MJUAJI: Simba, Yanga zafurahia vifo vya dabi zao

LEO Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kinawaka tena. Ni katika dabi. Ndio Tanzania dabi imebaki moja tu. Ni Simba dhidi ya Yanga. Hakuna nyingine. Dabi hii unaweza kuiita utakavyo Kariakoo Dabi, Dar es Salaam Dabi na hata Tanzania Dabi.
Ni pekee kubwa na yenye hadhi Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla. Na hii imekuja baada ya Simba na Yanga kufanikiwa kuua dabi nyingine zilizokuwa zinataka kuibuka dhidi yao.
KWANINI DABI
Ni baada ya baadhi ya viongozi na wachezaji wa timu ya New Young mwaka 1936 walipougomea uongozi wa timu hiyo na hatimaye kujitenga. Waliojitenga walijiita majina mbalimbali mpaka walifikia kujiita Simba. Awali walianza naa ‘Stanley’, Eagle of Night- (Tai wa Usiku) na Sunderland. Sunderland ilivuma sana Dar es Salaam na vijana walioanzisha walikuwa ni waliotoka katika madrasa ya Maalim Bu-Hamis. Lakini mwanzoni mwa miaka ya 1970 ikaitwa Simba Sports Club. Hivyo ndivyo dabi ilipozaliwa na kumbuka kabla ya kugawanyika New Young ilipitia majina mengine ya Jangwani Boys mwaka 1929 na baadaye Taliana na mwaka 1935 ndipo ikajiita Young African.
Mpinzani pekee aliyekuwa akizisumbua timu hizo tangu mwaka 1964 katika Ligi ya Taifa ilipoanzishwa ni Cosmopolitan. Ilikuwa timu ya kwanza kubeba ubingwa nje ya Simba na Yanga katika historia ya Ligi Kuu.
UPINZANI WA NDANI YA SIMBA, YANGA
Mwaka 1975, Simba ilianza kupata upinzani kutoka ndani ya klabu yao baada ya kufanyika uchaguzi na viongozi waliokuwa madarakani wote kupigwa chini.
Uchaguzi huo uliosimamamiwa na Katibu wa TANU Mkoa wa Dar es Salaam, Joseph Rwegasira ulisababisha wanachama wa Simba wapatao 50 kujiengua kwenye timu. Wanachama hao wakaanzisha Nyota Nyekundu iliyokuwa na masikani yake Mtaa wa Kongo na Aggrey jijini Dar es Salaam mita chache kutoka ilipo Klabu ya Simba. Alhamisi ya Mei 09, 1975 Mussa Libabu Mwambangulu alitangazwa kuwa mwenyekiti wa muda wa Nyota Nyekundu (Red Star). Cannute Mtemanyenje alichaguliwa kuwa katibu wa klabu hiyo.
wengine ni Amir Ali Bamchawi, A. Fakrudini na aliyekuwa nahodha wa Simba, Haidar Abeid naye alijiunga na timu hiyo.
Wengine ni Burhan Mlanzi na Hassan Haji (babu yake Haji Manara upande wa mama yake mzazi).
MECHI NGUMU
Simba ilikuwa na mechi ngumu ilipokutana na Nyota Nyekundu. Upinzani wake ulikuwa ni kama ule dhidi ya mtani wake wa jadi, Yanga. Hii ilitokana na viongozi wa timu hizo kujua kila mbinu za kutafuta matokeo ya ushindi ndani na nje ya uwanja. Kwa kuwa walikuwa pamoja kwa muda mrefu.
Mbaya zaidi, Nyota Nyekundu ikawa inaiba wachezaji wa Simba kama vile kina Abbas Said Mhunzi ‘Cooker’ na Maulid Dilunga ‘Mexico’. Hata mwaka 1982, Red Star iliwachukua baadhi ya wachezaji wa kikosi cha pili cha Simba akiwemo Rosta Ndunguru.
YANGA NAYO KILIIKUTA
Baada ya mgogoro kufukuta ndani ya klabu hiyo kwa muda mrefu hatimaye mwaka 1976, Yanga ilipasuka mara mbili. Ilikuwa baada ya Mwenyekiti Mangala Tabu Mangala na David Sam Mwambungu kutofautiana na ulipofanyika uchaguzi Juni 20, 1977 viongozi 15 wa zamani wa Yanga walishindwa kwenye uchaguzi huo. Ni Mangala peke yake aliyetetea kiti chake. Kumbuka uchaguzi huo pia ulikuwa chini ya Rwegasira.
