Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MHALWIKE: Kutoka gofu ya kuondoa uchovu hadi kubeba mataji

GOFU Pict

Muktasari:

  • Katika mahojiano na Mwanaspoti, Mhalwike anasema alianza kucheza gofu 2022 baada ya kuvutiwa na marafiki zake aliokuwa anawasindikiza kucheza katika viwanja vya Lugalo.

MCHEZAJI wa ridhaa wa gofu, Onesphory Mhalwike kutoka klabu ya Lugalo anasimulia alivyoanza kucheza mchezo huo ambao hakuwahi kufikiria kwamba ungeweza kumpa manufaa makubwa anayoyapata kwa sasa.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Mhalwike anasema alianza kucheza gofu 2022 baada ya kuvutiwa na marafiki zake aliokuwa anawasindikiza kucheza katika viwanja vya Lugalo.

Mchezaji huyo mwanajeshi, anasimulia kitendo cha kuwasindikiza marafiki zake alikichukulia kama moja ya njia ya kupumzisha akili yake baada ya majukumu  na kuingiza vitu vipya katika kichwani, lakini mwisho wa siku akaambulia kuupenda mchezo huo na hatamani kuachana nao.

“Awali nilikuwa napenda mandhari ya viwanja ile miti mingi walivyokuwa wanatembea kwa muda mrefu. Ni mchezo ambao haubagui mkubwa, mdogo, tajiri ama maskini - wachezaji wakiwa viwanjani wana usawa, hivyo vitu vikaanza kuniingia kichwani,” anasema.

GOF 01

FAIDA ZA GOFU

Mhalwike anazitaja faida za gofu kuwa umesaidia kumtengenezea koneksheni na watu na miongoni mwao anafanya nao biashara na kumpa ushauri wa namna ya kujenga maisha yake kuwa na nguvu kiuchumi.

“Nafanya biashara ya vyombo vya ndani, mashuka na pazia ninavyoviagiza nchini China. Kabla ya koneksheni na watu hao sikuwahi kuwaza uthubutu wa namna hiyo, hivyo ni kitu kikubwa sana nilichokipata katika mchezo huo,” anasema Mhalwike mwenye handcup tano (kiwango cha uchezaji).

Kutokana na mafanikio anayoyapata kupitia mchezo huo, anawashauri vijana kujifunza akiamini gofu itawapa hatua za kimaisha na kuwakutanisha na watu wa ndoto zao kuliko kushinda vijiweni na kuamini vitu haviwezekani.

“Wakati mwingine vijiweni tunadanganyana sana. Mfano mchezo huu unakukutanisha na viongozi katika nyanja tofauti na wafanyabiashara. Hao wanazungumza maisha na siyo vitu ambavyo havina kichwa wala miguu ama stori za kusadikika,” anasema na kuongeza:

“Gofu una viwanja 18 ambavyo ukivimaliza ni kama umetembea saa tatu. Unapopiga mpira (kuswimu) unatumia nguvu. Kutembea kwa muda mrefu ni mazoezi tosha ya mwili, hapo unakuwa umeshauriwa vitu vya maana na watu waliofanikiwa. Inakuwa ni ngumu kwenda kuvifanya vitu vya hovyo badala yake utalazimika kwenda kupumzika.”

Mhalwike anasema asilimia kubwa ya wachezaji wa gofu, miili yao ipo fiti.

“Ngumu kumkuta mchezaji wa gofu ana mwili usiojengeka kimazoezi ama kulalamika miguu (inauma), wapo fiti kwani ni mchezo unaokulazimisha mazoezi.”

GOF 02

NYUMA YA GEMU

Mhalwike anasema wanafanya ‘mchezo wa gemu’ kwa kuchangishana pesa, kisha wanaanza kushindana kwa kucheza gofu na anayeshinda anaondoka na kibunda cha pesa. “Nashinda mara nyingi huo mchezo wa gemu. Mfano juzi tulikuwa sita tukachanga Sh 40,000 nikashinda nikaondoka na pesa. Kwa wiki tunaweza tukacheza mara tatu hadi nne. Kuna wakati tunachanga Sh50,000 hadi Sh100,000 zikiwa pesa ndefu mfano tukawa 10 basi watapewa kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa tatu,” anasema na kuongeza:

‘Mfano kwa wiki mtu unapata Sh500,000 kwa mwezi unaweza ukapata Sh2 milioni je hujaongeza mtaji katika biashara zako ama kuwasaidia wazazi wako waliopo mkoani? Hivyo huo mchezo unatusaidia kiuchumi. Pia unatujengea ushindani na umakini na inapotokea mashindano rasmi tunakuwa tumeiva.”


NDOTO

Bado Mhalwike hajafanikiwa kuanza kucheza mashindano ya kimataifa, hivyo ndoto yake kubwa ni kujulikana duniani kupitia mchezo huo.

“Nina mataji zaidi ya matano nisingekuwa natingwa na ratiba za majukumu yangu ya kazi (mwanajeshi) ningekuwa na mataji mengi zaidi na huenda hilo ndilo limechelewesha kupata nafasi ya kucheza mashindano mbalimbali ya kimataifa maana muda mwingi nasafiri,” anasema.


ISIAHAKA MTU SANA

Mhalwike Anasema katika mchezo huo kwa hapa Tanzania anamkubali  Isihaka Daudi kutokana na mbinu, uzoefu na anaujua zaidi huo mchezo kwa sababu alianza kucheza akiwa mdogo.

“Ameanza kucheza tangu akiwa mdogo, hivyo anazijua zaidi sheria za mchezo huo na kuvisoma viwanja na namna ya kukabiliana navyo. Ndiyo maana anakuwa tishio katika mashindano mbalimbali,” anasema.

“Najifunza vitu vingi kutoka kwake amewahi kuhusika na ushindi wangu wa mashindano ya Morogoro Open kwa kundi ka division A. Tukiwa viwanja vya Lugalo alinisaidia sana katika mazoezi.

“Tukasafiri naye kwenda Morogoro akaangalia viwanja akaniambia kwa aina  viwanja vilivyo, akanipa mbinu ya kucheza na akasema ukizingatia utapata taji. Nikazingatia nikapata taji. Jamaa ana kipaji kikubwa na uelewa mkubwa na mchezo huo na ingekuwa anaonyesha uwezo huo katika mpira wa miguu angekuwa anaimbwa kila kona.”

GOF 03

GOFU NI UMAKINI

Mchezaji huyo anasema kwa aina ya mipira inayotumika kuchezea gofu wakati wa kupiga inahitajika umakini na siyo kwenda tofauti na utaratibu.

“Hivi karibuni tulikuwa watatu tunacheza sehemu fulani hivi mwenzetu mmoja akashenki (kwenda tofauti na utaratibu). Kimpira alichokipiga kikamkuta dada mmoja mkononi alilia sana. Akapewa huduma ya kwanza na kukimbizwa hospitali. Ingempiga maeneo mengine huenda tungeongea kitu kingine. Mchezo wa gofu ni hesabu na umakini,” anasema Mhalwike anayekiri zawadi kubwa aliyowahi kupewa ni rininga inchi 53.

Mbali na hilo anasema mwanawe Greyson mwenye umri wa miaka minne namna anavyoupenda mchezo huo ameanza kumfundisha kucheza: “Naenda naye viwanjani nina mpango wa kumnunulia fimbo za watoto, mfano nikirudi nyumbani anafungua begi na kuchukua vimpira na mwiko anaanza kupiga basi ndani panakuwa pamegeuzwa viwanja vya gofu.”