MGOGORO WA YANGA: Wachezaji 14 wafukuzwa Yanga

Katika sehemu hii ya mwisho ya 10 ya mfululizo wa makala za mgogoro mkubwa uliowahi kuikumba klabu ya Yanga, leo tunahitimisha na wachezaji kutimuliwa ndani ya klabu hiyo na Pan Afrika kuanzishwa... Endelea


KATIBU Mkuu wa Yanga, Mohamed Missanga alitangaza kuwafukuza wachezaji wote 21 wa klabu hiyo walioshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kule Mombasa, Kenya. Missanga alisema uongozi wao utaendelea kuheshimu mikataba iliyoingiwa na viongozi waliopita ukiwemo ule wa Kocha Tambwe Leya.

Wachezaji waliofukuzwa ni Patrick Nyaga, Juma Pondamali ‘Mensah’, Juma Shaban, Selemani Said, Jellah Mtagwa, Leodger Tenga, Omari Kapera, Ezekel Greyson, Sunday na Kitwana Manara.

Wengine ni Gibson Sembuli, Ahmed, Muhaji Muki, Ufunguo, Ramadhani Mwinda, Sam Kampambe, Juma Matokeo, Selemani Jongo, Ali Yusuf na Boi Idd Weckens.


OFISI YA TAMBWE YAVUNJWA

Kocha Msaidizi wa Yanga, Athuman Kilambo naye amesimamishwa kutokana na kudaiwa kuhusuka katika uvunjaji wa ofisi ya Kocha Tambwe Leya.

Mbali na Kilambo, wengine waliodaiwa kuhusika katika tukio hilo la Desemba 10, 1975 ni wachezaji Himid, Omari Kapera na dereva wa klabu hiyo, Sixmund Komba. Mbali na kuvunjwa kwa ofisi hiyo inadaiwa vifaa mbalimbali vya thamani viliibiwa vikiwemo medali za kocha huyo yenye thamani ya Sh 1,750 vifaa vyake binafsi na vingine vya klabu. Kesi hiyo iliachwa chini ya upelelezi wa polisi.


SABA TU WARUDI

Katibu Mkuu wa Yanga, Missanga alitangaza kuwarudisha baadhi ya wachezaji waliofukuzwa ambao ni kina Mwinda, Ezekel, Selemani Said, Twaha, Ufunguo, Selemani Jongo na Ahmad.

Pia, mchezaji Moshi Dayan pamoja na kutokuwepo katika wachezaji walishiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati naye alikubaliwa kujaza fomu na kujiunga na wachezaji hao.


TAMBWE ATIMULIWA NCHINI

Februari 1976, Serikali chini ya Waziri wa Utamaduni wa Taifa na Vijana, Mrisho Sarakikya ilitangaza kuwafukuza makocha wa kigeni wanaofundisha soka Tanzania. Pia, Waziri Sarakikya alitangaza kupiga marufuku klabu yoyote kuagiza kocha kutoka nje ya nchi. Kutokana na amri hiyo, Makocha Naby Kamara wa Simba aliyetokea Guinea na Tambwe Leya wa Yanga aliyetokea Zaire (sasa DR Congo) walilazimika kuondoka nchini.


WACHEZAJI WAOMBA RADHI

Wachezaji takribani 14 wa Yanga waliofukuzwa waliandika barua ya kuomba radhi na kutaka kurudishwa kundini kuitumikia klabu hiyo lakini uongozi wa klabu hiyo ulikataa ombi hilo.

Barua hiyo ilitiwa saini na wachezaji wote isipokuwa Nyaga na Wickens ambao tayari walishaanza kuitumikia timu ya Mseto ya Morogoro.


WAJIUNGA NA NYOTA AFRIKA

Baada ya msamaha wao kukataliwa wachezaji hao walijiunga na Nyota Afrika ya Morogoro. Kasoro wachezaji Juma Nassor ‘Mensah’, Mohamed Rishard ‘Adolf’, Jaffar Abdulrahaman, Mohammed Yahya ‘Tostao’ na Gordian Mapango ambao walijiunga na Breweries ya Dar es Salaam.

Kitendo cha Nyota Afrika kuwapokea wachezaji hao kiliingiza klabu hiyo katika mgogoro na Yanga kwa kuwa zilikuwa na uhusiano wa karibu sana. Viongozi wa Yanga waliona kama wamesalitiwa na wenzao hao.


NYOTA AFRIKA MATATANI

Baada ya kuwapokea wachezaji hao na kuwachezesha katika Ligi ya Wilaya ya Morogoro, klabu ya Nyota Afrika ilijiingiza katika matatizo makubwa. Viongozi wa soka wa Morogoro waliichukulia hatua timu hiyo baada ya kuinyanyang’anya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mapinduzi kufuatia kuwachezesha wachezaji hao. Baada ya msuguano mrefu hatimaye wachezaji hao waliruhusiwa kuitumikia timu hiyo.


PAN AFRIKA YAANZISHWA

Agosti 1976 Klabu ya Pan Afrika ilisajiliwa Wilaya ya Ilala baada ya kukubaliwa usajili. Awali kulikuwa na pingamizi la kusajiliwa kwa klabu mpya ambalo liliwekwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa zamani wa Yanga walikuwa wakihaha kutaka kuanzisha klabu yao.

Hatimaye, viongozi hao walikwenda kuzungumza na klabu ya Zamalik (Zama za Kale) ya Upanga jijini Dar es Salaam iliyokuwa timu ya maveterani waliokuwa wakifanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya zao.

Wachezaji wa kwanza waliounda Pan Afrika ni pamoja na kipa wa zamani wa Simba, Athumani Mambosasa.

Mambosasa alijiunga na Pan akitokea Nyota Afrika kwa kuwa lengo lake la kwanza ni kutoka Simba na kujiunga na Yanga. Hivyo akaondoka na wachezaji hao kwenda nao Morogoro. Wengine ni Ali Yusuf, Boi Idd Weckens, Nondo, Mikidadi, Muhaji Muki, Omari Kapera na Kitwana Manara. Pia, walikuwepo kina Juma Matokeo, Leodger Tenga, Juma Shaban, Gibson Sembuli, Jellah Mtagwa, Sunday Manara na Mohamed Migea. Wengine ni Zakaria Digosi, Idd Said China, Kivera James, Idd Sululu na Said Juma. Pia, kina Mohamed Hussein, Michael Mapunda, Ahmed Johari, Hassan Mohamed Mwangi, Kassim Manara, Adolf, Mohamed Tostao, Gordian Mapango, Jaffar Abdulrahaman, Mohammed Mkweche, Juma Nassoro Pondamali ‘Mensah; na Haruna Hemed. Awali Pan ilihifadhiwa na Kikundi cha Taarab cha Egyptian Mtaa wa Swahili na Mkunguni na baadaye kumiliki Jengo lake Mtaa wa Swahili na Mafia Kariakoo, Dar es Salaam. Mwisho.