Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 60 ya mataji, anguko la Small Simba

HAIPO tena kwenye Ligi Kuu Zanzibar, timu iliyobeba mataji mara saba, Small Simba imepotea kwenye ramani ya ushindani wa soka hivi sasa.

Wakati Wazanzibar wakihesabu siku kusherehekea kumbukumbu ya Miaka 60 ya Mapinduzi, anguko la Small Simba nalo linaingia kwenye vichwa vya wengi kutokana na historia na rekodi yake katika soka la visiwa hivyo.

Muasisi na mwanzilishi wa timu hiyo, Abdul Ghani Msoma anaeleza ilivyoanzishwa rasmi mwaka 1972, akimtaja kocha maarufu viswani humo, Masoud ambaye wakati huo alikuwa mchezaji wa Kikwajuni aliyeamua kuwakusanya vijana na kuwaendeleza kisoka.

“Zanzibar miaka mitatu hadi minne hivi baada ya Mapinduzi wale waliokuwa wakishughulikia mpira wa watoto ni kama waliachana nao, hiyo ilikuwa ni kati ya 1966 na 1967.

“Nakumbuka baada ya pale, tukawa tunaratibu wenyewe kikombe tunashindana kukiwania, hakukuwa na ushindani mwingine, tulikuwa tunaweka tu vikombe tunacheza wenyewe kwa wenyewe mtaani.

“Vilikuwa ni vikombe fulani vidogo hata vile vya chai ni vikubwa, hivi tulipewa na Wajerumani wa Mashariki, hivyo tukawa tunavitumia kwenye mashindano ya mtaa tunawania,” anasema.

Anasema Maalim, Rajabu Mzee aliyekuwa mwalimu wa skuli, alianza kurudisha uhai wa kusimamia mpira wa watoto, kuanzia mwaka 1968 kabla ya kocha Masoud kuanza kuwafundisha vijana hao wakati huo yeye na Masoud wakicheza Kikwajuni.


SMALL SIMBA NA UNDUGU NA SIMBA

Anasema mwaka 1969 klabu ya Kikwajuni ilitembelewa na Mwenyekiti wa Sunderland (sasa Simba SC ya Dar es Salaam) aliyemtaja kwa jina la Chimwaga, ambaye pale klabuni aliona picha ya vijana na kuuliza ni timu gani, akaambiwa ni watoto ambao wanafundishwa pale.

“Aliomba waitwe Small Sunderland, kipindi hicho Kikwajuni Sports Club na Sunderland (Simba SC) walikuwa na undugu wa kisoka, na kabla ya matembezi ya kiongozi huyo, ndizo klabu zilizoanzisha matembezi ya Pasaka mwaka 1953.

“Japo sasa maendeleo yao ni tofauti moja ni kubwa katika soka la Tanzania na nyingine imeshuka, lakini ni timu ndugu, walianzisha kwa pamoja mashidano ya Pasaka.

“Undugu wao ulianza mwaka 1952, walianza Kikwajuni kupeleka barua Sunderland (Simba) kuomba kuitembea klabu hiyo siku ya Pasaka, wakakubaliwa na kuitwa Dar es Salaam.

“Waliondoka Unguja watu wa Kikwajuni kwa bashasha kwenda kuitembelea Sunderland, pale ndipo undugu wao ulianzia hivyo hata Mwenyekiti wa Sunderland alipotaka watoto waliokuwa wakilelewa Kikwajuni kuitwa Small Sunderland hilo lilipitishwa,” anasema.

Anasema mwaka 1970, iliundwa timu ya Navy ambayo sasa inafahamika kama KMKM ambayo iliwachukua karibu wachezaji wote wa Kikwajuni.

“Kikwajuni ilipwaya, ikalazimika kuwachukua vijana wa Small Sunderland kuitumikia, bado hakukuwa na mtu anayeshughulika na watoto, walipelekwa tu.

“Masoud hakutaka timu ya Small Sunderland ife, alitafuta vijana wengine na kuendelea kuwafundisha, nilijiunga naye baadaye lakini tukiwa wachezaji wa Kikwajuni wakati huo,” anasema.


RAIS KARUME ATAJWA

Msoma anasema mwaka 1971 Rais wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume alipokwenda Msimbazi kufungua jengo la klabu ya Sunderland ndipo na jina la Small Sunderland lilipobadilika.

“Nilikuwepo katika hafla ile, Rais alitoa laki mbili unusu (Sh 250,000), nikiwa miongoni mwa wachezaji tulioalikwa kushuhudia hafla ile, Rais alisema Sunderland itoe jina la Kiulaya iitwe Simba, Zanzibar pia Masoud alibadilisha jina la Small Sunderland na kuuita Small Simba.

