Mayweather aambiwa, 'mbona ungechapwa'

Muktasari:
- Bingwa wa zamani wa dunia, James Toney amesema Chavez angetoa kichapo kwa Mayweather kama wangekutana wakiwa katika viwango vya juu.
NEW YORK, MAREKANI: BONDIA asiyepigika Floyd Mayweather ameambiwa mapambano yote 50 aliyocheza bila kupoteza ni lazima angepoteza iwapo angezichapa na mkali wa masumbwi wa Mexico, Julio Cesar Chavez.
Bingwa wa zamani wa dunia, James Toney amesema Chavez angetoa kichapo kwa Mayweather kama wangekutana wakiwa katika viwango vya juu.
Mayweather alistaafu akiwa na rekodi bora kabisa katika historia ya ngumi za kulipwa ushindi katika mapambano yote 50.

Nyota huyo wa Marekani anayejulikana pia kama 'Mr Money' amewahi kukabiliana na wakali kama Manny Pacquiao, Oscar De La Hoya na Canelo Alvarez ambao wote walijaribu kumshinda bila mafanikio.
Lakini, mijadala imeendelea kwa miaka mingi kuhusu iwapo mabondia wa zamani au wa sasa wangeweza kuvunja mfululizo wake wa kutoshindwa.

Kuna wakati promota maarufu wa ngumi za uzito wa juu duniani, Bob Arum aliwahi kusema Terence Crawford angeweza kumshinda Mayweather, lakini wawili hao hawakuwahi kukutana.
Hata hivyo, sasa bingwa wa zamani wa dunia, James Toney ametaja jina la Chavez kama bondia ambaye angemzuia Mayweather kustaafu bila kupoteza.

Alipoulizwa kama Mayweather ndiye bondia bora zaidi wa wakati wote, Toney alijibu kwa ukali: "Sio kweli. Haiingii kwenye enzi yangu... hakupigana na mabondia wa miaka ya '90 aliwasubiri wastaafu ndipo aanze kupigana. Hakupigana na Chavez. Asingemuweza. Hatton hakuwa chochote. Takataka. Alimshinda Canelo.”
Chavez, nyota wa Mexico ni mmoja wa mabondia wanaoheshimika duniani ambaye enzi zake alishinda mataji ya dunia katika uzani mtatu tofauti na aliweka rekodi ya kutetea taji lake mara 27 mfululizo kabla ya kustaafu akiwa na mapambano 115 – zaidi ya mara mbili ya idadi ya Mayweather.

Ingawa alishindwa mara sita, Chavez aliwahi kupigana na Oscar De La Hoya na kupoteza mara mbili, huku Mayweather akimshinda De La Hoya katika pambano la mwaka 2007.

Akizungumzia suala hilo, Chavez mwenyewe alikubaliana na kauli ya Toney akisema: “Katika kilele cha uwezo wetu lingekuwa pambano gumu. Lakini naamini kwenye uzani wa kilo 60 ningemshinda Mayweather. Huo ndio uzani wangu wa asili.”
“Uzani wa 80 haukunifaa. Nilipigania ubingwa lakini siyo uzani wangu halisi. Na kumbuka nilipigana na mjomba wake (Mayweather) ambaye ndiye aliyemfundisha. Hiyo ni sababu nyingine kwa nini naamini ningemshinda.”
Wakati fulani Mayweather aliwahi kusema angemkalisha hata Chavez iwapo wangekutana ulingoni, kwani mabondia aliowahi kupigana nao walikuwa wa viwango vya juu kuliko aliowachapa Chavez.

"Wakati mwingine wanasema, 'Julio Cesar Chavez alipigana mapambano 89 bila kupoteza.' Mimi nimewashinda mabingwa wengi zaidi kuliko yeye katika mapambano yake zaidi ya 100. Halafu wanazungumza kuhusu Sugar Ray. Tena, mimi nimewashinda mabingwa wengi zaidi kuliko Sugar Ray katika taaluma yake ya kuvutia."
Lakini, mwisho wa siku ni Mayweather aliyestaafu bila doa lolote kwenye rekodi yake ya mapambano ya kulipwa.