Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matukio tata Simba, Yanga yanavyoishia uwanjani

UTATA Pict

Muktasari:

  • Akiwa ndani ya eneo la penalti na bila ya kuzongwa na yeyote, Double R aliinama na kuudaka mpira uliokuwa unaenda kwake. Hapohapo alisikia refa akipuliza filimbi na aliponyanyua uso kumwangalia, aliona anaelekeza kidole eneo la penalti kuashiria adhabu hiyo kubwa.

INGEKUWA ni vigumu sana kuelewa maelezo ya beki wa zamani wa Yanga, Rajab Rashid, maarufu kwa jina la Double R, baada ya kusababisha penalti mwanzoni mwa mchezo dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru). Tukio hilo lilitokea katika mechi iliyopigwa Oktoba 20, 1990.

Akiwa ndani ya eneo la penalti na bila ya kuzongwa na yeyote, Double R aliinama na kuudaka mpira uliokuwa unaenda kwake. Hapohapo alisikia refa akipuliza filimbi na aliponyanyua uso kumwangalia, aliona anaelekeza kidole eneo la penalti kuashiria adhabu hiyo kubwa.

Rashid, ambaye ndiye kwanza alikuwa anaanza kubeba majukumu makubwa katika ngome ya Yanga, alishikwa na butwaa, lakini hakuwa na uwezo wa kubishana na uamuzi wa refa kwa kuwa ni dhahiri aliukamata mpira na ingekuwa kwa sheria za siku hizi, alitakiwa aonyeshwe kadi ya njano.

Double R aliudaka mpira akidhani refa alikuwa amepuliza filimbi, lakini alikuwa amesikia mawenge na si filimbi halisi. Ilikuwa ni penalti halali. Bahati yake ni Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’ aliyepewa jukumu la kupiga penalti hiyo alikosa.

Lakini Mungu mkubwa zaidi kwake, Simba hawakuibadilisha penalti hiyo kuwa goli, lakini na wapinzani wao wakamaliza mchezo kwa ushindi wa mabao 3-1, mabao ya Yanga yakifungwa na Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ a.k.a Bongabonga dk 33, Thomas Kipese ‘Uncle Tom’ dk 82 na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ dk 89, huku Edward Chumila ‘Edo Boy’ akiifungia Simba la kufutia machozi dk 58.

Tafsiri ya haraka sana ingekuwa Double R alifanya makusudi ili kuinufaisha Simba, lakini hilo halikutokea baada ya ushindi huo mnono.

UTA 01

Kwa tafsiri ya sasa, hata kama Yanga ingeibuka na ushindi huo, bado ingeonekana Double R alifanya kitu fulani kwa makusudi. Kwanza kabisa ni kuchukua mlungula kutoka kwa wapinzani, lakini pili ni utamaduni wa sasa wa wachezaji kucheza michezo ya kubashiri (betting) matokeo hata kwa mechi wanazoshiriki.

Angeweza kudhaniwa aliweka donge nono kwa ushindi wa Simba, au katika bao la kwanza au la kusawazisha au tukio jingine lolote.

Hilo ni tukio moja kati ya mengi tata ambayo hutokea katika mechi za Simba na Yanga zinazofuatiliwa na mamilioni ya mashabiki wa soka wa Tanzania, Afrika Mashariki na sehemu kubwa ya Bara la Afrika.

Lakini uzuri ni matukio haya hayajawahi kuhusishwa na tuhuma nzito za upangaji matokeo, ingawa baadhi yameshughulikiwa ndani ya klabu kwa mrengo huo wa tuhuma za kupanga matokeo bila ya wahusika kutoa taarifa rasmi zinazothibitisha uwepo wa uovu huo.

Pengine ni viongozi ambao huchukua muda mrefu kuyasahau matukio hayo, lakini mashabiki huyakubali mapema na kuendelea na utani wao wa jadi, hata kama ni mara tu baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa.

UTA 02

Wakati Yanga ikijitutumua kurejesha ufalme wake baada ya kuukosa ubingwa wa Bara kwa miaka mitatu, ilipigwa na kitu kizito kichwani mjini Kigoma katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Ndiyo kwanza mechi ilikuwa inaanza kuchangamka kipindi cha kwanza, wakati wa chini kiungo Mukoko Tonombe alipopata mpira huku akizongwa kwa nyuma na mshambuliaji wa Simba, John Bocco.