“Hakumshirikisha mtu yeyote, alifanya yeye kama yeye kwa kuwa wakati huo ndiye mtu aliyekuwa amejitoa kwenye soka la watoto visiwani hapa.”


YAANZA KUBEBA MATAJI

Msoma anasema mwaka 1975 aliungana na Masoud kuwanoa vijana hao, na mwaka mmoja baadaye ilianzishwa ligi ya vijana ambao timu hiyo ilishiriki.

“Mwaka 1977  ligi hiyo ilibadilishwa jina na kuitwa Central Ligi, ambayo ilisimamiwa kwa karibu na Maalim Rajabu akiwashirikisha yeye Msoma, Masoud, Hafidh Badru na wengine wengi,” anasema Msoma ambaye sasa ana umri wa miaka 73 akiwa anaendelea na soka lakini sasa akiinoa klabu kongwe ya Malindi.

“Wakati huo naingia kushirikiana na Masoud, tayari nilishapata ajira, hivyo kidogo nilikuwa na mfuko (pesa) mshahara wangu nilipokea Sh1,050 kwa mwezi ambayo ilikuwa ni pesa nyingi sana, tukaanza kunyanyua vijana, Small Simba ikaanza kuwa tiishio.

“Mwaka 1981 tukaingia daraja la pili kutoka kwenye Central Ligi, tukachukua ubingwa, 1983 tukaingia daraja la kwanza na mwaka huo huo tukawa mabingwa wa Zanzibar.”

Anasema kwenye mashindano ya Super League, Small Simba ilikuwa gumzo ilipoichapa Yanga bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan.

“Kuanzia hapo timu ikawa inatikisa, tulishinda ubingwa wa Zanzibar mara saba, tumekuwa wa tatu Afrika Mashariki mara mbili, na kuwa klabu bora nchini.

“Hatukuwahi kuchukua ubingwa wa Afrika Mashariki, lakini kwenye tatu bora tumeingia mara mbili, kwenye Super League tumekuwa wa pili mara tatu na kuiwakilisha Tanzania mara tatu, wakati ule nilikuwa na mapenzi na soka, nilitumia mali yangu yote, mshahara wangu na nilichelewa hadi kuoa sababu ya soka.”


FEDHA ILIUA TIMU

Msoma anasema Machi 17, 1996 ni siku ambayo itabaki kwenye kumbukumbu ya maisha yake ya mpira miaka yote baada ya kutimuliwa kwenye klabu hiyo na watu aliowakaribisha mwenyewe.

“Niliondoka nikawaambia, kama kweli mimi na Masoud ndiyo waanzilishi na waasisi wa hii timu, lakini leo hii mnatufukuza sababu ya pesa, basi haitafika popote,” anasema.

Akisimulia tukio hilo, Msoma anasema baada ya kuifunga Yanga, Small Simba ilianza kuwa tishio na kupata mashabiki huku mechi zake dhidi ya timu hiyo kongwe ya Bara na ile ya Simba zikiingiza mamilioni.

“Tulikuwa tukicheza na Simba mapato ya mlangoni ni Sh30 milioni, tukicheza na Yanga ni Sh40 milioni ambazo kwa wakati huo ni pesa nyingi sana, hapo ndipo fitina ilipoanzia, wakaingia watu ambao walidiriki hadi kunifukuza kwenye timu, tena wengine nikiwa nimewakaribisha mwenyewe.”

Anasema, yeye na Masoud utaratibu wao wakishinda mechi, pesa zote za mapato waligawana wachezaji, jambo ambalo anadai liliwakera baadhi ya viongozi.

“Walinifanyia fitina hadi wakanifukuza, nakumbuka wakati ule nilikuwa nimenunua nyumba ambayo niliifanya kuwa jengo la klabu, niliondoka nikawaachia ila niliwaambia naondoka kwenye timu, lakini ubingwa pia kwa Small Simba mtahusikia hadi leo timu imekufa,” anasema.


ANGUKO LAKE LAANZA

Anasema 1997 hadi 1998 timu hiyo ilijaribu kupambana kwenye Ligi ya Zanzibar lakini ilishindwa kurudi kwenye kasi ya mwanzo na kuanza kuporomoka polepole hadi sasa haipo tena katika Ligi.

“Nilipoondoka nikawaacha viongozi wale ambao waliongoza klabu kwa miaka minane, timu iliyumba na kupotea kwenye ramani ya Ligi ya Zanzibar, hivi sasa mimi na Masoud tumerudi tena kuanzisha akademia ya soka ya Small Simba, lakini timu kama timu ya ligi haipo.”

“Tunashukuru ni Serikali kuboresha viwanja vya Gombani (Pemba) na Amaan (Unguja) vinaongeza hamasa kwetu.”