MGAYA: Kutoka uarabuni hadi Ligi Kuu Bara

Muktasari:
- Nyota huyo alijiunga na Wagosi wa Kaya wakati wa dirisha dogo la usajili akitokea FleetWoods Falme za Uarabu, UAE alikocheza kwa misimu miwili.
WAKATI mwingine unapokumbana na changamoto inapaswa kuigeuza kuwa fursa.Ndivyo anavyosema mshambuliaji wa Coastal Union, Mgaya Ally.
Nyota huyo alijiunga na Wagosi wa Kaya wakati wa dirisha dogo la usajili akitokea FleetWoods Falme za Uarabu, UAE alikocheza kwa misimu miwili.
Wakati alipokuwa kwenye timu hiyo iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Pili UAE alikumbana na changamoto ya kubaguliwa lakini hakukata tamaa na kuigeuza kuwa fursa.
“Sio jambo geni wengi wamekutana na changamoto hii, Ulaya inatokea sana wachezaji kama Vinicus Jr., Mohamed Salah wamekuwa wakikumbana na janga hilo kwahiyo nilipambana sana,” anasema Mgaya.
Mshambuliaji huyo kabla ya kutimkia Uarabuni aliwahi kuichezea Coastal Union ya vijana msimu 2020/21.
Misimu miwili aliyoichezea FleetWoods aliweka kambani mabao 20 yaliyowafanya waliombagua kubadili mitazamo yao.
KILICHOMKUTA UARABUNI
Anasema msimu wake wa kwanza kuichezea FleetWoods alikumbana na changamoto ya ubaguzi wa rangi kwenye timu hiyo.
“Wachezaji wengi kutoka nje wanapokuja Bongo wengi wanabaki kwa sababu Tanzania ni nchi yenye amani na watu wake wana upendo sana tofauti na nchi nyingine kama Uarabuni.
“Nilikumbana na ishu ya kubaguliwa unajua tena ngozi nyeusi, muda mwingine nanyimwa pasi uwanjani lakini nilipambana sana kuhakikisha siingii kwenye mtego wao.
“Kilichotokea nikawa nawapuuza nikipata pasi basi nahakikisha nakiwasha kweli kweli ikafika kipindi sasa wakanikubali wenyewe.
“Nashukuru Mungu nilipambana sikukata tamaa, maana ishu kama hiyo wengine wanatoka mchezoni nilihakikisha namuaminisha kocha mazoezini hadi wakanikubali.”
SABABU YA KURUDI BONGO
Straika huko dirisha dogo alikuwa na ofa tatu kutoka ligi mbalimbali Oman, Kazakhstan na Jordan lakini alirejea bongo na kujiunga na Coastal Union.
Mgaya anasema ukiachana na ofa za timu hizo pia alikuwa na ofa kutoka Ligi Daraja la Pili nchini Hispania.
“Nilipata dili kubwa la kucheza Ligi Daraja la Pili Hispania na ilikuwa ili nicheze basi lazima niwe angalau nimecheza Ligi Kuu kutoka nchi yangu,” anasema na kuongeza
“Nikaona nirudi Bongo na kutafuta timu wakati huo nilikuwa nawaniwa na Kagera Sugar nikaona kuna vitu haviendi nikaamua kurudi Coastal ambao walikuwa siriazi na dili hilo.
“Dili la Hispania limenipa somo ningecheza hata nchi nyingine lakini huenda nikapata dili jingine tena kubwa kwahiyo nikaona nicheze japo msimu mmoja ili ikitokea nijulikane tayari nilicheza.”
Nyota huyo alimaliza mkataba wa miaka miwili hivi karibuni na Fleetwoods ya Falme za Kiarabu.
MALENGO YAKE
Mgaya anasema kila mchezaji ana malengo yake kwake anatamani siku moja kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars.
“Natamani nicheze Ligi kubwa duniani hiyo ni ndoto nafikiri ya kila mchezaji wa mpira, Mbwana Samatta ni miongoni mwa wachezaji ninaowatazama sana amekuwa kwenye soka kwa muda mrefu,” anasema na kuongeza:
“Sijawahi kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, kwangu natamani na mimi nilitumikie taifa langu hayo ni malengo yangu makubwa.”
NAFASI YAKE
Tangu atue Coastal Union dirisha dogo, nyota huyo hajacheza mchezo wowote wa Ligi Kuu na Kombe la ASFC ambapo Coastal iliondoshwa kwa mabao 3-1 na Yanga katika hatua ya 32 bora.
Akizungumzia nafasi yake ndani ya kikosi cha Wagosi wa Kaya, Mgaya anaamini muda wake wa kucheza bado haujafika akivuta subira ipo siku atacheza.
“Kila kocha ana matakwa yake amtumie nani kwa wakati gani naamini muda bado upo wa kucheza na kuonyesha kiwango changu na kuisadia timu yangu,” anasema.
“Kocha Mwambusi anaamini kwenye soka la vijana ili upate nafasi unapaswa kukazana sana mazoezini ili upewe mechi isitoshe eneo ninalocheza lina ushindani mkubwa sana wa namba, lakini nakomaa.”