Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MASTORI YA OSCAR: Kuna shida gani kwa Fiston Mayele?

HATUWEZI kuwakuza wachezaji wetu wazawa, kwa kuwachukia wachezaji wageni. George Mpole amekuwa mfungaji bora wa ligi iliyomalizika hivi karibuni nchini kwetu Tanzania. Pongezi nyingi sana kwake.

Unapocheza timu nje ya Simba na Yanga zenye miundombinu bora kuliko nyingine nchini, kuibuka kinara sio jambo dogo.

Kwa mara nyingine nimehisi chuki kwa mchezaji wa kigeni kwenye mpira wetu, Fiston Mayele kutoka Jamhuri ya Kidomokrasia ya Congo ni mchezaji wa Yanga. Amekamata nafasi ya pili akiwa na mabao 16 dhidi ya yake 17 ya Mpole ambaye ni mzawa.

Kumekuwa na kundi kubwa la watu kabla hata ligi haijaisha wakifurahia kila Mayele alipokuwa akizidiwa mabao na Mpole. Ukiniuliza sababu ni nini? Sina majibu. Kuna muda nawaza, labda ni chuki binafsi tu. Zinasababishwa na nini? Sina jibu.

Sio mara ya kwanza kwa Ligi ya Tanzania kutoa mfungaji bora mzawa. Wamewahi kushinda kina Simon Msuva, John Bocco, Mrisho Ngassa, Mussa Hassan Mgosi na wengine wengi. Sio mara ya kwanza mfungaji bora kuwa mchezaji wa kigeni. Wameshakuwa kina Meddie Kagere, Amis Tambwe na wengine wengi.

Ukiniuliza tatizo ni nini msimu huu hadi watu wamekuwa na makasiriko kwa Mayele? Sina Jibu. Labda ni chuki tu za kibinadamu.

Nimesikitisha sana kuona hadi ndugu zangu wa damu nao baadhi wakiingia kwenye mkumbo huo. Waandishi wa habari za michezo nao wameanza kampeni ya kuchangishana pesa eti za kumpa motisha Mpole.

Nimewahi kumsikia mheshimiwa mmoja akisema Mayele arudi kwao DRC akapigane vita badala ya kuendelea kutetema hapa nchini. Hii ni chuki ya wazi wazi tunayoionyesha dhidi ya wachezaji wa kigeni. Sina nia ya kuwakosea heshima ndugu zangu waandishi wa habari za michezo hapa nchini lakini, kumkandamiza Mayele hakutomwinua Mpole.

Kama tunadhani wachezaji wetu wazawa ni bora zaidi ya wageni, tuwaombe Shirikisho la Soka nchini (TFF) waondoe kanuni ya kurusu wageni kuja. Ndugu zangu, Waingereza pamoja na kupenda wachezaji wao, pale Manchester City sanamu zao za heshima za mwisho ni za Vincent Kompany (Mbelgiji), David Silva (Mhispania) na Kun Aguero (Muajentina).

Kuna muda unafika ni lazima mafuta na maji vitengane! Wachezaji wetu wazawa bado wana safari ndefu sana ya kujifunza kutoka kwa wachezaji wa kigeni. Kuna muda tunawapa ukubwa wasio stahili na matokeo yake wanaishia njiani.

Msimu wa 2024/2015 tuliwahi kumpa Tuzo ya kocha bora, Mbwana Makata na kumnyima Hans Van der Pluim. Sababu zilikuwa hizi hizi za kumbeba mzawa. Msimu wa 2020/2121 tuliwahi kumpa Tuzo ya Mchezaji Bora wa FA, Feisal Salamu ambaye alizidiwa kila kitu na Luis Miquessone.

Hatuwezi kuwakuza wachezaji wetu wazawa kwa kuwaumiza wachezaji wa kigeni! Ni kweli Mpole amekuwa mfungaji Bora lakini tusitumie nguvu kubwa kuumiza kihisia wachezaji wa kigeni.

Kuna mambo yanapaswa kuendelea kufanywa na mashabiki na sio sisi Waandishi. Ningesikia mashabiki wa Geita Gold FC wamemchangia pesa Mpole, nisingeshangaa. Ningewapongeza.

Ningesikia Uongozi wa Geita wameamua kumnunulia mchezaji wao Range Rover, ningefarijika sana. Kazi ya uandishi wa habari sio kutoa motisha kwa mchezaji mzawa. Kazi za utangazaji sio kumfia mchezaji mzawa na kumkandamiza wa kigeni.

Nadhani kazi za kutoa motisha sisi kama wana habari sio majukumu yetu. Hatuwezi kuwakuza wachezaji wetu wazawa kwa kuwakandamiza wachezaji wa kigeni.

Ligi yetu inaonekana kupiga hatua mbele lakini bado wachezaji wetu wazawa wana safari ndefu. Kila msimu mpya unapokwisha wachezaji wa kigeni ndiyo wanaongoza kwa kutakiwa na klabu nyingine kubwa Afrika.

Wakati tunadhani Feisal ni bora kuliko Luis, matokeo yake Luis yuko Ligi ya Misri na Fei yuko hapa hapa. Tuwasaidie wachezaji kuwa wakubwa bila kuwaumiza wachezaji wa kigeni.

Hakuna siku wachezaji wetu wazawa watakuwa wakubwa kwa kuwaumiza wa kigeni. Kama mshindani wa Mpole angekuwa mchezaji mwingine, sidhani kama watu wangehangaika na michango ya motisha.

Kama washindani wa ufungaji bora wangekuwa wote wazawa, sidhani kama mchango wa motisha ungekuwepo. Mpole ndiye mfungaji bora lakini bado ana mengi ya kujifunza kutoka kwa Mayele.

Naitwa Baba Mzungu, kama una lolote nitumie ujumbe mfupi wa maandishi kupitia 0789-784858 au tukutane Instagram @oscaroscarjr au Twitter @mzeewakaliua