Mchezaji anahitaji kuwa na vitu hivi

Muktasari:
- Wahenga walisema mpira unadunda. Pamoja na timu zote hizo kuwa katika nne za juu EPL, lakini msimu huu makali ya Manchester City yamepungua.
JUMAPILI ilikuwa burudani kwa wapenzi wa soka waliposhuhudia mechi kali ya Ligi Kuu England wakati Arsenal ikiifunga Manchester City mabao 5-1.
Wahenga walisema mpira unadunda. Pamoja na timu zote hizo kuwa katika nne za juu EPL, lakini msimu huu makali ya Manchester City yamepungua.
Arsenal inaonekana kuwa bora zaidi ikishika nafasi ya pili ikitumia wachezaji wa bei ya wastani huku pia ikiwapa nafasi makinda wenye uwezo.
Taaluma ya sayansi ya michezo na nyinginezo ndizo zinawezesha kupata wachezaji wenye uwezo mkubwa wangali na umri mdogo kama ilivyo kinda wa Arsenal mwenye miaka 18, Myles Lewis Skelly.
Timu imara lazima iwe na ukamilifu wa idara zote ikiwamo benchi la ufundi, jopo la madaktari na makocha wa mazoezi ya viungo.
Kufanikiwa kwa mchezaji kunahitaji kushikamana na kanuni kuu tatu ambazo ni kula mlo sahihi ukizingatia milo ya wachezaji, mazoezi na mafunzo na mwisho ni kupumzika na kulala.
Mambo hayo ndio yanayowafanya wanasoka wengi wa kulipwa kufanikiwa kucheza kwa kiwango wakiwa timamu kimwili na kudumu katika medani ya soka kwa muda mrefu.
Mchezaji kucheza kwa kiwango na kuifikisha timu katika mafanikio ni utimamu wa afya ya mwili ambapo ndani yake huwa na vitu vifuatavyo:
KASI
Miaka ya 1990 hapa nchini kulikuwa na winga maarufu Edibily Lunyamila aliyekuwa na kasi ya juu kuwazidi mabeki.
Wanasoka wote wanahitaji kuwa na kasi uwanjani na kadri mchezaji anavyokuwa na kasi ndivyo pia anavyocheza vizuri, ingawa kasi ya mpira wa miguu ni tofauti na michezo mingine.
Mara kwa mara mwanasoka anahitaji kukimbia na mpira, kukimbia kawaida au kufunguka kwa kasi yenye nguvu.
Mara nyingi kasi huhitajika mahala pasipotarajiwa, mfano mchezaji anaweza kuwa anakimbia kidogo kidogo lakini anaponyakua mpira anaweza kufunguka kwa kasi ili ashambulie.
Vilevile mchezaji anayekaba atahitajika kufunguka ghafla kwa kasi ili kumzuia mshambuliaji ambaye si rahisi kupata ikiwa hana kasi.
Hivyo ni kawaida kumuona mcheza soka mara kwa mara kukumbana na mbio fupi fupi za kasi ambazo zinahitaji atumie nguvu kubwa kuweza kufanya hivyo.
Kasi ya mwanasoka inajengwa kwa mazoezi tangu akiwa kinda anahitajika kutunza uwezo wake wa kuwa na kasi kwa kuzingatia programu nzima ya mazoezi anayopewa na wakufunzi.
Mazoezi ya kujenga kasi huwa na muda maalumu, umbali na mtindo wake.
UKAKAMAVU NA STAMINA
Soka ni mchezo mgumu unaohitaji mwili mkakamavu ili kuweza kustahimili mikikimikiki na kucheza kwa ushindani katika mazingira magumu ya kimchezo.
Unapokuwa na mwili mkakamavu ina maana ni mwili ambao unaweza kudumu na kuvumilia mambo mengi ikiwamo kutopata majeraha ya mara kwa mara.
Vilevile mchezaji mkakamavu huweza kudumu na mwili na kiwango chake kwa muda mrefu zaidi.
