MTU WA MPIRA: Wala mihogo ndo wenye Yanga yao

GHAFLA sana nimemkumbuka marehemu Abbas Gulamali. Huyu alikuwa Mwenyekiti wa zamani wa Yanga. Vijana wengi wa siku hizi hawamfahamu kwa sababu hazungumzwi sana.

Gulamali alikuwa anaipenda Yanga kuliko hata nafsi yake. Angeweza kufanya chochote kwa ajili ya Yanga. Na hata utajiri wake uliyumba kwa kiasi kikubwa wakati huo kwa sababu ya Yanga. Alitumia fedha nyingi sana kwa ajili ya Yanga na wala hakuwahi kuona shida.

Watu kadhaa wamewahi kunukuliwa wakizungumza kuhusu Gulamali. Lakini kauli ambayo huwa naikumbuka mara nyingi ni ile ya Azim Dewji. Huyu alikuwa mfadhili wa Simba enzi hizo Gulamali akiwa Yanga.

Azim amewahi kukiri mara kadhaa kuwa Gulamali ndiye aliyeharibu mpira wa Tanzania. Kwanini? Subiri nitakueleza.

Wakati Azim akiwa anatoa fedha zake kuipa sapoti Simba, bado alipata wakati mgumu sana kushindana na Yanga ya Gulamali. Kila akitoa, Gulamali angetoa zaidi.

Gulamali ndiye aliyeanzisha utaratibu wa kuwalipa fedha nyingi wachezaji. Kabla ya hapo wachezaji walicheza kwasababu wanaipenda timu fulani, lakini wakati wa Gulamali mambo yakawa tofauti. Angeweza kumpa fedha mchezaji mahiri wa Simba ahamie Yanga.

Huyu ndiye marehemu Gulamali. Ndio sababu hadi leo Azim anadai kuwa Gulamali ndiye aliharibu mpira wetu kwa kuupeleka kwenye fedha. Ila kwa uhalisia hakuharibu, aliupeleka tu ulipokuwa unakwenda. Katika ushindani wa kweli.

Achana kwanza na huyu Gulamali. Njoo hapa tumzungumze huyu tajiri karne ya vijana hawa wadogo pale Yanga. Tuzungumze kidogo kuhusu Yusuf Manji. Huwa napenda kumuita kichaa wa soka.

Manji alikuwa chizi kweli linapokuja suala la Yanga. Huyu ndiye binadamu pekee katika zama hizi ambaye amewahi kulipia mashabiki wote viingilio waingie bure uwanjani kutazama mechi za Yanga. Yaani alilipa viingilio vya mashabiki wote, sio mmoja wala wawili.

Nakumbuka aliwahi kufanya hivyo wakati Yanga ikicheza na Moro United kwenye fainali ya Kombe la Tusker enzi hizo. Akalipa kiingilio cha mashabiki wote wa Yanga pale CCM Kirumba Mwanza.

Wengi wanakumbuka zaidi alivyolipa kiingilio mashabiki wote waingie kuitazama Yanga dhidi ya TP Mazembe kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016. Huyu ndiye Manji. Akiamua kufanya jambo lake huwa hafikirii mara mbili.

Baada ya Gulamali kuufanya mpira kuwa wa kulipwa, Manji ndiye aliyepandisha zaidi thamani za wachezaji nchini. Enzi za Manji, mchezaji yeyote bora nchini angeweza kucheza Yanga. Ni katika wakati wake alimchukua Juma Kaseja katika ubora wake pale Simba akampeleka Yanga.

Nani aliwahi kuwaza kama Kaseja yule angeweza kwenda Yanga? Lakini Manji alifanya kuwa jambo jepesi sana. Angeweza kununua mchezaji yoyote mahiri ndani na nje ya nchi. Alikuwa ni kichaa kweli kweli katika soka.

Ni katika enzi za Manji tulishuhudia mchezaji wa kwanza wa kigeni kulipwa mshahara wa dola 1000 kwa mwezi. Ni katika enzi zake tulishuhudia wachezaji wakisajiliwa kwa dola 50,000 na zaidi. Haikuwa hivyo hapo nyuma.

Timu nyingi nchini zilinunua wachezaji wa dola 20,000 ama pungufu. Lakini Manji angeweza kununua mchezaji hata dola 100,0000. Hakujali sana katika enzi zake. Alitumia pesa kwa ajili ya Yanga na kila mtu aliona hilo. Huyu ni tajiri wa soka kweli kweli.

Lakini pamoja na matumizi makubwa ya fedha waliyofanya Gulamali pamoja na Manji, bado waliishi kwa kuwaheshimu sana mashabiki wa Yanga. Wanafahamu thamani ya hawa mashabiki na wanachama wa timu yao. Ndio maana nimekwambia hapo awali, Manji angeweza kufanya yote kwaajili ya mechi na bado akalipia watu waingie bure.

Kuna jambo la kujifunza hapa. Pamoja na fedha alizokuwa anatoa Manji, bado walikuwepo wazee wengi wa Yanga ambao walimsumbua. Waliona kama ananufaika zaidi na Yanga. Hawa Wazee wangeweza kusimama na kumtukana Manji.

Unadhani Manji alijali? Hapana. Anafahamu hawa ndio wenye timu yao. Hawa ndiyo wanaokupa thamana ya kuongoza timu ama la. Manji alitambua hilo na ndiyo maana aliishi nao vizuri. Alitoa fedha na bado wakamsema vibaya, lakini hakuwajibu akasonga mbele.

Hiki ndicho anachopaswa kufahamu Rais wa sasa wa Yanga, Injinia Hersi Saidi. Hawa watu aliosema ‘wameshiba mihogo’ ndio wenye Yanga yao. Hawa ndio wanaumia zaidi timu ikifungwa. Hawa ndio wamerithi hii timu kwa vizazi na vizazi. Ndio maana Yanga ipo salama mpaka leo.

Hawa watu ‘walioshiba mihogo’ ndio waliomchagua kuongoza timu. Ni watu wenye maana kubwa sana hapa Yanga. Hapaswi kuwachukulia poa. Ni kama kina Gulamali na Manji walivyofanya. Unatoa pesa zako lakini usisahau kuwa Yanga ina wenyewe.

Yanga ilikuwepo kabla ya Hersi na itaendelea kuwepo baada yake. Asidhani kama yeye na ‘Bosi wake’ wanafanya mambo makubwa sana pale Yanga. Mengi waliyofanya yalishafanywa na wengine zamani. Nimewazungumza tu hao wawili, ila wapo wengi enzi na enzi. Lakini bado Yanga itabaki kuwa ya wenyewe.

Hii ndiyo sababu hata kwenye mfumo wa uwekezaji, bado upande wa Wanachama unakuwa na asilimia 51%. Unajua kwanini? Ni kwasababu hao ndio walioshiba mihogo na ndio wenye Yanga yao.