Ghafla Tonombe aligeuza mkono wake wa kulia na kumpiga kwa kiwiko Bocco, ambaye hakuwa anaweza kuupora mpira.

Tonombe alipewa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi, na Yanga ikipoteza mchezo huo kwa mabao 2-1, bao la ushindi likifungwa dakika ya mwisho kutokana na mpira wa kona.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mwisho wake Yanga kwa Mukoko Tonombe, kiungo aliyeshika vyema sehemu ya kiungo kutokana na utulivu wake, uwezo wa kumiliki mpira, matumizi ya nguvu na pumzi ya kuzunguka uwanja mzima kusaidia wenzake.

Habari zinasema shughuli zake kabla ya mechi hiyo zilianza kutoeleweka, hadi mchezaji mwenzake waliyekuwa wakiishi chumba kimoja alilazimika kumuuliza kilichokuwa kinaendelea.

Hakuna taarifa rasmi iliyotoka klabuni na Tonombe akauzwa TP Mazembe. Inaonekana nyota huyo hapewi heshima kama mchezaji gwiji aliyewahi kupitia klabu hiyo.

Jonas Mkude, akiwa tegemeo katika nafasi ya kiungo Simba, alijikuta akipewa kadi nyekundu dakika ya 26 ya mechi ya watani hao wa jadi. Alikuwa akipinga bao lililofungwa na Amissi Tambwe pembeni ya uwanja. Picha za marudio zilionyesha kama Tambwe aliugusa mpira kwa mkono wakati akiutuliza kabla ya kufunga.

UTA 03

Mkude alimsukuma refa hadi akaanguka. Lakini tukio tata ambalo bado linazungumzwa hadi sasa ni picha zinazoonyesha Tambwe akiudhibiti mpira kwa mkono (ingawa kuna uchache wa kamera kuthibitisha hilo bila ya shaka) na kuujaza wavuni.

Refa wa mchezo huo hakuingia katika tuhuma za kula rushwa ili kuipendelea Yanga na pengine ni kutokana na mechi hiyo ya Oktoba Mosi, 2016 kuisha kwa sare ya bao 1-1.

Lakini mashabiki wa Simba na Yanga hawatakuja kuzisahau mechi mbili zilizohusisha timu zote kufunga mabao mengi. Ya kwanza ilikuwa ni sare ya ajabu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha ambako timu hizo zilifungana mabao 4-4. Ilikuwa ni funga nikufunge, Simba wakitangulia kufunga hadi bao la tatu na baadaye Yanga kuchukua usukani mwishoni.

Sanifu Lazaro alifunga bao la nne, lakini wakati Yanga wakijihesabia ushindi mwingine msimu huo, Duah Said akaisawazisha Simba dakika za majeruhi. Yanga ilimaliza Ligi Kuu ikiwa na pointi 44 na Simba 38.

Unaweza kuchukulia kuwa matokeo ya mchezo huu yalipangwa. Yanga iliingia uwanjani ikihitaji sare itangazwe kuwa bingwa mpya baada ya Simba kutwaa kwa miaka miwili mfululizo. Simba, ambayo ilishakuwa na sare 10 na kupoteza mechi mbili, ilihitaji ushindi kuipiku Yanga, lakini ikajikuta ikitafuta sare mwishoni mwa mchezo.

Hakukuwa na tuhuma za upangaji matokeo zilizofuata baada ya sare hiyo kubwa kwa vigogo hao wa Kariakoo. Si penalti wala bao la kujifunga la beki Mustafa Hoza lililotiliwa shaka.

Abdi Banda, beki wa Dodoma jiji aliyewahi kucheza soka Afrika Kusini, naye yumo katika matukio tata ya mechi za watani wa jadi. Katika mchezo wa Februari 20, 2016, Banda alionyeshwa kadi mbili za njano ndani ya dakika tano na hivyo kuonyeshwa njia ya kutoka uwanjani.