Misuli ya mchezaji mkakamavu hujengeka kimazoezi au kwa neno lilizoeleka sana ‘stamina’. Neno hili sio geni kwa wanamichezo.
Stamina ni uwezo aliojifunza mtu kutokana na mafunzo na kuzoeleka ukijengeka katika ubongo na mwili.
Baadaye mwili ukaweza kujijenga na kufanya mambo kwa vitendo vyenye kuonyesha uwezo mkubwa wa kutenda na hivyo mtu akautumia mara kwa mara kwa kiwango kinachotakiwa muda mrefu.
Hivyo tunapata picha kuwa stamina ni mchanganyiko wa uwezo wa mwili pamoja na ukakamavu wake kuweza kudumu kwa muda mrefu bila kuchoka katika mazingira magumu ya mwili ikiwemo kucheza mechi nyingi kwa kiwango cha juu.
Misuli inapojengwa kwa mazoezi akili nayo inajifunza hayo mazoezi na aina ya mafunzo ya mchezo husika. Ili kuwa na stamina nzuri ni lazima kuwe na ushirikiano wa hali ya juu wa ubongo na viungo.
Ukakamavu wa mwili huweza kujengwa kwa mazoezi mbalimbali ikiwamo yale ya viungo, gym - kama kunyanyua vitu vizito, mazoezi ya uchezaji soka, mbio na kuogelea.
WEPESI NA KUNYUMBULIKA
Mchezaji anahitajika kuwa na uzito wa wastani kwa sababu uzito uliokithiri humfanya kutokuwa mwepesi kucheza. Kunyumbulika ni uwezo wa kubadilika kwa wakati pale inapohitajika kuendana na majukumu. Mpira unahitaji kuucheza kwa kasi na huku ukihitaji kubadilika ukiwa katika kasi.
Wepesi na kunyumbulika mchezaji kunategemeana na wataalamu wa benchi la ufundi na juhudi za mchezaji kufanya mazoezi ya viungo na kulainisha viungo.
NGUVU NA UIMARA
Kiungo mkabaji wa klabu ya soka ambaye ndio anahitajika kuwepo kila mahali katika maeneo mengi uwanjani akikaba, kupokonya mpira, kutoa pasi na kushambulia.
Kasi yake na kukimbia kila mahali bila kuchoka na kuwakaba wapinzani katika mechi zote alizocheza, bila kuwa na nguvu ni vigumu kucheza. Utimamu wa mwili wa mchezaji mwenye ukakamavu na kasi huitaji kuwa na misuli yenye nguvu ili kuweza kutekeleza majukumu ya uwanjani.
Nguvu ya mchezaji inajengwa kwa lishe maalumu na mazoezi ya kuimarisha na kujenga misuli. Misuli inakunjuka na kujikunja kwa kutumia nishati tunayoipata katika vyakula.
Mwanasoka hushauriwa kula vyakula vya kumpa nguvu na kujenga mwili yaani protini pasipo kuathiri uzito wa mwili. Lishe inajenga mwili na kuupa uzito wa wastani ambao unahitajika kuweza kukabiliana na mikiki ya soka.
Ikumbukwe kuwa mchezo wa soka anahitaji uzito wa wastani kwani uzito mkubwa zaidi unasababisha kutokuwa na kasi au kuwa mvivu. Mara nyingi uzito wa wanasoka wa kimataifa huwa ni kati ya kilo 65-80.
Hivyo pamoja na kula vyakula mbalimbali mchezaji anahitaji kutunza uzito wake ili usipungue sana wala kuongezeka sana.
Ili kuweza kuwa na nguvu yenye ufanisi kujenga mwili imara wenye afya wachezaji hupumzika na kulala muda mwingi kwa kawaida ni saa 6-8 kwa siku. Lengo ni kutoa nafasi kwa mwili kujijenga, kujisahihisha, kuondoa uchovu na kupata utulivu wa kimwili na kiakili.
Ubora wa afya ya akili kwa mchezo ni jambo muhimu ili kuweza kuwa na maamuzi sahihi anapokuwa uwanjani. Vitu vyote hivyo vinaratibiwa na ubongo.