MTU WA MPIRA: Taifa Stars bila Tshabalala na Kapombe ni kichekesho kingine

KUNA nyakati vitu vinatokea na kushtua sana. Ni kama hiki kilichotokea kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ majuzi. Ni kichekesho kwelikweli.

Taifa Stars inakwenda kwenye mechi mbili muhimu za kufuzu fainali za Afrika(AFCON) dhidi ya Uganda. Ni mechi muhimu sana kuliko hata umuhimu wenyewe.

Kumbuka Stars ina alama moja tu kwenye kundi mpaka sasa. Ilipata sare ya goli 1-1 ugenini dhidi ya Niger. Ikapoteza 2-0 kwa Algeria hapa nyumbani.

Hivyo ni muhimu kwa Stars kushinda mechi hizi mbili zinazofuata dhidi ya Uganda. Vinginevyo safari ya kufuzu AFCON mwakani itakuwa imeishia hapa.

Ni katika nyakati hizi unahitaji timu imara zaidi uwanjani. Ila kichekesho ni pale ambapo tunakwenda katika mechi hizi muhimu na wachezaji wa majaribio.

Kila mmoja anafahamu nchi hii kwa sasa hakuna mabeki bora wa pembeni kuliko Shomary Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Hawa wanaanza kila siku pale Simba. Wanacheza vyema kwenye ligi na mashindano ya kimataifa. Kwanini wameachwa? Inashtua sana. Ni kweli kuna vijana wengine wanakuja vizuri lakini bado hawajafikia kwenye viwango vya hawa nyota wawili wa Simba. Kila mmoja anaona hilo. Benchi la Taifa Stars limeona nini cha tofauti? Wanajua wenyewe.

Tunacheza kamari katika mechi muhimu. Tunakwenda kwenye mechi hizi na David Luhende, Datius Peter, Yahya Mbegu na Kibwana Shomary.

Ni kweli wanacheza vizuri kwenye ligi lakini bado hawana uzoefu wa Kapombe na Tshabalala. Kwa Mbegu na Datius ni mara yao ya kwanza kuitwa Stars. Kweli tunategemea wakaanze kwenye mechi hizi muhimu? Ni kamari kubwa.

Ningependa kuona wachezaji wengi zaidi wakiitwa Taifa Stars lakini tusiwazime wengine kwa kutaka kuwapa wengine nafasi.

Hawa vijana wangeendelea kupewa nafasi polepole wakati hao wenye uzoefu wakiendelea kuwepo pia. Ndio nchi nyingi zinafanya hivyo.

Ila kuwazima wengine ili kuwapa nafasi hao wengine siyo sawa. Angalau zingekuwa mechi za kirafiki tungesema wanapewa uzoefu. Ila kwenye mechi hizi muhimu ni kujilipua.

Tunawapa watu sababu za kuongea. Ni kweli tunaweza kufungwa hawa Kapombe na Tshabalala wakiwepo, lakini tukipoteza wakiwa hawapo tunawapa watu maneno.

Inashangaza sana. Naamini Kocha Adel Amouroche hajachagua kikosi hiki, ni sisi wenyewe ndio tuliomchagulia na kumpa kikosi cha kuanzia. Ni kweli hatufahamu ubora wa wachezaji hawa?

Timu ya Taifa lazima iwe na mwendelezo hasa katika maeneo muhimu kama ya ulinzi na ushambuliaji. Huwezi kujaribu tu watu wapya kila siku hasa kama kwenye maeneo hayo una watu wanaofanya vyema.

Kwa upande mwingine niwapongeze kwa kuitwa kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’. Ni kweli hajawa uwanjani kwa muda mrefu lakini bado katika nafasi yake hakuna kiungo aliyeweza kucheza vyema zaidi yake.

Pamoja na kwamba sakata lake bado halijamalizika, ila bado kama taifa tunahitaji ubora wa mchezaji kama Feisal uwanjani.

Tunahitaji ubunifu wake kwenye eneo la mwisho. Nina imani kubwa atafanya vyema.

Yote kwa yote tuitakie kheri Taifa Stars. Ni timu yetu ya taifa na tungependa kuona inafanya vyema sana.

Hawa waamuzi wanakatisha tamaa wawekezaji

Msimu huu kumekuwa na mambo mengi yanaendelea. Kubwa ni kuondolewa kwenye orodha kwa waamuzi zaidi ya 20 kuchezesha ligi.

Tena wengi walioondolewa ni waamuzi wakubwa. Ni kama hawa kina Elly Sasii, Florentina Zablon, Hance Mabena, Soud Lila, Amina Kyando na wengineo.

Waamuzi hawa wazoefu waliondolewa kwa kushindwa kumudu michezo mingi ya ligi. Wamewekwa pembeni na kuachwa hawa waliopo sasa.

Lakini ajabu ni kwamba hawa waliobaki bado hawajifunzi kitu. Vituko vimeendelea kutokea kila siku.

Niliona pale Ubaruku wale Ihefu walipewa penalti ya mchongo dhidi ya Singida Big Stars. Hakukuwa na faulo iliyochezwa ila kwa kuwa mchezaji wa Ihefu alianguka kwenye eneo la hatari basi mwamuzi akafunika.

Singida ikalalamika lakini haikusaidia. Bahati mbaya Ihefu ikakosa mkwaju huo.

Majuzi tukaona kituko kingine pale Tanga. Beki wa Costal Union alimkaba shingoni mshambuliaji wa Singida, France Kazadi Kasengu. Ila kwa uzoefu wake bado Kazadi alifunga goli. Ila kituko ni mwamuzi aliamuru iwe faulo kwenda Singida.

Yaani mchezaji wa Singida ndiye amechezewa faulo tena ndani ya eneo la hatari lakini bado faulo ikaenda kwao. Inashangaza sana. Kituko zaidi kikawa pale Jamhuri Dodoma. Wenyeji Dodoma Jiji wakicheza na Polisi Tanzania. Ndani ya kipindi cha kwanza kulikuwa na matukio manne ya penalti za wazi. Nini kilitokea? Mwamuzi hakutoa hata moja. Inshangaza sana.

Mwamuzi wa Ligi Kuu anashindwaje kuona faulo za wazi kabisa kama zile?