UTA 04

Alimchezea rafu Donald Ngoma wa Yanga dakika ya 21 na mwamuzi Jonesia Rukiyaa hakuona ajizi kumwonyesha kadi nyingine ya njano dakika ya 25 baada ya kurudia kumchezea rafu Ngoma.

Kimpira matukio hayo ni ya kawaida kwa wanamichezo, lakini utata huja pale yanapoonekana kufanyika bila ya kujali uzito wa mechi unavyochukuliwa na mashabiki pamoja na viongozi.

Mara kadhaa wachezaji wanaotuhumiwa kuhujumu timu, hufanya matukio kama hayo ya kadi nyekundu ndani ya muda mfupi kuvutia hasira za refa ili amuadhibu vikali, lakini Banda hakuingizwa kwenye wasiwasi huo.

Matukio ya refa kutoa penalti tata au mchezaji kutoa penalti rahisi pia huvuta hisia za upangaji matokeo, lakini kwa Simba na Yanga, hilo hufanyika kisiri sana.

Nyakati matukio hayo yanatokea ilikuwa vigumu kumhusisha mchezaji au refa na masuala ya kamari wala upangaji wa matokeo, lakini kwa jinsi kampuni za kubeti zilivyoongeza teknolojia na kuwafikia watu mikononi, huku zikitenga madonge manono kwa washindi, hali sasa si ya kuichukulia kwa urahisi, kama wasiwasi ulioanza kuonyeshwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu wachezaji na waamuzi kushiriki kubeti.

Katika kashfa ya upangaji matokeo Ujerumani, refa Robert Hoyzer na mwenzake Dominik Marks walijipatia takriban Euro 24,000 kila mmoja baada ya kupanga au kujaribu kupanga matokeo ya mechi 13, huku raia wa Croatia aliyetumiwa na magenge ya kamari ya barani Asia akitengeneza takriban Euro 1 milioni.

Haijulikana kama mtandao wa magenge hayo umeshafika hadi Afrika Mashariki, ambako kwa sasa Yanga na Simba ndio timu zinazofuatiliwa kwa karibu nusu ya watu milioni 500 walio ukanda huu.

Katika matukio mengine, timu hizo mbili pia zimewahi kugomea mechi kwa nyakati tofauti. Mwaka 1985, Simba iligomea kurejea uwanjani kipindi cha pili cha mchezo wao wa Ligi ya Muungano, Simba ilidai baadaye mwamuzi Hafidh Ali kutoka Zanzibar alikuwa akiwaambia ni lazima wafungwe na hata ilipoonekana wanacheza rafu. Inadaiwa refa huyo aliwasisitizia hangemtoa mchezaji hata mmoja kwa kuwa alitaka aone Simba ikifungwa ikiwa kamili.

Yanga iligomea mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa Kombe la Kagame dhidi ya Simba, ikitaka ilipwe kwanza Sh30 milioni  kabla ya kupeleka timu uwanjani.

Matukio haya tata huwa hayaangaliwi wakati wa matayarisho ya mechi za watani hao wa jadi ambazo hujaa mambo mengi.

Kutokana na mabadiliko ya kanuni, ni vigumu sana kwa siku hizi klabu kugomea kwenda uwanjani, huku kuundwa kwa kamati ya maadili kukizuia wengi kufanya vituko vinavyoweza kutafsiriwa kuwa ni upangaji matokeo japokuwa suala hilo ni gumu kulithibitisha.

Hata hivyo, mechi ya watani, ni ya watani. Lolote laweza kutokea ama kwa kupangwa, kwa bahati mbaya ama kwa kusudio la mchezaji au mwamuzi kutokana na masilahi binafsi.

Hivyo, usijekushangaa kuona kadi nyekundu ikitoka ndani ya dakika 10 za kwanza, au mchezaji akifanya rafu mbili mbaya ndani ya muda mfupi, au hata kosa linaloweza kusababisha penalti kama la Double R.

Mchezo kumalizika huku tukio moja au mawili kama hayo kutokea na baadaye kutochukuliwa hatua zozote na wahusika ndiyo mambo yanayofanya mchezo huo kuwa wa watani wa jadi hasa.

Jukwaani, mashabiki waliovalia nguo za rangi nyekundu na nyeupe huungana na waliovaa kijani na njano kupanda bodaboda, bajaj au daladala kurudi makwao.