Mastraika wa kigeni waliotisha VPL miaka 10

Friday January 15 2021
wakali pic
By Eliya Solomon
By Olipa Assa

KUNA chachu inayoletwa na wachezaji wa kigeni, katika Ligi Kuu Bara, ambao wamekuwa wakionyesha ushindani dhidi ya wazawa katika timu zao zilizowasajili dhidi ya wapinzani.

Kutokana na umuhimu wao, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilitoa baraka kusajiliwa wachezaji wakigeni 10, kutoka saba baada ya kikao cha bodi ya ligi, walileta mapendekezo ya kanuni mbalimbali kwa kamati ya utendaji ya TFF, ili yapitishe, moja ya mapendekezo yao yalikuwa ni mabadiliko ya kanuni ya 57.

Kanuni hiyo walipendekeza wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi 10, mapendekezo ya kanuni yalijadiliwa katika kikao cha utendaji ya TFF, wakakubaliana hoja za klabu na kupitisha maombi hayo.

Mwanaspoti linakuchambulia kwa uchache orodha fupi ya washambuliaji wa kigeni, ambao wametoa changamoto kwa wazawa ndani ya miaka 10 ya hivi karibuni lakini pia hii ni njia ya kuthamini michango yao.


EMMANUEL OKWI-SIMBA

Advertisement

Raia huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 27 kwa sasa anachezea Al Ittihad ya Misri ambayo alijiunga nayo mwaka jana akitokea Simba.

wakali okwi

Katika kipindi ambacho Okwi amecheza soka la kulipwa hapa nchini, ameweza kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu akiwa na Simba lakini pia kuvaa medali ya ushindi ya Kombe la Mapinduzi.

Aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa mechi ya Nani Mtani Jembe msimu wa 2014/2015 lakini pia msimu wa 2018/2019 aliweza kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Simba.


AMISSI TAMBWE -SIMBA/ YANGA

Alikuja nchini mwaka 2013 kujiunga na Simba na baada ya kuichezea kwa msimu mmoja, alitimka zake na kujiunga na Yanga.

wakali tambwe pic

Katika muda wote aliocheza Tanzania, ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu zote akiwa na Yanga kuanzia msimu wa 2014/2015 hadi msimu wa 2016/2017 huku pia akitinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili akiwa na Yanga.

Mbali na hayo, amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili tofauti ambazo ni msimu wa 2013/2014 na 2015/2016 na katika kipindi chote alichocheza Tanzania amefunga mabao 75 katika mashindano mbalimbali.


KIPRE TCHECHE -AZAM

Alijiunga na Azam FC mwaka 2011 akitokea kwao Ivory Coast alikokuwa akiitumikia timu ya JC Abidjan na baada ya hapo akaitumikia klabu hiyo kwa miaka sita hadi 2017 alipotimkia Al Nahda ya Oman.

wakali tcheche pic

Katika kipindi alichoichezea Azam, Kipre alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara moja, ubingwa wa Kombe la Kagame mara moja na Kombe la Mapinduzi mara mbili.

Amewahi kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2013/2014 na pia amewahi kuwa Mfungaji Bora wa Ligi hiyo ya msimu wa 2012/2013, mpaka anaondoka nchini rekodi zinaonyesha jamaa alifunga zaidi ya mabao 50.


MEDDIE KAGERE-SIMBA

Straika wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere hadi sasa amefikisha jumla ya mabao 52, msimu wake wa kwanza 2018/19 alimaliza akiwa kinara kwa mabao 23, uliofuata 22 na sasa ana saba. Alitwaa mara mbili mfululizo tuzo ya ufungaji bora VPL.

wakali kagere

Jumla ya mabao 52 ni ya Ligi Kuu Bara, nje na mashindano mengine ambayo Simba ilishiriki kama Ligi ya Mabingwa, Kombe la FA, Mapinduzi na mechi za kirafiki. Amekuwa sehemu ya mafanikio ya Simba kwa kutwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi, hii ni awamu yake ya pili kuisaidia timu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


BONIFACE AMBANI -YANGA

Straika wa zamani Mkenya Boniface Ambani, Julai 2008 alijiunga na klabu ya Yanga, ambapo katika mechi 16 za msimu huu alifunga mabao 15 ya Ligi Kuu Bara. Anatajwa kuwa mmoja wa washambuliaji hatari wa kigeni waliowahi kucheza VPL ndani ya miaka 10 ya hivi karibuni.

Inaelezwa kipindi anacheza ligi ya Tanzania, alikuwa na uadui na nyavu, hivyo mabeki walikuwa na kazi ya kumkaba kuhakikisha aachi madhara.

Amewahi pia kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2008-2009 kwa kufunga mabao 18.


BLAISE BIGIRIMANA - NAMUNGO

Ni kati ya wachezaji wa kigeni, maisha yake yalianzia Stand United, ilivyoshuka Daraja, ambapo msimu ulioisha alimaliza akiwa na mabao 10, pia amewahi kuzifunga Simba na Yanga katika mechi za Ligi Kuu Bara.


PRINCE DUBE -AZAM

Straika wa Azam FC, Prince Dube ameanza ligi kwa kasi kabla ya kuumia bega la mkono wake wa kulia, wakati wa mechi ya raundi ya kwanza na Yanga, iliyopigwa Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamanzi nje kidogo wa jiji la Dar es Salaam.

Kabla ya kuumia Dube, alikuwa amefunga mabao sita na alitawala vyombo vya habari vikimuelezea umalidadi wake wa kucheka na nyavu.


DAVID MOLINGA -YANGA

Ndani ya msimu mmoja ambao alicheza Yanga, David Molinga alifunga mabao 13 katika mashindano yote, jina lake lilikuwa kubwa mbele ya mashabiki wa soka, kutokana na mwili wake na aina ya upigaji wake wa faulo, ambapo alikuwa anarudi nyuma kama Cristiano Ronaldo.

molinga wakali pic


HERITIER MAKAMBO-YANGA

Nyota ya straika wa zamani wa Yanga, ilikuwa na kibali mbele ya mashabiki wa timu hiyo, aliondoka kiwango chake kikitikisa na hata alipowaaga katika mechi na Mbeya City, wengi wao hawakuamini kama anaondoka.

wakali makambooo pic

Licha ya kwamba Makambo, hakumaliza msimu wa mwakajuzi, alifunga mabao 17 akiwaachia mashabiki wa Yanga, staili ya kushangilia kwa kuwajaza.


DONALD NGOMA - YANGA/ AZAM

Msimu wake wa kwanza wa 2015/16 Yanga, straika Mzimbabwe Donald Ngoma alifunga mabao 19 ya mashindano yote na alikuwa kwenye kiwango cha juu zaidi, kabla ya kupatwa na majeraha yaliomuweka nje kwa muda mrefu, kisha kutimkia Azam.

wakali ngoma pic

Tangu ajiunge na Azam FC, mwaka 2018 hadi alipoondoka 2020 alifunga jumla ya mabao 20 kwenye mechi 42 ya mashindano yote, ingawa kipindi cha mwisho hakuwa na kiwango cha juu kilichozoeleka.

Advertisement