Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rio buana! Eti kwa Carrick anafumba mdomo!

PAZIA Pict


“...MPE mkataba mezani, aambiwe asaini mkataba. Aweke kiasi chochote cha pesa anachotaka kama mshahara. Hakuna haja ya kuchelewa. Manchester United imerudi tena kuwa kama ilivyokuwa. Fanyeni haraka. Ole ameshikilia usukani tena..”


Mwili ulikuwa umemsisimka Rio Ferdinand wakati akisema hivi Machi 2019 wakati kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, alipokuwa anafanya vyema katika kibarua chake alichopokea kutoka kwa Jose Mourinho ambaye alikuwa amefukuzwa old Trafford. Rio alikuwa amesisimkwa haswa.


Nyakati hizo kulikuwa na kizungumkuti cha joto ambalo Sir Alex Ferguson alikuwa ameliacha Manchester United. United walikuwa wamemfukuza David Moyes. Baadaye nafasi yake ikaenda kwa Ryan Giggs ambaye alikuwa ameishikilia timu kwa mechi chache. Baadaye Giggs akaachilia kiti na nafasi ikaenda kwa Louis van Gaal.

Baadaye maisha yakawa magumu kwa Van Gaal nafasi ikaenda kwa Jose Mourinho. Huyu Mreno kiburi naye maisha yake yakawa magumu kwake na baadaye nafasi yake ikaenda kwa Solskjaer kama kocha wa muda.

Mechi chache za kwanza Ole Gunnar alishinda mechi nyingi mfululizo. Moja kati ya mechi ambazo alishinda na Rio Ferdinand akajikuta anaropoka ni hii hapa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG. Hapo ndipo Rio akaropoka nilichoandika hapo juu.

Na kweli, United wakamsikiliza Rio. Sio Rio pekee, United waliwasikiliza mashabiki wengi ambao walitaka Ole Gunnar apewe kiti moja kwa moja. Miongoni mwa wanafiki ambao walisimama nyuma ya Rio ni pamoja na mastaa wa zamani wa Manchester United.

Kina Roy Keane, Garry Neville, Paul Scholes walimpiga mawe ya kutosha Mourinho wakati timu ikiwa inayumba. Mshkaji wao alipoonyesha mwelekeo mzuri wakataka apewe timu moja kwa moja. Na kweli akapewa. Kilichofuata ni historia. Manchester United ilidoda katika mikono ya Ole Gunnar mpaka alipofukuzwa.

Nadhani ndio maana sasa hivi Rio atakuwa anaiangalia hali nzima inayoendelea Manchester United na anaamua kukaa kimya. Michael Carrick amepewa timu na imekuwa ya moto haswa. Arsenal alikufa mabao 2-3 akiwa nyumbani. Matokeo pekee hasi ambayo Manchester United imepata baada ya ujio wa Carrick ni sare ya 1-1 ugenini kwa West ham Jumatano usiku.

PAZ 05

Vinginevyo Carrick amerudisha tabasamu. Hata hivyo, Rio anaambatana na mashabiki wengi wa Manchester United ambao hawana uhakika na kinachoendelea. Kitadumu au ni suala la muda tu? Kuna mambo mawili ambayo huwa wanayakumbuka zaidi kwa sasa. Mambo ambayo yanawafanya wasiamini katika ndoto zao.

Jambo la kwanza ni kwamba walishawahi kuwa na kocha kama Carrick hapo nyuma. Kocha aliyempa jeuri Rio. Rafiki yetu Ole Gunnar. Kuna wakati huwa inatokea. Kocha anakuwa wa moto kwelikweli akiwa kama kocha wa muda, lakini akipewa jukumu rasmi mambo yanaenda kombo. Manchester United sio timu ya kwanza kumuamini kocha wa muda halafu akipewa kazi mambo yanaenda mrama.

PAZ 04

Jambo jingine ambalo linaweza kuwapa jinamizi Manchester United ni ukweli kwamba Carrick alifukuzwa na Middlesbrough Juni msimu uliopita baada ya kushindwa kuipeleka timu walau katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Championship kufuzu kwenda Ligi Kuu England baada ya kushindwa kupata nafasi mbili za juu ambazo timu hufuzu moja kwa moja kwenda katika ligi hiyo.

