Mastraika Zenji wanavyokumbana na upepo mbaya Bara

Muktasari:
Baadhi ya nyota hao, wamefanya vizuri kwa mfano Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyetoka KVZ FC akiwa mfungaji bora msimu wa 2023-2024, baada ya kufunga mabao 20 na kuasisti saba katika mechi 27 alizocheza kati ya 30 za kikosi hicho msimu mzima.
KUMEKUWA na wimbi kubwa la washambuliaji waliofanya vizuri Ligi Kuu ya Zanzibar na kubeba tuzo ya ufungaji bora, ingawa baadhi yao wanapojiunga na timu za Ligi Kuu Bara hali inakuwa tofauti na ilivyokuwa matarajio ya mashabiki.
Baadhi ya nyota hao, wamefanya vizuri kwa mfano Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyetoka KVZ FC akiwa mfungaji bora msimu wa 2023-2024, baada ya kufunga mabao 20 na kuasisti saba katika mechi 27 alizocheza kati ya 30 za kikosi hicho msimu mzima.
Kiwango hicho, kikamfanya kusajiliwa na Singida Black Stars msimu huu, ingawa alitolewa kwa mkopo kwenda Fountain Gate na kufunga mabao sita ya Ligi Kuu Bara, kisha dirisha dogo la Januari 2025, akajiunga na Wydad Casablanca ya Morocco.
Huenda nyota huyo angeendelea kufanya vizuri kutokana na kiwango alichokionyesha tangu mwanzo wa msimu huu, ingawa kwa nyota wenzake waliowika Ligi Kuu ya Zanzibar wamekuwa na wakati mgumu Ligi Kuu Bara, kama Mwanaspoti linavyowaelezea.

MUDRIK ABDI SHEHE ‘GONDA’
Baada ya kuondoka Seleman Mwalimu ‘Gomez’ katika kikosi cha Fountain Gate, mabosi wa timu hiyo wakamsajili, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’, kutoka JKU ya Zanzibar dirisha dogo la Januari 2025, kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha.
Usajili wa nyota huyo, ulikuwa kwa ajili ya kuziba nafasi ya ‘Gomez’, baada ya kufunga mabao manane akiwa na kikosi cha JKU, japo tangu amejiunga na timu hiyo, ‘Gonda’ ameshindwa kabisa kuonyesha makali yake akiwa pia hajafunga bao lolote.
Ujio wake, ulikuwa kwa ajili ya kutengeneza pacha kali ya ushambuliaji na nyota mwenzake, Edgar William aliyekuwa hatari zaidi wakati akicheza na ‘Gomez’, ingawa hadi sasa imeshindikana, licha ya matarajio makubwa ya mashabiki wa timu hiyo.

MAABAD MAULID
Mshambuliaji Maabad Maulid ni nyota mwingine aliyefanya vizuri akitokea Zanzibar na kiwango bora alichokionyesha kikawavutia mabosi wa Coastal Union, japo licha ya uwezo wake mzuri wa kufunga ila imekuwa ni tofauti na Ligi Kuu Bara.
Maabad alijiunga na kikosi hicho Julai 11, 2022, akitokea KVZ FC ya Zanzibar na alikuwa pia mfungaji bora mara mbili mfululizo, akianza na msimu wa 2020-2021, alipofunga mabao 17, kisha na msimu uliofuata wa 2021-2022, akafunga mabao 21.
Licha ya rekodi hiyo bora kwake, ila tangu amejiunga na Coastal Union hajawahi kufikisha hata mabao 10 ya Ligi Kuu Bara, kwa sababu msimu wake wa kwanza wa 2022-2023, alifunga mabao manne na msimu uliopita wa 2023-2024, alifunga matatu tu.
Msimu huu wa 2024-2025, tayari nyota huyo amefunga mabao matano, huku bao la mwisho kufunga lilikuwa la ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1, dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Februari 7, 2025.

