Prime
Mpanzu anavyokwenda kuinogesha Simba

Muktasari:
- Winga huyo raia wa DR Congo aliyetambulishwa kikosini hapo Septemba 30 mwaka huu, hakuwa na nafasi ya kucheza kwa sababu ya kuchelewa dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosti 15, mwaka huu.
WANASIMBA walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa sana usajili wa dirisha dogo ufunguliwe ili waanze kuona mavitu ya nyota wao mpya, Elie Mpanzu.
Winga huyo raia wa DR Congo aliyetambulishwa kikosini hapo Septemba 30 mwaka huu, hakuwa na nafasi ya kucheza kwa sababu ya kuchelewa dirisha kubwa la usajili lililofungwa Agosti 15, mwaka huu.
Wakati usajili wa dirisha dogo ukifunguliwa Desemba 15 mwaka huu, sasa ni rasmi Mpanzu ataanza kuitumikia Simba lakini ni katika michuano ya ndani huku akisubiri hadi Januari kuanza kuonekana kimataifa.
Leo Jumatano, Simba itaikaribisha KenGold kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar, hapo tunaweza kumshuhudia Mpanzu akiitumikia timu hiyo kwa mara ya kwanza katika mechi za kimashindano.

Usajili wa Mpanzu umeonekana kumkosha kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids baada ya kusema wazi akianza kuitumikia timu hiyo kuna kitu kitaongezeka eneo la ushambuliaji.
“Mpanzu amechangamka, ni mtu mwenye ushirikiano na mchango mkubwa kwenye timu, nasubiri kwa hamu aanze kazi, kwani imani yangu ni kubwa kutokana na kiwango bora alichokionyesha,” alisema kocha huyo Msauzi na kuongeza.
“Kuwa na mchezaji mwenye uwezo wa kucheza maeneo mawili akitokea pembeni ni jambo zuri kwani anakupa vitu vingi uwanjani, naweza kumtegemea kama kiungo na hata winga.”
Uchezaji wa Mpanzu, ndani ya kikosi cha Simba anakwenda kupambania nafasi na Kibu Denis, Edwin Balua, Ladaki Chasambi, Joshua Mutale na Saleh Karabaka, ambao wamekuwa wakipishana mara kwa mara eneo la kiungo mshambuliaji kutokea pembeni.

Mbali na eneo hilo, pia Mpanzu anaweza kucheza kama mshambuliaji wa pili kwa maana ya namba kumi huku akiwa na uwezo wa kufunga na kutengeneza nafasi kwa wenzake. Nafasi hiyo huwa anacheza Awesu Awesu na Jean Charles Ahoua. Wakati mwingine anaweza kusimamishwa mshambuliaji wa mwisho, aliwahi kucheza mara kadhaa akiwa AS Vita. Eneo hilo Simba inawategemea Leonel Ateba anayesaidiana na Steven Mukwala, huku Valentino Mashaka naye akicheza hapo.
Kukaa takribani miezi mitatu akifanya mazoezi na wenzake bila ya kucheza mechi za kiushindani huku ikielezwa amekuwa akionyesha juhudi kubwa, ni wazi Mpanzu ana kitu anataka kuonyesha kwa nini mabosi wa Simba walimsajili.
“Shauku ya Mpanzu ni kufanya vizuri wakati wote, namuona mazoezini anavyojituma kama anacheza mechi kubwa, wachezaji wenzake ni mashahidi, nasubiri muda wake wa kucheza ufike ili aongeze ushindani ndani ya timu,” alibainisha Fadlu.

Mpanzu amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba na kutambulishwa Septemba 30 mwaka huu, huku akikadiriwa kuchukua Sh782milioni ndani ya mkataba huo.
Kabla ya kutua Simba akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na AS Vita kumalizika, aliripotiwa kufanya majaribio KRC Genk ya Ubelgiji lakini mambo hayakwenda vizuri.
KUANZA KUCHEZA
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi alisema Mpanzu ataitumikia Simba mara baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa kwa kuwa ni mchezaji huru, lakini lazima timu hiyo imuondoe mchezaji mmoja wa kimataifa kwani idadi waliyonayo sasa ukimuweka kando nyota huyo imetimia 12.
“Ataweza kucheza baada ya dirisha dogo kufunguliwa mwezi huu, lakini kuhusu idadi ya wachezaji wakigeni tayari walishakamilisha 12 wanaohitajika kikanuni ili kuingiza jina la Mpanzu,” alisema Madadi.
Nyota wa kigeni waliopo Simba hivi sasa ukimwondoa Mpanzu ni Moussa Camara na Ayoub Lakred ambao ni makipa. Mabeki wapo Che Malone Fondoh, Chamou Karaboue na Valentine Nouma.

