MTU WA MPIRA: Nchi ina uhaba mkubwa wa mabeki wa kati

NCHI imeingia katika janga zito kwa haraka. Ni uhaba mkubwa wa mabeki wa kati. Nani aliwahi kuliwaza hili kwa siku za karibuni? Hakuna!
Alianza kustaafu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ miaka michache nyuma. Baada ya miaka mingi ya kuchezea Yanga na Taifa Stars akaona inatosha. Akatundika daruga.
Ndizo nyakati ambazo Yanga iliona pia pacha wake, Kelvin Yondani amechoka pia kucheza. Ikamruhusu aende zake. Wakaanza maisha mapya.
Usiku wa juzi pale Chamazi kwenye Uwanja wa Azam Complex nilikuwa namuonea huruma Aggrey Morris. Alikuwa akipambana na Fiston Mayele. Alikuwa kwenye wakati mgumu kweli kweli. Akili inatamani kufanya kitu, lakini mwili unagoma. Ndio sababu hata bao la pili la Yanga, Aggrey aliliona shambulizi lakini hakujua cha kufanya. Unajua kwanini? Machi 12, mwaka huu Agrrey alitimiza miaka 38. Ni umri wa mtu mzima. Ni wanasoka wachache bado wanacheza katika timu kubwa wakiwa na umri huo.
Ila ni wanasoka wachache mno ambao bado ni tegemeo katika umri huo. Ndio maana hata pale Manchester United, Cristiano Ronaldo sio tegemeo sana umri umekwenda zake.
Changamoto kubwa sio umri wa Aggrey kusogea. Tatizo ni kwamba mabeki wengi wa shoka wanaondoka kwa pamoja na kuiacha nchi kwenye janga.
Tangu Yondani ameondoka pale Polisi Tanzania bado safu yao ya ulinzi haijakaa sawa. Ndizo nyakati timu yao imekuwa ikiruhusu mabao mengi ya kizembe.
Pale Geita pamoja na kuwaamini vijana wengi, safu yao ya ulinzi ilipwaya muda mwingi. Ndio sababu wakawasaini Yondani na Juma Nyosso kwa pamoja katika dirisha dogo.
Yondani ana miaka 38 pia. Vivyo hivyo kwa Nyosso anatimiza miaka 38, Agosti mwaka huu. Lakini bado wanaendelea kuwa tegemeo pale Geita. Kuna shida mahala.
Mabeki wengi wa kizazi kipya wameshindwa kuwa hodari kama hawa wanaoondoka. Ni Dickson Job na Bakari Mwamnyeto tu wamefikia ubora huo. Wengine wote bado. Tuliwategemea hawa kina Idd Kubwa Mobby, Ibrahim Ame, Kennedy Juma, Abdulmajid Mangalo na wengine kuziba nafasi hizo lakini wameshindwa. Ndio sababu mpaka leo baada ya Job na Mwamnyeto hatufahamu nani ni mbadala wao pale Taifa Stars.
Klabu zetu zinawategemea zaidi mabeki wa kigeni. Unadhani ni kosa lao? Hapana. Sokoni kuna beki gani wa shoka wa kumuweka Henock Inonga benchi? Hakuna.
Ni mabeki wachache wanaonyesha mwanga. Labda huyu Mangalo wa Biashara United. Japo pia bado ana safari ndefu kufikia ubora waliokuwa nayo kina Yondani na Cannavaro.
Baadhi ya timu zinajaribu kuzalisha mabeki wapya, lakini bado hawaonyeshi dalili ya kukua mapema. Beki mzuri anaonekana mapema. Ndio maana Yanga ilimsajili Job mapema tu kutoka pale Mtibwa Sugar.
Azam imewajaribu hawa kina Oscar Masai na Lusajo Mwaikenda lakini bado wana safari ndefu kufika kwenye ubora aliokuwa nao Aggrey. Wana safari ndefu kuziba pengo lake.
Hili la Simba, Yanga ni tatizo sugu
Huwa nawaonea huruma sana Wachungaji na Masheikh wanaofanya kazi ya kukemea mapepo. Huwa naamini ni miongoni mwa kazi ngumu zaidi hapa duniani.
Hebu fikiria unapambana na kitu usichokiona. Ni vita kali za imani na kiroho. Lakini huwa wanapamba kila siku. Wamechagua kazi ya Allah.
Lakini pia kukemea hili tatizo la mashabiki wa Simba na Yanga nayo ni kazi ngumu sana. Ni utamaduni fulani wa kijinga ambao sasa umeanza kuwa fasheni.
Imekuwa kawaida sasa kwa mashabiki wa Simba ama Yanga kwenda kuwapokea wageni pale Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Imetokea mara nyingi.
Majuzi tu hapa tuliona mashabiki wa Yanga wakiipokea RS Berkane ya Morocco. Wakatumia nguvu kubwa kuomba waifunge Simba. Inachekesha sana.
Klabu inapokwenda kwenye mashindano ya kimataifa inawakilisha nchi. Ni kama vile bondia mzawa anapigana na mgeni. Ama Taifa Stars inacheza na Cameroon.
Utanzania unapaswa kutangulia kwanza, lakini ujinga na ushamba wa maisha ya Instagram umewafanya watu kukosa uzalendo. Ni jambo la aibu.
Tunapaswa kuipongeza sana Simba kwa kuufanya Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuwa machinjio ya wageni. Kwa Mkapa imekuwa sehemu ngumu kweli kweli kwa wageni.
Leo hii hadi timu kubwa Afrika kama Al Ahly, Mamelodi Sundowns na nyinginezo zinapaogopa kwa Mkapa. Ndivyo inavyopaswa kuwa. Siyo wageni wanakuja na kutamba kwetu.