenyezi Mungu nitimize hilo," anasema.

SOKA LIMEMPA HATUA
Japokuwa vitu vyake vingi vya kimaendeleo kavifanya na pesa nje ya soka, mchezaji huyo anasema hawezi kuficha ukweli kwamba kupitia kucheza anaweza kufanya mambo kwa urahisi na kuheshimika na watu.
"Sio muumini wa kuweka mambo yangu wazi kuna vitu nimefanya kutokana na mpira wa miguu. Vipo vingine ni kutokana na shughuli mbalimbali ninazozifanya. Nafanya biashara tofauti ilimradi zisiwe za kumkosea Mungu," anasema.
FEI TOTO, BACCA
Anasema kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' na beki wa Yanga, Ibrahim Bacca ukiachana na ubora wao uwanjani ni watu wanaopenda utani na kucheka na kila mtu.
"Nakumbuka tukiwa wadogo nilikuwa nahodha katika timu ya Mapembeani ambako nilicheza pamoja na Bacca alionyesha kipaji kikubwa pia tulicheza wote Malindi, naona jinsi anavyopambana kuisaidia Yanga na Stars namkubali ni mchezaji mzuri,' anasema.
"Zanzibar ni tofauti na Bara kuna programu ama miradi ya kukuza soka la vijana. Kuna daraja tofauti lipo la chini na kati, hivyo nikiwa Mapembeani lilikuwa daraja la kati tunafundishwa misingi ya soka toka tukiwa wadogo ndio maana unaona wachezaji wanaotoka upande huo wana vipaji vikubwa."