MTU WA MPIRA: Yanga imepiga hatua moja, bado 100 mbele

NIMEONA sherehe kubwa sana kwa Yanga kufuzu hatua ya makundi. Ni sherehe kubwa mno mithili ya ndoa ya mwanaume aliyegoma kuwa hata na mchumba kwa muda mrefu.

Ni sherehe kwa Wanayanga wakubwa na wadogo. Nilitazama picha za video namna ambavyo Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na viongozi wenzake walivyoshangilia pale Tunisia.

Halafu nikatazama video ya shangwe na wachezaji wao. Nikaburudika zaidi kumuona Ofisa Habari wao kijana wangu, Ally Kamwe akiwa juu ya ngamia pale Tunisia baada ya ushindi.

Kusema kweli watu wa Yanga wamefurahi sana. Hawakuwa na matumaini makubwa ya kuwatoa Waarabu wa Tunisia pale kwao. Ni jambo gumu kuliko hata ugumu wenyewe, lakini Yanga wameweza.

Wanastahili pongezi kubwa. Japokuwa Club Africain hakuwa mpinzani wa kutisha sana, lakini suluhu katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam ilipunguza matumaini ya Yanga kusonga mbele.

Katika historia hii siyo mara ya kwanza kwa Yanga kufuzu hatua ya makundi ya michuano mikubwa ya CAF. Walifuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 1998. Tena wakati ule ni timu nane tu zilikuwa zinaingia hatua ya makundi, lakini waliweza.

Wakafuzu tena hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho 2016 na 2018. Hii ni mara ya tatu wanafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini furaha imekuwa kubwa sana awamu hii. Unajua kwanini? Ni kwa sababu wamefuzu katika mazingira magumu.

Pamoja na kufuzu hatua ya makundi, lazima tuwaambie ukweli Yanga kuwa wana mtihani mkubwa zaidi mbele. Kufuzu hatua ya makundi ni jambo moja, lakini kucheza mechi za makundi ni jambo gumu zaidi.

Hapa Yanga inakwenda kukutana na timu 15 nyingine zilizofanya vyema zaidi katika michuano. Haijalishi unapangwa na nani, lakini hatua ya makundi haijawahi kuwa nyepesi.

Mwaka 2016 wakati wamefuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza, walipangwa na MO Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya DR Congo na Medeama ya Ghana. Ikaonekana kama siyo kundi gumu sana.

Mazembe aliyekwenda kutwaa ubingwa katika mwaka huo ndio alionekana kuwa tishio. Lakini nini kilitokea? Yanga ilimaliza mkiani mwa kundi. Tena hii ilikuwa Yanga ya Yusuf Manji. Tajiri asiyekuwa na shoo ndogo katika kutoa fedha. Hapa ni dhahiri ugumu ulionekana.

Walipofuzu kwa mara ya pili mwaka 2018, hawakupangwa dhidi ya timu ngumu sana. Walikuwa na USM Alger ya Algeria, Rayon Sports ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya. Nini kilitokea?

Yanga ilimaliza tena mkiani mwa kundi. Licha ya awamu hii kuonekana kama Rayon Sports na Gor Mahia siyo wapinzani wa kumtisha sana Yanga, lakini bado walifanya vizuri zaidi yake. Ilikuwa ni aibu. Ni kama vile tu ilivyotokea 1998. Yanga ilimaliza tena mkiani mwa kundi lake. Haikuwa na jipya sana. Tena ilikumbana na vipigo vya aibu ikiwemo kile cha mabao 6-0 kutoka kwa Raja Casablanca ya Morocco. Ilikuwa ni aibu zaidi.

Funzo la hatua za makundi walizoingia awali linapaswa kuwaingia vizuri. Ubaya ni kwamba Yanga katika mashindano haya imeshindwa kuwa na ngome yake. Ikiwa nyumbani ni kama vile ipo ugenini, na ikiwa ugenini ni kama vile ipo ugenini pia. Hatishi sana.

Ni tofauti na Simba ambao wanafahamu namna ya kuzicheza vyema mechi zao. Mwaka 2003 Simba walipofuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi lao wakiwa na alama saba.

Wakati ule Enyimba ndio ilikuwa timu tishio zaidi na ndio waliotwaa ubingwa mwaka huo. Lakini pamoja na kuwa tishio haikuweza kupata ushindi dhidi ya Simba hapa Dar es Salaam. Simba ilikuwa imara sana ikiwa nyumbani.

Ndivyo ambavyo Simba walifanya katika mechi za msimu wa 2018/19 ambapo walishinda mechi zote za nyumbani na kufuzu hatua ya robo fainali. Simba licha ya kuwa na vigogo kama Al Ahly na AS Vita lakini wote kwa Mkapa walitepeta na kuacha alama tatu.

Vivyo hivyo kwa miaka iliyofuatia. Simba kwa Mkapa hafungwi wala kupata sare kirahisi. Ni ngome yake. Vipi ngome ya Yanga iko wapi? Hakuna, na ndiyo sababu kila mwaka wanamaliza mkiani mwa kundi.

Pamoja sherehe za sasa, Yanga inapaswa kutafuta namna njema ya kucheza mechi zake za nyumbani. Tunatamani kuona wapinzani wakipata tabu kubwa pindi wanapokuja kwa Mkapa. Vinginevyo Wananchi wataburuza tena mkia awamu hii.