Viungo ni Fabrice Ngoma, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Jean Charles Ahoua na Debora Mavambo huku washambuliaji wakiwa Steven Mukwala na Leonel Ateba ambaye alikuwa nyota wa mwisho kusajiliwa dirisha kubwa msimu huu.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Simba zinabainisha Ayoub Lakred ambaye alifanya vizuri msimu uliopita wakati kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula akisumbuliwa na majeraha ya muda mrefu, ndiye atakatwa kisha Mpanzu achukue nafasi yake.
Ayoub aliyeongeza mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Simba mwanzoni mwa msimu huu, hajacheza mechi yoyote tangu asaini mkataba huo kutokana na kuuguza majeraha huku akionekana kupoteza nafasi mbele ya Camara aliyecheza mechi zote za kimashindano za Simba msimu huu kuanzia Ngao ya Jamii (2), Ligi Kuu Bara (11) na Kombe la Shirikisho Afrika (5).
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmedy Ally, ameweka wazi siku ambayo Mpanzu anaweza kuonekana kimataifa akisema: “Mechi yetu ya marudiano katika michuano ya Shirikisho dhidi ya SC Sfaxien ya Tunisia ndio ataweza kucheza. Mchezo huo utachezwa Januari 2025 na atakuwa tayari, pia ITC yake ilishafika kilichobaki ni kukamilisha mchakato wa kikanuni kwa usajili wake kuingizwa kwenye mfumo.”
ANACHOKWENDA KUKIONGEZA
Kutokana na namna ambavyo Fadlu amemuona nyota huyo huku ikielezwa bado haridhishwi na timu inavyotengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia vizuri, ni wazi Mpanzu kuna watu anakwenda kuwaweka benchi.
Tukianzia eneo la kiungo cha ushambuliaji kutokea pembeni (winga), Simba ina utajiri wa wachezaji hapo wakiwemo watano, Mpanzu anakuwa wa sita. Nyota hao ni Karabaka, Balua, Chasambi, Mutale na Kibu.
Ukiangalia takwimu za nyota hao katika michuano tofauti msimu huu, Karabaka ndiye mwenye namba ndogo zaidi akitumika kwenye mechi mbili pekee, moja Ngao ya Jamii na alifunga bao dhidi ya Coastal Union na kuifanya Simba kushika nafasi ya tatu waliposhinda 1-0.