KARIAKOO DABI SITA
Mbali na viongozi wa zamani kujiengua, Agosti, 1979 Yanga ilipoteza wachezaji takribani 14 ambao walikwenda kujiunga na Nyota Afrika ya Morogoro na baadaye kurudi Dar es Salaam na kujiunga na timu ya Zama za Kale au Zamaleki ya Upanga na kuibadili jina kuiita Pan Africans.
Upinzani kati ya Pan na Yanga ulikuwa mkali. Ilikuwa ni vita ya viongozi wanaojuana kama ilivyokuwa kwa Simba na Nyota Nyekundu. Pan nayo iliweka masikani yake Kariakoo katika Mtaa wa Swahili na Kariakoo. Kama leo hii timu hizo zingekuwepo Ligi Kuu, basi kungekuwa na dabi za Kariakoo sita. Simba na Yanga, Pan na Yanga, Simba na Nyota Nyekundu na Pan na Simba na Nyota Nyekundu na Yanga na pia Pan na Nyota Nyekundu.
RAHA ZAIDI
Pan ilipocheza dhidi ya Simba ni kama vile Yanga ilikuwa ikicheza na miamba hiyo ya Msimbazi, hali kadhalika kwa Nyota Nyekundu ilivyokuwa ikicheza dhidi ya Yanga. Na hata zilipokutana zenyewe kwa zenyewe zilikuwa na ule upinzani wa Uyanga na Usimba. Pan ilipokutana na Yanga moto uliwaka kama vile Nyota Nyekundu ilivyocheza dhidi ya Simba. Palikuwa hapatoshi.
KAMA ULAYA
Kama timu hizo zingekuwa na nguvu ileile hadi leo hii (Pan bado inajikongoja lakini Nyota Nyekundu imeshajifia), soka la Tanzania lingepiga hatua kubwa. Ni kama vile FC Barcelona mbali na kuwa na upinzani na Real Madrid katika dabi ya El Clasico, pia ina upinzani mkali na Espanyol (Barcelona Derby, Espanyol imeshuka daraja), huku Real Madrid pia ikiwa na dabi ya Madrid dhidi ya Atletico Madrid (Madrid Derby). Hata England, Manchester United nyumbani ina upinzani na Manchester City lakini kwenye ligi ina upinzani na Liverpool, ambayo nayo ina upinzani mkali na Everton katika Merseyside Derby.
Na hata Tanga kulikuwa na Coastal Union na Africans Sports kisha zikawa zinakutakana na Simba na Yanga kwenye ligi, soka lilipigwa. Unadhani kama timu hizi zingekuwepo na upinzani uleule na kuongezeka na hizi Azam FC kuna timu ingechukua taji la Ligi Kuu mara 29 au 22 mpaka leo hii? Thubutu.
PAN, NYOTA NYEKUNDU
Kwa hiyo kukosekana kwa timu hizo kumezifanya Simba na Yanga kukosa upinzani wa kweli. Kuna timu zilijaribu kujenga upinzani dhidi ya Simba na Yanga lakini hazikudumu kwa miaka mingi. Kulikuwa na Pamba ya Mwanza, Mwadui (ilee sio hii ya juzi), Reli ya Morogoro, CDA ya Dodoma, Ushirika Moshi na Majimaji ya Songea (sio hii ya juzi) naamini kama zingekuwa na uwekezaji mkubwa tungekuwa tunazungumza vitu tofauti.
AZAM NA SINGIDA BIG STARS
Bado hazitoi ushindani unaostahiki kwa Simba na Yanga kwani kila siku tunatarajia taji la Ligi Kuu litatua Kariakoo. Inadaiwa tatizo kubwa la klabu za sasa zinakamia zaidi. Ni kama zilivyokuwa Mbeya City na Tanzania Prisons zinazikamia zaidi Simba na Yanga huku zikipoteza kirahisi na timu zenye hadhi zao. Naamini kabisa, Simba na Yanga zinafurahia ‘vifo’ vya Pan na Nyota Nyekundu kwasababu zingepata tabu sana kugawana ubingwa wa Tanzania Bara.