Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morad: Hizi simba na yanga sijawahi kuzitamani

New Content Item (1)
New Content Item (1)

UMESHAWAHI kupiga stori na Morad? Jamaa anachekesha sana na zaidi ya yote hutatamani aache kukusimulia mambo yake.

Ana matukio mengi ndani na nje ya uwanja na akikusimullia huchoki kumsikiliza, hasa anaposimulia tukio la kupigwa kwa refa kwenye mchezo wa Azam FC dhidi ya Yanga, ingawa pia ana stori zake za kuhuzunisha. Mwanaspoti lilifanya mahojiano na nyota huyo wa zamani wa Azam FC na Taifa Stars, Said Morad na kueleza mambomengi ikiwamo kwa nini hakutaka kabisa kucheza Simba na Yanga na kwa nini anaipenda Azam.


AFURAHI REFA KUPIGWA

Morad anakumbuka tukio la refa kupigwa kwenye mchezo wao akiwa Azam dhidi ya Yanga.

Ilikuwa Machi 2012 na anasimulia namna tukio lile lilivyompa nafuu siku hiyo kwenye mchezo huo. “Si kwamba nilifurahia alivyopigwa, hapana. Ni kwa sababu tulipata nafuu kutokana na mchezo,” anasimulia akikumbuka mchezo ulivyokuwa.

“Kwanza wakati wa ugomvi nikakaa pembeni sikutaka kuamulia, baada ya kazi nikawapa pole.” anasema na kuongeza;.

“Nakumbuka mchezo ulikuwa mgumu sana. Yanga ilivyoona mambo magumu, wakawa na hasira. Nadir Haroub ‘Canavaro’ alitolewa anje kwa kadi nyekundu na hilo liliibua mzozo na wachezaji wengine wakiongozwa na Stephane Mwasika walimshambulia mwamuzi Israel Nkongo, Mwasika akapewa kadi nyekundu. Ilitupa nafuu kwani pia tulishinda mchezo huo mabao 3-1.”


UMRI NAMBA TU, KUKIPIGA KAMA RONALDO

Morad ambaye anajiamini kweli kweli, anaona bado ana nafasi ya kuendelea kukipiga popote, kuanzia ligi za madaraja ya chini hadi Ligi Kuu anasema

“Nitakuwa Christiano Ronaldo wa Tanzania, licha ya umri kwenda kuna madogo nitawaburuza kwa kuonyesha uwezo wangu.”


ALIVYOONDOKA AZAM

 Anakumbuka alivyoondoka Azam bila kutarajia na jambo hilo lilimchanganya na kumkosesha raha.

“Hadi leo sijui kwa nini Azam iliniacha, ni swali linalonisumbua moyo wangu, ila ninavyoipenda  sitofautiani na mashabiki wa Simba na Yanga wanavyozipenda timu hizo,” anasema na kuongeza;

“Zikiwa zimebakia mechi tano kabla ya kuchukua ubingwa 2013/14 mkataba wangu ulikuwa umeisha, lakini sikuacha kujituma kwa bidii hadi tukafanikisha taji hilo, sasa baada ya kumalizika kwa msimu nikaambiwa natakiwa kwenda Mzizima.

“Nikajua nakwenda kusaini mkataba mpya, ajabu nikakutana na barua ya kuachana na mimi, hali hiyo iliniumiza sana, nikamkumbuka Erasto Nyoni aliyeniambia mapema niulize kuhusu mkataba wangu.”

Anasema anatamani kupata nafasi ya kuzungumza na Yusuf Bakhresa, ishu ambayo hawezi kuizungumza kwenye vyombo vya Habari.

“Namwomba yeye maana wakati nasajiliwa Azam sikuwa na meneja, ndiye aliyenisainisha, ukiachana na hilo nina mengi ya kuzungumza naye,” anasema.


HAZITAKI SIMBA, YANGA

Anasema kwenye maisha yake, hajawahi kuzihusudu jezi za Simba na Yanga na hatarajii kufanya hivyo, kwani timu yake pendwa kwa hapa Tanzania ni Azam.

Anaeleza timu hiyo, imebeba tafsiri ya kujivunia kucheza soka kwa kiwango cha juu na hakuwahi kutamani kuzichezea Simba na Yanga, kwani matarajio yake yalikuwa akistaafu uwanjani, angetumika kwenye sekta nyingine ndani ya klabu hiyo.


TUHUMA ZA RUSHWA

Morad alikuwa kati ya wachezaji wanne waliowahi kutuhumiwa kuchukua rushwa kutoka Simba na timu yake ilifungwa mabao 3-1 mwaka 2011, wenzake ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Aggrey Moris na  Erasto Nyoni, amelifafanua hilo.

“Sikuwahi kuchukua pesa ya Simba, ni kitu ambacho kiliniumiza sana, kwani tuliitwa hadi Takukuru na hawakunikuta na makosa, nilipata wakati mgumu sana mbele ya jamii,” anasema na kuongeza;

“Nakumbuka nilikuwa nikienda kucheza ndondo mtaani wakati tumesimamishwa, mashabiki walikuwa wananiita ‘mla rushwa huyo’, basi walinifanya nijitume kwa bidii, ili waache kuniita hivyo badala yake washangilie kazi zangu.

“Ishu hiyo nadhani ni timu pinzani zilikuwa zinataka kuharibu timu tu, kwani kipindi hicho Azam tulikuwa wa moto sana, wakaona wakituvuruga watakuwa wamefanikiwa kupunguza makali ya timu.”


KUSINGIZIWA DAWA

Anasema kuna wakati alipitia maisha magumu kiasi kwamba alishindwa hadi kuzitunza rasta zake. Hii ilisababisha hadi watu kuanza kufikiri anatumia dawa za kulevya.Ndipo akaamua kuzinyoa.