Pia akacheza kwa dakika tisa mechi moja ya ligi dhidi ya Fountain Gate, hana asisti wala bao lingine zaidi. Namba hizo zinaonyesha si mchezaji ambaye anapewa nafasi kubwa ya kucheza.
Mpanzu mwenye umri wa miaka 22, rekodi zinaonyesha hana namba nzuri katika kucheka na nyavu tangu akiwa AS Vita aliyojiunga nayo mwaka 2022 kwani msimu wa 2023-2024 alicheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali bila ya kufunga.
Kasi yake na ubunifu katika eneo la mwisho, inatajwa ndiyo silaha kubwa inayombeba kitu ambacho Fadlu anaamini kitaongeza kitu katika kikosi chake.
Kama ilivyo kwa Leonel Ateba ambaye ametua Simba akitokea USM Alger alipocheza kwa miezi sita, namba zake hazikuwa nzuri lakini amekuwa mtu muhimu kikosini hapo eneo la mshambuliaji wa mwisho.
Ateba ambaye msimu mzima wa 2023-2024 alifunga mabao matatu na asisti saba katika mechi 23 za mashindano tofauti akizitumikia USM Alger ya Algeria na Dynamo Doula ya kwao Cameroon, ndiye mshambuliaji kiongozi wa Simba.
Hivyo licha ya kwamba namba za Mpanzu ambaye bado ana muda mwingi wa kucheza kutokana na umri wake kutokuwa nzuri hivi sasa, lakini anaweza kuwa kiungo muhimu ndani ya Simba katika suala la kuzalisha mabao.
Simba ikiwa imefunga mabao 30 katika mechi 18 za mashindano tofauti msimu huu (ligi Kuu – 22, Kombe la Shirikisho – 7 na Ngao ya Jamii - 1), asilimia kubwa yametokana na viungo wake hivyo Mpanzu anakwenda kuongeza kitu hapo.
Ukiangalia ndani ya ligi, Simba ikiwa imefunga mabao 22, viungo washambuliaji wamehusika kwenye mabao 14 wakifunga manane na asisti sita.
Kwa upande wa kimataifa, Simba imefunga mabao saba, viungo washambuliaji wamehusika kwenye mabao matano.
Lile bao moja la Ngao ya Jamii pia limefungwa na kiungo mshambuliaji. Kwa takwimu hizo, ni wazi Simba nguvu yao ipo hapo ndio maana imemchukua Mpanzu kuendelea kujiimarisha zaidi.
TAKWIMU ZA VIUNGO WASHAMBULIAJI
Edwin Balua takwimu zake katika Ligi Kuu Bara msimu huu, amecheza mechi nane kati ya 11 kwa dakika 341 huku akifanikiwa kufunga mabao mawili, hana asisti.
Kwa upande wa kimataifa, winga huyo ana bao moja alilofunga dhidi ya Al Ahli Tripoli wakati Simba ikishinda 3-1.
Ladack Chasambi hakuanza vizuri msimu, mechi sita za kwanza katika ligi alizikosa zote, akaibukia dhidi ya Tanzania Prisons na tangu hapo amekuwa akicheza kikosi cha kwanza akicheza mechi tano za ligi kwa dakika 338. Kimataifa pia hana bao wala asisti.
Kibu Denis ni kati ya wachezaji wanaopewa nafasi kubwa sana ya kucheza kwenye eneo la winga kwani amekosekana mechi moja tu ya ligi kati ya 11 ambazo Simba imecheza.
Nyota huyo ambaye hajafunga bao lolote kwenye ligi kwa takribani siku 407 tangu alipofanya hivyo Novemba 5, 2023 wakati Simba ikifungwa 5-1 na Yanga, bado amekuwa mchezaji muhimu na kimataifa amefunga mabao matatu yakiwemo mawili ya hivi karibuni walipoilaza CS Sfaxien 2-1 hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, kabla ya hapo alifunga bao la kusawazisha dhidi ya Al Ahli Tripoli kabla ya mengine kufungwa na Leonel Ateba na Edwin Balua, Simba ikishinda 3-1 na kufuzu makundi ya michuano hiyo.
Katika mechi 10 za ligi alizocheza msimu huu, ametumika kwa dakika 597.
Joshua Mutale alitarajiwa ataiongoza vizuri safu hiyo kutokana na kasi aliyonayo, lakini ameonekana kutokuwa mbunifu eneo la mwisho huku majeraha ya mara kwa mara yakitajwa kumtibulia huku ikielezwa mabosi wa timu hiyo wanafikiria kuvunja mkataba wake.
Licha ya kucheza mechi saba za ligi kwa dakika 356 sambamba na zile za kimataifa, lakini hajafunga wala kuasisti. Katika mechi zote hizo, hakuna aliyomaliza dakika 90.
Awesu Awesu anafuatia kwa kucheza mechi nyingi za ligi sambamba na Kibu. Awesu ambaye ametua Simba msimu huu akitokea KMC, naye anaonekana kuwa muhimu kikosini hapo akichangia mabao matatu katika ligi akifunga mawili na asisti moja akicheza mechi 10 kwa dakika 448.
Jean Charles Ahoua, huyu anacheza namba 10, eneo ambalo pia Mpanzu anaweza kucheza. Ahoua ndiye mchezaji mwenye mchango mkubwa wa mabao katika kikosi cha Simba msimu huu kutokana na kufunga matano na asisti nne kwenye ligi, huku kimataifa akifunga mabao mawili likiwemo lile lililowapa ushindi Simba wa 1-0 dhidi ya Bravos ukiwa ni mchezo wa kwanza hatua ya makundi.
Juzi alitoa asisti katika bao la kwanza lililofungwa na Kibu dhidi ya CS Sfaxien. Dakika zake ndani ya ligi ni 707 akicheza mechi 10, kati ya hizo nne amemaliza dakika zote 90.
WASHAMBULIAJI JE?
Valentino Mashaka alianza kwa kasi, alicheza mechi mbili za kwanza na kufnga mabao mawili, hadi leo hajaonekana uwanjani katika mechi yoyote ile huku majeraha yakitajwa kumuandama.
Katika mechi mbili alizocheza, zote alitokea benchi akitumika kwa dakika 68 pekee.
Steven Mukwala ndiye alitoa asisti wakati Simba ikishinda 1-0 katika Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union na kukamata nafasi ya tatu.
Kwenye ligi amecheza mechi zote 11 lakini kuna wakati amekuwa akiingia uwanjani kama kuongeza namba tu kwani mechi mbili dhidi ya Yanga na Pamba Jiji aliingia katika muda wa nyongeza za kufidia kuwa 90. Huku dhidi ya Coastal Union akiingia dakika ya 86. Pia mechi mbili dhidi ya Namungo na KMC akimaliza dakika zote tisini.
Kwa jumla, Mukwala amecheza mechi 11 za ligi kwa dakika 419 akifunga mabao mawili na asisti mbili. Leonel Ateba ambaye alikuwa mchezaji wa mwisho kusajiliwa Simba dirisha kubwa msimu huu, amecheza mechi nane za ligi na kufungua mabao matatu akitoa asisti moja, kimataifa ana bao moja.
Kutokana na kuchelewa kwake kuungana na timu, alizikosa mechi mbili za ligi za kwanza. Pia alikosekana katika mchezo wa 10 dhidi ya KMC. Dakika zake kwenye ligi ni 577 huku mechi tatu akimaliza dakika zote tisini.