YASSIN MGAZA
Nyota mwingine ni Yassin Mgaza ambaye pia alikuwa mfungaji bora katika Ligi ya Zanzibar akiwa na kikosi cha KMKM msimu wa 2022-2023 na alichangia mabao 25, baada ya kufunga 17 na kuasisti manane kwenye mechi 25 kati ya 30, alizocheza.
Mgaza alijiunga na KMKM akitokea Mbuni ya Arusha ambayo kwa sasa inashiriki Ligi ya Championship, ingawa kwa msimu huo ilikuwa Ligi Daraja la Pili, First League na alionyesha kiwango kizuri kilichoishawishi KMKM kuihitaji saini yake.
Akiwa na Mbuni, Mgaza alihusika katika jumla ya mabao 22 kwa msimu mzima kwenye mechi 16, alizocheza, baada ya kufunga mabao 16 na kuasisti mengine sita, ingawa kiwango hicho bora kwake alikiendeleza hadi alipojiunga na kikosi cha KMKM.
Baada ya hapo, mabosi wa Dodoma Jiji wakamsajili kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kwa msimu wa 2023-2024 na kubeba matarajio makubwa ndani ya kikosi hicho, ingawa aliangukia pua baada ya kufunga mabao matatu tu msimu mzima.
Msimu huu wa 2024-2025, Mgaza amefunga bao moja tu lililokuwa la kichapo ilichokipata Dodoma Jiji cha mabao 2-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Uwanja wa CCM Liti Singida, Desemba 12, 2024.

IBRAHIM HAMAD HILIKA
Hilika ni miongoni mwa washambuliaji bora waliofanya makubwa katika Ligi ya Zanzibar, japo kwa upande wa Ligi Kuu Bara, nyota huyo ameshindwa kuonyesha makali yake, licha ya kuzichezea timu mbalimbali za, Polisi Tanzania na Mtibwa Sugar.
Mshambuliaji huyo, alijizoelea umaarufu mkubwa wakati akiichezea Zimamoto ya visiwani Zanzibar na alikuwa mfungaji bora mara mbili, akianza msimu wa 2016-2017 alipofunga jumla ya mabao 33, kuanzia Ligi ya Kanda hadi hatua ya nane bora.
Katika Kanda ya Unguja, Hilika alifunga mabao 19 msimu huo, huku kwenye hatua ya nane bora nyota huyo alifunga jumla ya mabao 14, hivyo kuhitimisha msimu kibabe kwa kufunga 33, hali iliyovutia timu mbalimbali zilizohitaji kupata saini yake.
Msimu mwingine wa 2019-2020, nyota huyo akaendeleza balaa akiwa na kikosi hicho cha Zimamoto na alifunga jumla ya mabao 20, akimpita bao moja tu mshambuliaji wa kikosi cha JKU, Shehuu Magaji Buwa aliyehitimisha msimu huo na mabao 19.
Kabla ya Hilika kuibuka mfungaji bora, msimu uliopita wa 2018-2019, nyota wa Zimamoto, Abubakar Khamis Sufiani ‘Kabela Kanu’ na Mussa Ali Mbarouk wa KMKM FC, wote walikuwa wafungaji bora wa Ligi hiyo baada ya kufunga mabao 23, kila mmoja.
Licha ya rekodi tamu kwa Hilika, ila nyota huyo ameshindwa kuonyesha makali yake katika Ligi Kuu, baada ya kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo za Mtibwa Sugar, maafande wa Polisi Tanzania na hadi sasa pia Tabora United ‘Nyuki wa Tabora’.
Hilika hadi sasa hajafunga bao lolote la Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho cha Tabora United, huku pia hata nafasi ya kucheza mara kwa mara ikiwa ni finyu, kutokana na ushindani wa eneo la ushambuliaji linaloongozwa na Heritier Makambo.
MSIKIE GONDA
Akizungumzia kiwango chake msimu huu na Fountain Gate, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’, anasema Ligi ya Bara ni ngumu tofauti na ya Zanzibar, ingawa kadri anavyoendelea kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza inazidi kumwongezea morali zaidi.
“Nimeingia katika dirisha dogo na ukiangalia presha kutokana na mwenendo wa timu ni mkubwa hivyo, isingekuwa pia rahisi kuendana na ushindani sehemu ambayo sijaizoea, naamini msimu ujao nitakuwa bora zaidi ya nilichoonyesha,” anasema Gonda.
Mshambuliaji huyo, anasema haamini washambuliaji waliofanya vizuri Zanzibar wamefeli kabisa kama wengi wao wanavyosema, ingawa muda mwingine wanakutana na upepo mbaya, hali inayosababisha kuhitaji muda zaidi wa kuzoeana na wengine kikosini.