“Nilinyoa rasta zangu baada ya kipindi hicho kushindwa kuzitunza, ndio maana unaniona nina staili nyingine kichwani, usiombe upitie nyakati ngumu ambazo jamii inakuwa inakushusha thamani yako, inahitaji msaada wa Mungu kuvuka nyakati hizo,” anasema na kuongeza.

“Baada ya kunyoa rasta zangu maneno ya kusemwa natumia dawa za kulevya hayapo tena, wakati mwingine naonekana mfano wa vijana wanaopambana zaidi mtaani.”

Anawakumbusha wachezaji wa sasa kujiwekeza zaidi kipindi hiki ambacho wao wanapata pesa ndefu “Kipindi nasajiliwa mimi Azam kwa mara ya kwanza kutoka Kagera Sugar nilipewa Sh5 milioni, ikaanza kupanda wakati naendelea kucheza, tofauti na sasa wanavuta pesa ndefu.”


KISA CHA MAPENZI

Kama hujui kwa wachezaji kuna wakati inawawia vigumu kupata wenza wao wa maisha, wengi wao wanajikuta wakiambulia maumivu makali, hayo yalimkuta Morad.

Anaeleza namna wachezaji wanakaa muda mchache mtaani, hivyo inawawia wakati ngumu kujua wenza wema wa maisha yao, ndio maana asilimia kubwa wengi ndoa zinawasumbua.

“Niliwahi kukutana na mwanamke ambaye alinifanyia matukio, ingawa kuna wakati nikikaa chini na kutafakari naona ilikuwa sahihi kupigwa matukio, kutokana na sehemu nilikokutana naye,” anasema na kuongeza;

“Kuna sehemu ya baa nilikuwa nakwenda kunywa, hivyo nilimwona mara kadhaa, nikaanza kumpanga si nikajua atakuwa mke mwema kumbe najichimbia shimo.

“Basi nikamchukua na kuanza kuishi naye, kama unavyojua kazi ya mpira ni kusafiri, nilikuwa nikirudi nyumbani washikaji wananiambia mwanamke wako anafanya vitu vya ovyo, nikawa naona wana wivu, sasa kuna siku baada ya kutoka safari nikakuta kabeba vitu vya ndani na kuondoka.

“Nilikaa naye kwa muda wa miezi sita, iliniumiza kwani niliweka malengo ya kumuoa, kumbe ningechukua bomu la kunilipua, pamoja na hayo yote kwa sasa naishi na mwanamke ila bado hatujafunga ndoa.”


TATOO ZA 2.2 MILIONI

Kwenye mwili wake anaishi na tatoo sita zilizomgharimu Sh2.2 milioni kuzichora ingawa haoni kama zina maana yoyote, alizipenda kama fasheni tu.

“Kila mchezaji anapenda muonekano fulani, zipo ambazo nilichora nikiwa India na nyingine hapa hapa Tanzania, ila siyo kwamba zinamaanisha kitu chochote,” anasema.

Je unataka kujua Nepal alikwenda kufanya nini? anasimulia “Nilikwenda kusaka maisha nilikuwa nacheza timu za madaraja ya chini,tulipata koneksheni kupitia Pius Kasambala ambaye mara ya kwanza walienda na Shadrack Nsajigwa.

“Wakati naenda huko sikuwa na meneja, nikauza mashamba mawili ya kunisaidia nauli, tuliondoka na Yona Ndabila, nikatoka huko nikaenda India, kisha Hong Kong ambako nilikutana na mama mtoto wangu ni Mtanzania, nikazaa naye mtoto mmoja anaitwa Fahumu, wanaishi huko huko.”


NYAKATI NGUMU ALIZOPITIA

Baada ya kurejea Tanzania hakukata tamaa kupambania kipaji chake, akajiunga na Kagera Sugar kwa miezi sita na baada ya mkataba wake kumalizika akaachana nao.

“Nilivyoondoka Kagera nikaanza kucheza ndondo hadi leo, mara nyingi timu ninazofanya nazo mazoezi mtaani wakiwa na mechi wananipigia simu kuniambia kuna kazi, kuna sehemu unaokota Sh40,000, wakati mwingine 30,000 maisha yanaenda,” anasema na kuongeza;

“Nipo fiti kwa sababu nafanya sana mazoezi, nikimaliza ya asubuhi wakati mwingine uwanjani au ya kukimbia naoga nakuja kwenye shughuli zangu za kuuza spea za magari kwenye ofisi ya Juma Shine, ikifika saa 10:00 jioni wananiruhusu naingia gmy baada ya hapo nakuja tena ofisini kufunga duka.”


KIKOSI BORA

Morad ametaja kikosi chake bora katika maisha ya soka akianza na Ivo Mapunda, Erasto Nyoni, Juma Jabu, Morad, Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji’, Himid Mao, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Elias Maguri na Danny Mrwanda.

Anakizungumzia kikosi hicho kwamba kwa enzi hizo wakati wapo moto, anaamini wangekutana na timu pinzani wangekiwasha na kuifunga.

“Kila kipindi kina wachezaji wake, binafsi hicho kikosi nilichokutajia, hao jamaa walikuwa wanaupiga mwingi sana, wanastahili heshima yao,” anasema.

Kwa sasa anamtaja beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Abdullah Hamad ‘Bacca’ ndie anafanya vizuri,

”Ni mchezaji asiyekata tamaa, nakumbuka wakati nacheza Azam alikuja kufanya majaribio akiwa mdogo na alikuwa anapenda ninavyocheza na sasa kapambana ni msaada kwa Yanga.”