Kwa mfumo wa Ligi Daraja la Kwanza England maarufu kama Championship timu mbili za juu zinapanda moja kwa moja halafu timu nne zinazofuata kwa maana ya timu ya tatu hadi ya sita huwa zinacheza mtoano mpaka apatikane mtu mmoja wa kucheza ligi kuu.

PAZ 03

Carrick na Middlesbrough yake waliishia nje ya timu sita za juu na mabosi wake wakaona inatosha. Wakamuonyesha mlango wa kutokea. Mashabiki wa Manchester United ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu Carrick watakuwa wanashangaa kinachotokea kwa sasa.

Wengi kati yao wanaweza kuhisi kwamba kinachotokea kwa sasa ni moto wa kifuu tu baada ya Carrick kushika mikoba ya Ruben Amorim. Wakikumbuka na kilichotokea kwa Solskjaer ni wazi kwamba watakuwa na wakati mgumu kumuamini Carrick.

Kitu kingine kikubwa zaidi ambacho kitakuwa kinawapa kizunguzungu mashabiki wa Manchester United ni jinamizi ambalo wanalo tangu Sir Alex Ferguson aondoke zake Old Trafford 2013.

Wamejaribu kila aina ya makocha klabuni lakini mambo yameendelea kuwa magumu. Hawataamini kwamba kuna mtu atawakoa mpaka mtu huyo akifanikiwa kufanya hivyo.

PAZ 02

United imejaribu kwa makocha ambao walikuwa wana uzoefu wa kawaida na wakatengeneza vikosi vizuri walikotoka ikaonekana kwamba labda tatizo lilikuwa pesa tu kwa makocha hao kufanikiwa.

Na wao pesa wanazo. Ndio maana wakampa timu David Moyes wa Everton kwa ajili ya kumrithi Sir Alex Ferguson. Hata hivyo mambo yalishindikana kwa kiwango kikubwa tu.

Wakajaribu kwa makocha wazoefu kama Louis van Gaal na Jose Mourinho. Bado mambo yalikuwa magumu na yakashindikana kwa kiasi kikubwa. Wote hawa wawili walionekana kuwa daraja la juu ya Moyes. Wote hawa walionekana kwamba wangeweza kuwa karibu na kariba ya Sir Alex Ferguson lakini mambo bado yalishindikana kwa kiasi kikubwa.

Wakarudi tena kwa makocha ambao walionekana wanachipukia barani Ulaya na wangeweza kufanya kazi kama ile ambayo Mikel Arteta ameifanyia Arsenal au Cesc Fabregas ameifanyia Como ya Italia.

PAZ 01

Wakaenda kwa Ruben Amorim na wakampa mradi wao wa muda mrefu. Bado ilishindikana kwa kiasi kikubwa na wote tunakumbuka namna ambavyo Amorim ameiacha Manchester United katika shimo.

Sihitaji kurudia tena na tena katika makala hii hii moja kuelezea namna ambavyo waliwahi hata kumuamini kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer awe kocha wa kudumu. Kiukweli wamejaribu kwa kila namna. Manchester United bado haina mwelekeo wa kushindania mataji makubwa katika soka la Ulaya kwa sasa.

Na sasa tunasubiri Carrick ataishia wapi msimu huu. Na tunasubiri kuona kama akiishia vizuri je Manchester United wanaweza kumuamini katika mradi wao mpya akapambane na akina Pep Guardiola na Mikel Arteta msimu ujao.

Ni jambo la kusubiri na kuona. Ukiniuliza maoni yangu nitakwambia kwamba Carrick ni moto wa kifuu tu. Inawezekana ana mambo machache amebadili lakini sio kocha wa kumuamini kumpa timu.

Siku nyingine naweza kurudi hapa na kuelezea namna ambavyo Xabi Alonso anavyoweza kuwa kocha mzuri Manchester United msimu ujao. Unaweza usinielewe kwa sababu ametoka kufukuzwa Real Madrid baada ya timu kukosa mwelekeo lakini nina sababu zaidi ya tano ambazo nitakueleza kwanini Alonso ni kocha mwafaka Manchester United msimu ujao.